Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO:Atangulie Mzee Ngwilizi, vijana tunaona aibu

Thu, 23 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ghafla majuzi nikasikia msiba wa Bridgedia Hassan Ngwilizi. Nikakumbuka mbali sana. Enzi hizo unasikia jina lake katika nyadhifa mbalimbali. Leo yuko hapa, kesho yuko pale. Keshokutwa yuko katika nyadhifa nyingine.

Tukadhani wazee hawa ni wabinafsi sana. Mbona kila siku nyadhifa wanashika wao tu? Mara kibao tukawakumbusha kwamba “vijana ni taifa la leo”. Hatukutaka kabisa kuambiwa vijana ni Taifa la kesho. Hatukuwaelewa vyema.

Tulikuwa tunawasema sana hawa akina Ngwilizi, John Malecela, Kingunge Ngombale Mwiru na wengineo. Wakati mwingine walipewa hadi ile wizara ambayo ilikuwa inatushangaza wengi. Waziri wake aliitwa ‘waziri asiye na wizara maalumu’. Sijui siku hizi imekwenda wapi?

Basi tukawapiga sana vijembe. Nyakati zikaenda wakastaafu kimyakimya. Lile Taifa la leo likaingia katika nyadhifa mbalimbali nchini. Muda si mrefu sana tukaanza kuwakumbuka tena akina Ngwilizi.

Kumbe kulikuwa na kila sababu ya kuongozwa na wazee kama hawa akina Ngwilizi. Vijana wanasumbua sana bwana! Wababe, watemi. Katika hizi VX na V8 siku hizi wanapiga mikwara kuliko akina Ngwilizi ambao walikuwa wanajeshi wa vyeo vya juu.

Vijana ndio wanaongoza kwa ule usemi wa ‘hivi unanijua mimi wewe?’ Wengine wanyonge huku maskani ndio inatufanya tuwakumbuke akina Ngwilizi ambao tulikuwa tunawasikia katika taarifa za habari na kuwasoma magazetini.

Pia Soma

Inawezekana labda akina Ngwilizi walikuwa wakali sana, hata hivyo uzuri wake ni kwamba mlikuwa hamkutani sana katika maeneo ya ujana na vurugu. Ungekutana vipi disko na mzee Ngwilizi? Ndio maana tabia zao binafsi zilibaki sirini. Walikuwa wakikutana wazee kwa wazee katika ‘club’ zao za viongozi huko uzunguni na maisha yao yakabakia sirini. Kwa sasa hali ni tofauti.

Atangulie kwa amani Mzee Ngwilizi. Ameondoka huku vijana tunaona aibu. Nadhani alipata wasaa wa kuwaona vijana wa Namba Moja aliyepita na vijana wa Namba Moja wa leo. kule katika wilaya zetu ni ‘miunguwatu’. Kuna yule mmoja kule kwetu Kusini alimchomolea bastola muuza madafu. Vipi kama angefikia cheo cha brigedia ingekuaje?

Columnist: mwananchi.co.tz