Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: ‘Braza’ Nape, kiungo mtata asiyetulia uwanjani

67495 Edo+kumwembe

Fri, 19 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

‘Braza’ Nape bwana! Mtu wa kwetu kule Kusini. Nilikuwa namuwaza sana majuzi, mpaka nikafikia kuwaza lipi lilikuwa jambo bora, kumuacha awepo katika ‘kebineti’ au kumuondoa? Nadhani yaliwazwa mengi kabla ya kumpiga chini.

Huenda iliwazwa kwamba kumbakisha angekuwa anavujisha siri. Waliowaza hayo labda walikuwa sahihi. Braza nasikia ana urafiki wa karibu na vigogo ambao wanampingapinga Namba Moja kwa maneno ya chinichini.

Juzi, nikasikia mahala kuna madai ya kuwapo kwa maongezi yaliyorekodiwa kati yake na Kanali. Wengine wanasema maongezi hayo ni feki. Yawe feki (bandia) au sio feki lakini hapo Braza katengenezwa kama muandaa mipango. Kijana anayetumwa kazi za vigogo walio pembeni.

Naam, ina maana awepo uwanjani au nje ya uwanja inajulikana kwamba anasumbua. Akiwepo ndani anapeleka siri nje, akiwa nje anapiga kazi maridadi ya ukarani ambayo inasumbua kweli kweli. Afanywe nini huyu mtu? Inawezekana vigogo wenye hadhi wanawaza sana juu yake.

Ukigeuka upande mwingine unakutana naye katika mitandao. Kule Twitter amejaa mafumbo. Angekuwa ndani asingeandika. Angeishi katika kivuli kinachoitwa ‘Collective responsibility’ (yaani uwajibikaji wa pamoja), lakini kwa kuwa yupo nje, anaandika tu mafumbo yake.

Baada ya kumuwaza sana nikafikiria mambo mawili. Kwanza kabisa Braza sio mfanyabiashara. Maisha yake ni siasa tu. Ina maana anaishi siasa, anakula siasa, analala siasa. Itabidi avumiliwe tu kwa sababu watu wengine wakitoka katika siasa wanakwenda katika biashara zao, yeye hana biashara ya maana.

Pia Soma

Pia, hapo hapo nikawaza, hivi kuna siri nzito imejificha kabla ya 2020 au hakuna? Ina maana Namba Moja akirudi madarakani 2020 Braza ataendelea kuishi hivi hivi tu? Ina maana tutakuwa tunakutana naye Twitter tu au atarudi kuunga mkono juhudi?

Ukiwawaza watu kama Braza unapata hamu ya kuona mwaka 2020 ukifika na kuondoka zake. Siye ambao tupo pembeni tunapata hamu ya kujua hatima ya baadhi ya wanasiasa wetu kama Braza, kabla na baada ya uchaguzi wa 2020.

Kwa sasa mashabiki acha tuendelee tu kumtazama kiungo huyu mtata asiyetulia uwanjani. Mwakani sio mbali. Tuendelee kunywa mtori tu, nyama tutazikuta chini.

Columnist: mwananchi.co.tz