Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Ghafla nimemkumbuka Mzee wa Vijisenti

51213 Edo+Kumwembe

Wed, 10 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nimemkumbuka Mzee wa Vijisenti. Ghafla tu nimemkumbuka. Sio kila siku twende sawa na ‘topiki’ (mada) za nchi. Maisha yanaenda kasi. Nchi ina topiki nyingi. Ukitaka kwenda nazo sambamba unahitaji tuwe na magazeti ya asubuhi na jioni kama yale ya Alasiri na Dar Leo.

Nimemkumbuka tu Mzee wa Vijisenti. Yupo kimya. Nadhani atakuwa haelewi kinachoendelea nchini kwa sasa. Sio aina yake ya maisha. Nilikuwa namkubali kwa mambo mawili. Kwanza akili zake nyingi kichwani. Kwa sasa nadhani hatumii sana akili zake nyingi, hasa pale mjengoni. Mchezo umekuwa wa upande mmoja sana.

Mzee wa Vijisenti wakati ule wa Mama wa Njombe alikuwa anatumika kama akili kubwa ya upande wa pili. Kwa sasa naona yupo kimya. Nadhani bosi wa mjengoni anamaliza ubishi juu kwa juu. Wakati ule ‘mama’ alikuwa anamtupia kipaza sauti apambane na akina Lissu.

Mzee wa vijisenti nasikia kasoma Havard yule. Akina Lisu na kurukaruka kwao kote Mzee wa Vijisenti alikuwa anapambana nao kwa nguvu ya hoja kila siku. Kuna ile siku walipambana na Lissu mpaka usiku wa manane. Mama alikuwa kama refa wa pambano la ngumi tu. Anaamua, kisha anaamuru mechi iendelee. Mzee wa vijisenti alikuwa hatari sana.

Katika nyakati za hoja ya nguvu nadhani Mzee wa Vijisenti atakuwa anasinzia tu. Anaacha mambo yaende. Inatunyima raha sisi mashabiki wake. Nahisi nyakati hizi ‘akili kubwa’ nyingi zimeamua kususa. Zimekaa kimya. Nimemkumbuka Mzee wa Vijisenti.

Halafu kitu cha pili kilichosababisha nimkumbuke ni dili zake. Nadhani atakuwa ametulia tu. Yale madude makubwa yaliyokuwa yanaleta kesi kubwa hayapo kwa sasa. Nahisi Namba Moja ameyadhibiti. Zamani kila kesi kubwa ya mikataba usingeweza kumkosa Mzee wa vijisenti. Kilichokuwa kinatuacha mdomo wazi ni jinsi ambavyo usingeweza kumkamata. Alikuwa ananikosha sana.

Nadhani amestaafu katika mambo haya ya dili. Anataka kupumzika kwa amani. Ukimya wake ndani na nje ya mjengo umenifanya nimkumbuke sana. ‘Akili kubwa’ chache zinapokaa kimya tunakosa raha. Wengine ambao tumeishia darasa la saba tulikuwa tunajifunza mengi kupitia kwao. Nimemkumbuka sana. Sikuwa na lingine.



Columnist: mwananchi.co.tz