Baada ya kutesa uswahilini kwa muda mrefu tangu atinge magwanda, hatimaye juzi nikasikia ‘braza’ Lazaro ametinga selo. Simzungumzii yule Lazaro wa Biblia. Namzungumzia braza Lazaro Nyalandu. Aliwahi kuwa mtu mzito katika utawala uliopita.
Kitaswira huku mtaani anaonekana kuwa mtu wa kimataifa, asiyegusika kirahisi. Tukasikia minong’ono kwamba hata vigogo waendesha nchi huwa wanamgwaya kutokana na ukaribu wake na wazungu wanaoziendesha hizi nchi za dunia ya tatu.
Braza amekaa sana uswahilini tangu atinge magwanda. Nikaanza kuamini kwamba hagusiki. Ukizingatia kwamba karibu kila mpinzani amewahi kuwekwa katika zile kuta nne za Polisi. Juzi, nikasoma mahala kwamba yuko ndani. Mara kachukuliwa na watu wasiojulikana, mara kaenda kwa mabosi wazuia rushwa, mara kapelekwa kwa maafande.
Sijui kitakachofuata lakini nadhani hili nalo litapita. Hata hivyo, tunaelekea katika uchaguzi kwa hiyo nadhani hata kama hili litapita bado mengine yatakuja. Hapo ndipo tutajua kama amehamia rasmi upinzani au vinginevyo.
Wakati mwingine kunahitajika vipimo kama hivi kujua uimara wa moyo wako katika itikadi zilizopo. Kuna watu huwa unawajua kwa vipimo hivi. Pale unapoambiwa “vua mkanda, toa simu, weka hapo kaunta, ingia huku”.
Hapo ndipo unapoona mtu anatangaza kurudi alikokuwa zamani. Ni muhimu kwa braza kupitishwa katika mizani hii kujua uimara wake. Anaonekana kuwa mtu mwenye akili nyingi katika kuendesha mambo yake, lakini linapokuja suala la vipimo kama hivi ndipo unapojua ameingia upinzani au bado anadhani yupo upande uleule.
Pia Soma
- Nyalandu aripoti polisi, ahojiwa Takukuru
- Watumishi waliopandishwa madaraja Simanjiro watakiwa kuongeza juhudi
Wakati mwingine sio kwa kutembelea vituo vya polisi tu, bali hata kuzibwa kwa baadhi ya ‘vimifereji vya riziki’. Haya mambo mawili yakichanganywa pamoja ndipo unapopitishwa rasmi katika kundi la watu wenye roho ngumu ambao wanaweza kuaminika katika mapambano. Wengi wamevua magwanda na kuyasusa kabisa. Familia na maisha kwa ujumla yaliyumba bila kujali kama ana hatia au hana, lakini hicho ni kipimo cha kujua kama amehamia upinzani rasmi. Ndivyo ilivyo.