Ilikuwa wiki nzuri. Wiki iliyoishia jana. Ghafla Namba Moja akaibuka na kitu kizito katika mkutano na wafanyabiashara pale kwake Magogoni. Kuna kitu kilikuwa kinausumbua moyo wake. Alitaka kutapika nyongo. Ni kuhusu bandari ya Bagamoyo.
Tulisikia mradi umevunjwa. Labda tuongee tena. Halafu mkuu wa mjengo wa Dodoma akashangaa kwa nini ‘mradi mzuri’ kama ule tumeamua kuachana nao. Niliwahi kuandika hapa. Waliouanzisha sio wendawazimu, na walioachana nao sio wendawazimu. Lazima kuna kitu.
Juzi Namba Moja akatuambia kwamba ulikuwa mkataba kama ule wa mkoloni wa Kijerumani, Carl Peters. Mkataba wa kikoloni, ni kweli. Kilichotajwa ndani yake ni aibu. Mengi yalisikitisha. Kila mtu amesikia. Kuanzia TRA kutogusa kwao hadi baadhi ya bandari kutoendelezwa. Kisa? Bandari ya Bagamoyo.
Sisi tulioishia darasa la saba tumeshangaa sana, lakini hapo hapo imetufikirisha. Kwanza kabisa tukajiuliza. Baada ya hili bomu tunaweza kusikia majibu kutoka upande wa pili? Upande wa wale jamaa wa China, au wale vigogo walioshika usukani utawala uliopita. Je, ndivyo mambo yalivyokuwa? Lakini inawezekana pia kwamba Namba Moja akisema basi tunaamini na kufunga mjadala.
Linakuja jambo jingine. Huu ni mwanzo wa kufungua lile boksi linaloitwa Pandora? Kwamba kuanzia sasa mambo yawe yanawekwa hadharani tu katika mikataba ya nchi yetu, au tuendelee kuwaamini wawakilishi wetu katika mikataba? Huu ni mwanzo mpya wa mikataba ya sasa na ile ya zamani kuwekwa hadharani?
Kuna mikataba ya madini ambayo akina Zitto waliwahi kutuambia haifai. Kuna ile iliyosainiwa haraka haraka. Kuna hii ambayo inasainiwa sasa.
Pia Soma
- Lukuvi: TTCL, Tanesco wadaiwa sugu kodi ya ardhi
- Mwanafunzi afanya mtihani dakika 30 baada ya kujifungua
- Rais Pakistan akamatwa kwa rushwa
- Mwanajeshi Uganda auawa kisa 'kiroba' cha pombe
Tatizo ni kwamba walio chini yake wanapewa dakika za kuongea, yeye hapewi, anajipangia mwenyewe. Anajiwakilisha mwenyewe. Bila shaka katika hili atajifunza kitu.