Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Fire extinguisher bao la mkono la trafiki

33147 Edo+Kumwembe Tanzania Web Photo

Mon, 24 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati mwingine ni raha iliyoje kuwa trafiki! Juzi nilikuwa nikitafakari nilipokamatwa na trafiki mmoja wa kike wakati naelekea Morogoro. Tulioishia darasa la saba uswahilini tunasema ‘alinipiga mkono’. Namaanisha aliniambia niweke gari langu pembeni akiwa amesimama katikati ya barabara.

Akaomba leseni yangu kabla ya salamu. Niliwahi kusikia siku moja afande Sirro akitaka tusiwape. Hata hivyo, ni bora umpe tu kwani usipompa na ukajifanya unajua haki zako hapo utazidisha hasira zake kwako. Anaweza kukuzushia kwamba umemkashifu au kumtukana. Nikaepusha shari.

Nikatabasamu kwa sababu nilijua kinachofuata. Nchi za wenzetu polisi anakusimamisha ikiwa anakushuku. Huku kwetu unasimamishwa kwanza halafu unatengenezewa mazingira ya kushukiwa. “triangle iko wapi?” akauliza. Nilikuwa nayo.

Akaangalia bima. Ilikuwa sahihi. Nadhani alisonya kimoyomoyo alipokumbuka kwamba siku hizi hatutakiwi kuwa na ‘Road Licence’. Imewaondolea kigezo kimoja cha kufinyiwa rushwa mkononi. Nadhani inawakera sana.

Tukafika katika suala la kifaaa kinachoitwa ‘fire extinguisher’. Nikatabasamu. Sikuwa nayo. Mama yule akajua sasa amenipata. Ndiyo, sijawahi kuwa na kifaa hicho na nitakwambia sababu, na ndiyo hiyo hiyo niliyomweleza trafiki huyo.

Nilimuomba atafakari kwa makini kama amewahi kuona gari lolote likiungua moto nchini halafu mhanga akatoa fire extinguisher na kuuzima. Si yeye tu, hata wale wanaokuja kumsaidia hawana muda huo. Asilimia 99.9 ya Watanzania hawajui hata inavyotumika.

Kimebaki kuwa kifaa tunachoambiwa ni ‘muhimu’ katika gari. Imeachwa iwe hivyo kwa sababu ni mwanya wa rushwa. Wanaosisitiza tuwe nayo wana sababu nyingine nje ya ‘uongo’ kwamba itatusaidia kuzima moto. Mabasi mangapi yameteketea bila kujitokeza mtu anayetumia fire extinguisher na kujaribu kuuzima. Sio ule mtungi uliopo katika gari wala katika magari yanayopita eneo la tukio. Tunaishi kwa mazoea.

Kwa mfano, yule trafiki ningemwambia ninayo basi asingeniandikia faini bila ya kujali kama naweza au siwezi kuitumia. Hii ndio mianya ya rushwa ambayo hatutaki kuiziba. Hatutaki kuwaza ukweli kwa sababu tukiziondoa na labda tukasema kwa mwaka kila gari liwe linatoa Sh20,000 kwa ajili ya kuimarisha vituo vya uzimaji moto kila wilaya, basi faini zitapungua na rushwa ile itaondoka kama ilivyoondoka ya Road Licence.

Unataka kujua mama trafiki alichukua hatua gani? alinitoza faini. Siku hizi ni moja kati ya sehemu muhimu ya mapato ya nchi kuimarisha uchumi wetu. Moyoni alijua nilikuwa nimesema kweli.



Columnist: mwananchi.co.tz