Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Jumba la kifahari ni uthibitisho wa rushwa?

49122 Edo+Kumwembe

Thu, 28 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Inafikirisha kidogo. Juzi katika taarifa za habari tukaonyeshwa wakubwa wa mambo ya kuzuia rushwa wakiwa katika hekalu moja la mtu anayetuhumiwa kwa rushwa. Walizurura kweli. Ni hekalu kubwa.

Katika tafsiri ya haraka ilionekana mtuhumiwa alikuwa anajihusisha na mambo ya rushwa na ndio maana amejenga jumba zuri la kifahari. Hii ndiyo ilikuwa tafsiri ya tulichoonyeshwa. Inachekesha kidogo. Bado tunatumia mawazo ya kimaskini kuujadili utajiri.

Kwamba ukiwa na jumba la kifahari basi fedha zako zimepatikana kwa kuiba au kula rushwa? Sio sawa. Inawezekana ni kweli mtuhumiwa amekula rushwa, lakini sio matokeo ya ujenzi wa jumba la kifahari. Kuna wengine wanakula rushwa kubwa na hawajengi majumba ya kifahari.

Kitu cha msingi ni mashtaka yanayomkabili. Kuna watu wanajipenda zaidi. Wanaweza kujenga nyumba ya kifahari wakati wana maisha ya kawaida. Wanapeleka kila walichonacho katika ujenzi. Tunaishi nao mitaani watu wa namna hii.

Kuna watu wana magari ya kifahari na hawana sehemu nzuri za kulala. Kuna watu wana majumba ya kifahari na hawana magari. Pia, kuna watu wana dili nzuri nje ya kazi zao za kawaida na wanaweza kujenga nyumba za kifahari.

Kuthibitisha ulaji rushwa wa mtuhumiwa kwa sababu ya ujenzi wa nyumba yake ya kifahari sio sawa. Kama aliachiwa fedha nyingi za urithi toka kwa wazazi wake? Inawezekana ni kweli amehusika na rushwa lakini ujenzi wa jumba lake la kifahari haukutokana na fedha hizo.

Wakati mwingine watuhumiwa kama hawa huponyoka katika mikono ya sheria pindi linapokuja suala la kuthibitisha kwamba fedha zao za rushwa ndizo ambazo zilifanikisha ujenzi wa nyumba hizo. Rushwa haina risiti.

Pia, tusiwafanye watu wanaotamani kujenga nyumba za thamani wasifanye hivyo. Wananchi lazima waishi maisha mazuri. Ni kitu cha kawaida. Ujamaa umetuachia hasira dhidi ya matajiri. Wakati mwingine inashangaza ni kwa nini chuki hiyo imerudi tena. Kila mwenye jumba la kifahari anaonekana fisadi.

Tuache kuonyesha majumba ya kifahari au magari ya kifahari kama kielelezo cha mashtaka. Tupeleke mashtaka ya msingi, watu wapate wanachostahili, ama kwenda jela, kuachiwa huru au kufilisiwa kwa misingi ya sheria.



Columnist: mwananchi.co.tz