Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: ‘Anko’ bado yupo katika ubora wake

66943 Edo+Kumwembe

Tue, 16 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Namba Moja bado yupo katika ubora wake. Midomo wazi kwa makada. Juzi alimchagua rafiki yangu bwana Julius Mtatiro kuwa Mkuu wa Wilaya kule kwetu Tunduru. Huyu bwana alikuwa mpinzani kisha akaunga mkono juhudi.

Aliunga mkono juhudi katika namna ya kushangaza kidogo. Awali rafiki yangu huyu alikuwa mkali kwelikweli. Kuanzia utawala wa JK mpaka huu wa Namba Moja wa sasa. Ghafla tukaona kimya. Baadae tukaona ameunga mkono juhudi. Tulishangaa kidogo.

Inahitaji moyo kutoka kuwa mtu mkali mitandaoni, kisha ghafla ukaunga mkono juhudi, lakini hata hivyo tukumbuke kuwa mwanadamu anaishi mara moja tu. Kuna wakati anafanya uamuzi mgumu kwa ajili ya kujiokoa na mambo mengi.

Sasa amekuwa bosi wa wilaya yetu kule Tunduru. Kinachofuraisha hapa wanaonuna sio wapinzani. Wanaonuna ni wenzake katika chama alichokwenda. Kuna watu wamepambana kwelikweli kukipa uhai chama lakini Namba Moja hana muda wa kuwateua. Anajenga chama upya.

Hawa makada kama walivyo raia wengine nchini waliamini kwamba tukifika mwaka 2019 Anko atajaribu kurudi nyuma na kuwakumbuka watu wa zamani chamani. Hapana, kumbe walikosea. Katika chama inaonekana Namba Moja hajarudi nyuma. Msimamo wake ni ule ule kwamba kuna watu walivuruga chama kwa kivuli cha ukada na wataishia kunawa tu. Hawaruhusiwi kula tena.

Huku katika masuala ya uchumi na mengineyo, hasa biashara, Namba Moja kidogo anaonekana kukubali kubadilika. Katika chama inaonekana hali tete. Ilidhaniwa kwamba kuna watu wa zamani wangeanza kufikiriwa upya ili kurudisha umoja katika chama, lakini Namba Moja hana muda huo.

Pia Soma

Mpinzani mwingine kapewa wilaya, na huyu alikuwa mpinzani kweli kweli. Ndugu zangu makada wa zamani wanaendelea kuumia lakini wavumilie tu. Kitu cha msingi ni kwamba Namba Moja anatufundisha kutokariri maisha.

Hata sasa wanapaswa kujifunza kumzoea Namba Moja kuliko kushangaa. Itawasaidia kisaikolojia. Itawasadia pia katika zoezi la kutotukana ovyo wapinzani. Huwezi kujua ni lini mpinzani anaweza kuwa bosi wako bila hata ya chama chake kuingia madarakani.

Columnist: mwananchi.co.tz