Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO:Eti mafanikio ya maisha ni kujenga nyumba!

28851 Uchokozi+picTanzaniaWeb

Mon, 26 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nilihudhuria msiba wa rafiki yangu wiki iliyopita. Nilipata majonzi mara mbili. Kwanza kumpoteza rafiki. Majonzi ya pili ni namna ambavyo maisha yetu bado yametawaliwa na fikra potofu. Kuna fikra nyingi potofu sijui tutaziacha lini?.

Watu waliokuwa msibani walikuwa wanamsifia marehemu kwamba alikuwa na mafanikio. Kisa? Ameacha nyumba mbili nyuma yake. Nikajiuliza, mafanikio makubwa ya Mtanzania ni kujenga nyumba? Halafu basi. Ndiyo, halafu basi.

Unaweza kugundua kitu cha maana kwa manufaa ya Watanzania wote, lakini hauwezi kuhesabika kama maisha yako yalikuwa na mafanikio. Watu watasema ‘Jamaa alikuwa hodari, lakini mjinga sana, hajaacha hata nyumba’.

Unaweza kubuni miradi mizuri, ukapata faida kubwa kibiashara, ukapanga katika nyumba nzuri kwa maisha yako yote, watoto wako wakapata elimu nzuri, wakajitegemea, lakini ukifa bila kujenga nyumba inaonekana kama hukuwa na mafanikio.

Ni ujinga. Tuanze kupima. Mafanikio ni nini? Halafu pili tusiendeleze makosa tuliyoyafanya tangu uhuru. Kujenga ni ujinga wa sera za watu wanaotuongoza. Tangu lini mtu binafsi akajenga London? New York? Paris, Johannesburg na kwingineko?

Tulikosea wakati wa Ujamaa. Tukaamua kuwa na shirika moja la nyumba, NHC. Wakajenga nyumba chache kwa kuangalia idadi ya watu wa wakati huo bila ya kujua mbele ya safari mambo yatakuaje. Kampuni binafsi zilipangwa kujenga nyumba kubwa ambazo sisi tungekuwa wapangaji wake. Baada ya hapo tungeweza kuzinunua.

Matokeo yake tunajisifu kujenga huku tukijenga holela. Leo Mbezi Beach imekutana na Bagamoyo kwa idadi ya watu ambao wangeweza kukaa katika ‘Apartment’ tano tu za kwenda juu. Tungejenga Apartment za matajiri, za mabachela, za wanaoanza familia, za maskini, za kila mtu. Tunajenga kwa kusambaza nyumba zetu za chini badala ya kujenga nyumba zinazokwenda juu ambazo zingechukua watu wengi na kutumia maeneo machache.

Leo ushindi wa maisha ya mwanadamu wa kawaida ni kujenga. Si kupeleka watoto shule nzuri, si kuwalisha vema, si kwenda likizo na familia Mauritius, si kuwa mwanahisa wa benki maarufu nchini. Ushindi ni kujenga, tulipaswa kupanga kwa bei nafuu au kununua zilizojengwa kwa mikopo. Kujenga si ushindi sana kama tunavyofikiri.



Columnist: mwananchi.co.tz