Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Askofu Gwajima atabakia kuwa juu kileleni

61467 Edo+Kumwembe

Thu, 6 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hivi ndivyo jinsi maisha yanavyokwenda kasi. Wiki mbili zilizopita Askofu wetu, Josephat Gwajima alikuwa akijaribu kufafanua tuhuma za mtu ‘aliyefanana’ naye katika mkanda mmoja wa kijinga wa ngono uliosambaa mitandaoni.

Ungeweza kudhani kwamba ulikuwa mwisho wake. Mkanda umesambaa leo, kesho tu akaitisha waandishi wa habari. Kando mwa mkewe akamwaga sera zake vyema. Mkewe naye akanyanyuka akasimama upande wa mume wake kipenzi.

Mpaka leo sijauelewa ule utetezi lakini wakati mwingine tunaambiwa kukubali yaishe. Kwa upande wangu nimekubali yameisha kwani hata nikikataa itanisaidia nini? James Hardley Chase aliwahi kuandika kitabu kilichoitwa ‘Things Men do’. Nadhani nimeeleweka.

Ghafla juzi askofu akaibuka kando mwa Namba Moja pale Magogoni. Suti yake ilikuwa maridadi. Nadhani atakuwa amenunua katika duka la Zara Marekani, Harrod’s pale London au maduka ya Gucci kule Milan Italia.

Askofu akamwaga sera zake kuhusu mradi wa Stigler’s Gorge. Nilimuelewa vyema hasa alipotoa mfano kuhusu mayai na chipsi. Kwa nini wazungu watuhangaishe akili zetu? Wao wakianzisha miradi yao huwa hawajali mazingira, sisi tukianzisha yetu huwa wanapiga kelele za mazingira.

Kuna vitu huwa tunajifanya hatumuelewi Namba Moja, lakini anakuwa sahihi. Hili yuko sahihi na alitumia akili kumpata Askofu Gwajima atuelezee.

Pia Soma

Nilimuelewa sana Askofu hadi alipoanza kutoa mifano ya mkataba wa Kyoto. Alimwaga sana sera zake nje ya mlango wa Ikulu. Ghafla nikawaza jinsi alivyo mmoja kati ya Watanzania wenye bahati. Kuanzia ile kashfa ya kutajwa katika orodha ya watu ambao inawezekana wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Akaponyoka.

Ikaja hii ya mkanda wa video. Ameponyoka. Sasa anasimama kando mwa Namba Moja kutuelezea umuhimu wa mradi wetu huu mkubwa. Kuna mawili hapa. Inawezekana kweli Askofu ana Mungu kando yake ama inawezekana ana bahati ya mtende au inawezekana ana kipaji cha ajabu cha ushawishi.

Vyovyote ilivyo, kama ambavyo yule mlevi Pierre anavyosema. Gwajima atabakia kuwa juu juu zaidi. Juu kileleni! Ningependa kuambukizwa bahati yake. Usidhani natania. Nani asingependa kuwa yeye? Atabakia kuwa juu kileleni.

Columnist: mwananchi.co.tz