Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO : Darasa la saba, maprofesa katika shule moja ya uchumi

56193 Edo+Kumwembe

Wed, 8 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

‘Nimepamiss’ kijiweni kwangu Mwananyamala. Kwa sasa nazurura Ulaya. Jana nikapakumbuka zaidi maskani kwangu. Huwa tunakaa tulioishia darasa la saba tu. Mara nyingi huwa wanapita wasomi wakiongea na simu kwa mbwembwe.

Mara kadhaa wanapita wasomi katika magari yao huku wakiongea na simu wakijadili uchumi ‘actually our economy is very stable’. Huwa wanaongea kwa mbwembwe kwelikweli. Unaweza kudhani wanaendesha uchumi wa dunia.

Kuna siku tulikaa na wenzangu walioishia darasa la saba tukaanza kujadili kufungwa kwa maduka. Huku kwetu tunaita ‘frame’. Tukawa tunapiga soga kwamba kufungwa kwa maduka na watu wa TRA kwa sababu ya kushindwa kulipa kodi kutashusha uchumi zaidi. Kwa nini watu wasiachwe wafanye biashara huku wakilipa kodi kidogo kidogo?

Mwisho wa maongezi tukatazamana usoni tukajiona hatujui uchumi. Labda hawa wanaovaa suti maridadi za Paris, wanaoongea kiingereza cha mbwembwe, huenda wanajua zaidi kuliko sisi. Wao wamesoma sisi tumeishia darasa la saba. Tukaacha hilo lipite.

Juzi nikiwa huku Uswiss nikasoma mahala ‘TRA sasa kutofunga biashara’. Nikacheka. Moyoni nikajiambia “yale yale tuliyojadili na darasa la saba wenzangu Mwananyamala”. Nikakumbuka sana maongezi yetu ya zamani wakati biashara zilipoanza kufungwa.

Sasa ni wazi kwamba tunapata darasa la uchumi bila ya ada. Tunajifunza taratibu jinsi uchumi ulivyo. Haueleweki. Unahitaji fedha izunguke ili uwe imara. Kama maduka yakifungwa ina maana fedha inasita kuzunguka katika mzunguko wake. Kinachohitajika ni akili tu, sio mabavu.

Tulichoamini sisi wa darasa la saba ndicho kinachofanywa sasa na wale wasomi wetu wavaa suti maridadi ambao baadhi yao ni washauri wa Namba Moja.

Kumbe hata kuruhusu wafanyakazi wa Serikali kufanya semina zao mahotelini kunainua biashara ya nchi. Wafanyabiashara wanapata fedha wanalipa kodi. Kumbe kufungwa kwa hoteli sio sifa.

Kadri siku zinavyoyoyoma ndivyo ambavyo Watanzania wote tunajifunza uchumi taratibu. Nilidhani darasa la saba tumeachwa nyuma kumbe na sisi tupo pamoja nao. Hakuna kinachoharibika. Katika msafara wa mamba hata sisi kenge tumo.



Columnist: mwananchi.co.tz