Namba Moja alikuwa mjengoni kwake pale karibu na Feri Ijumaa mchana. Nakukumbusha tu, Rais wangu huwa namuita Namba Moja. Ndiye raia namba moja nchini. Ndiye mwenye uamuzi namba moja nchini. Analoamua ndio mwisho.
Ijumaa alikuwa ameamua kuvunja kitu kinachoitwa kikokotoo cha mafao. Hatujui hiki kikokotoo kilitoka wapi lakini ndani yake kilijaa dhulma dhidi ya watu walio katika hatua ya uzeeni, au kwa sisi wengine ambao tunaelekea kama tutafika.
Swali la wapi kikokotoo kilitoka tulifiche kwa sasa. Swali la wapi jeuri ya baadhi ya mawaziri kutetea kikokotoo ilikotoka tulifiche kwa sasa. Kitu muhimu ni kwamba Namba Moja ameamua wanaotunza pensheni zetu waachane na habari za vikokotoo.
Ni kitu muhimu. Ilikuwa ni dhulma. Namba Moja ameahirisha habari hii mpaka mwaka 2023 kwa ajili ya kupata mwelekeo mpya. Lakini hata mwaka huo ukifika kuna kitu kimoja cha msingi zaidi ambacho tunahitaji kujadili. Tunahitaji majadiliano kati yetu na wale wanaotunza fedha zetu.
Haiwezekani mwanadamu mmoja akakutana na wenzake halafu kiurahisi tu wakapanga matumizi ya fedha binafsi za mtu mwingine. Hata kama kuna nia njema lakini yanahitajika majadiliano. Pasipo na majadiliano ni dhuluma. Ni ukosefu wa haki.
Mwaka 2023 ukifika tukumbuke kuwa Mwenyezi Mungu alituumba tofauti. Linapokuja suala la matumizi ya fedha alituumba tofauti pia. Nadhani ni vema kila mtu akafa na chake. Kuna wale ambao hata ukiwapa fedha nyingi za kustaafu watatumia ovyo. Kuna wale ambao hata ukiwapa fedha chache za kustaafu watatumia vema.
Kuna wale ambao unaweza kuwapa fedha kiasi halafu katika kikokotoo wakapata fedha taratibu na bado wakaishia kuwa walevi na wazinzi. Kuna wale ambao kabla hata hawajaanza kulipwa taratibu watakuwa wameshaanza kutengeneza faida kutoka katika fedha chache za mkupuo.
Serikali haingii lawamani pale inapompa mzee fedha akaamua kuzitwanga kadri anavyoweza. Ili mradi ilimpa tu na haikumdhulumu. Mtaani wote tunageuka kuwa mashuhuda. Haya ndio mambo ya kuzingatia pindi mwaka 2023 utakapofika.
Kwa sasa hakuna tunachoweza kufanya zaidi ya kumpigia saluti Namba Moja. Ametimiza wajibu wake. Haki imetendeka hata kama ni kwa muda.