Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Ghafla Mwendokasi imekuwa mwendo wa kasi

47199 Edo+kumwembe

Tue, 19 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Sijui nini kilikuwa kinanizuia kusifu mradi wa mabasi ya Mwendokasi. Nyakati fulani nilikuwa naona mradi uliofanikiwa zaidi nchini. Nilikuwa naandika, nafuta, naandika nafuta, naandika tena, nafuta. Katika kurasa zangu za Facebook na Instagram nilikuwa nakaribia kusifu halafu naacha.

Jinsi wakazi wa Kimara na Mbezi Mwisho walivyokuwa na nyodo nilianza kuwaonea wivu. Nakumbuka jinsi ambavyo wenzao wa maeneo mengine tulivyolazimika kushinda baa za katikati ya jiji kuhofia foleni za kurudi majumbani. Wale wa Kimara na Mbezi wangeweza kurudi makwao, wakabadili nguo na kurudi katikati ya mji kunywa bia zao.

Leo sijui kimetokea nini. Ghafla naona Basi moja linakuja kituoni bada ya nusu saa. Msururu wa watu wanagombea kuingia katika basi wakitumia mwendo wa kasi kupita mlangoni. Wengine wameanza kutumia mwendo wa kasi kurudi majumbani mwao. Wale wanaojikuta Shekilango halafu majumbani kwao ni Kimara mwanzoni wanaamua tu kutembea mwendo wa kasi kurudi makwao.

Sijui chanzo ni nini, lakini najisifu kutosifu mradi huu. Nilikuwa naupa muda kwanza. Wakati mwingine mwafrika usimsifie kwanza. Subiri. Lazima kuna wakati litakuja tatizo ambalo litakutia kichefuchefu, kama hili la sasa.

Ukiuliza tatizo ni nini utajibiwa kwa viingereza vingi sana. Utasikia tu ‘Actually its temporary situation while we are looking for permanent solution’. Nawapenda Wanasiasa wetu. Wakiona tatizo linatia aibu basi huwa wanajibu kwa kiingereza. Wananikumbusha marehemu Syllerside Mziray. Taifa Stars ilikuwa ikifungwa alipenda kujibu maswali ya waandishi kwa kiingereza. Kama vile anafundisha timu ya taifa ya England.

Nasikia kuna Mabasi yapo yamepaki tu sehemu. Kuna ugomvi wa chini chini kwa wanaopaswa kusimamia mradi wenyewe. Tatizo hapa ni kwamba mwananchi wa kawaida hataki kujua nani ana haki katika mgogoro huu. Anataka kupanda basi aende nyumbani. Hasa ukizingatia kwamba barabara zenyewe za mwendo kasi zilijengwa kwa kodi yake na nauli analipa mwenyewe.

Watawala lazima wajue kwamba usafiri ni huduma kwa jamii. Haijalishi kama wanalipia lakini ni huduma. Inabidi waipate kwa wakati mwafaka bila ya kujali mgogoro uliopo ambao unaathiri utendaji wa shughuli zao ambazo hapana shaka ni muhimu kwa ujenzi wa taifa.



Columnist: mwananchi.co.tz