Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHAMBUZI: Vyama vya siasa visidhibitiwe ila viwekewe utaratibu kisiasa

28110 Pic+vyama TanzaniaWeb

Wed, 21 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Uwepo wa vyama vingi vya siasa, nadharia yake haikuja kwa fikra za kubabaisha. Viliruhusiwa kikatiba baada ya tafakuri ya kina. Ushindani wa vyama vya siasa ni alama muhimu kwa nchi ya kidemokrasia.

Chama kinaposhika dola au vyama washirika vinapochukua uongozi wa nchi, vinakuwa na wajibu wa kuheshimu vingine ambavyo havina mamlaka.

Tofauti inayokuwapo ni yale mamlaka ambayo hutolewa wananchi. Na uwepo wa vyama vingi ni kumtendea haki mwananchi ili akiona kuwa alichokikasimisha dola hakitimizi matarajio yake, anakipa kingine ambacho anaona kinavutia.

Sasa basi, uwepo wa vyama vya siasa sio matakwa au masilahi ya wanasiasa, bali wananchi. Hatua yoyote ya kuvikandamiza, kuvinyamazisha, kuvifanya visiwepo au kuvidhibiti visifanye kazi kwa uhuru, ni hujuma dhidi ya mwananchi.

Kwamba ule ushindani wa kisiasa, husababisha muda mwingi nchi kukumbwa na harakati za kisiasa, badala ya kujenga nchi kuleta maendeleo. Dhana hiyo ni batili.

Ni adui wa maendeleo?

Mwaka jana nchini Afrika Kusini, Rais wa Nne, Jakaya Kikwete alisema kuwa makosa yenye kufanywa na watawala ni kuvichukulia vyama vya upinzani kuwa maadui badala ya washindani. Kikwete alisema vyama vya upinzani ni washirika wa utawala bora na maendeleo.

Kusherehesha hoja hiyo ya Kikwete ni kuwa watawala wanatakiwa kupigania uwepo wa vyama vya upinzani, kwani ndivyo vinavyofanya walio madarakani wasilale.

Mwaka 2014, nilichekeshwa na makala kuhusu India, iliyoandikwa na mwandishi wa nchi hiyo, Rakesh Dubbudu. Aliandika kuwa vyama vya siasa nchini humo vinakua kwa kasi kuliko ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo.

Kichekesho ni kuwa India ni moja ya mataifa duniani ambayo uchumi wake unakua kwa kasi. Umaskini kama taifa na kwa wananchi wake umeshaoneshwa njia ya kutokea. Hata hivyo, eti vyama vya siasa vinazidi kasi ya uchumi kwa namna vinavyokua.

Hoja yake ilikuwa namna ambavyo India inakuwa na idadi kubwa ya vyama vya siasa. Uchaguzi wa mwaka 2014, vyama vya siasa vilikuwa zaidi ya 1,700, wakati vilivyoshiriki uchaguzi vilikuwa 43 tu. Hapo hapo zingatia kwamba uchumi wa India unapaa kwa kasi kubwa.

Tanzania ilipofikia

Mifano iliyotangulia, iunganishwe na mazingira ya Karne ya tano Kabla ya Kristo, katika uliokuwa utawala wa Roma ya kale, seneti yake iliwakilishwa na makundi mawili ambayo yaliitwa Patricians na Plebeians. Patricians ni kundi la viongozi na watu wenye hadhi kubwa kwenye jamii, wakati plebeians walikuwa wafanyabiashara wakubwa.

Vyama vya siasa vilianza mwaka 1678 kutokana na nadharia inayoitwa Popish Plot. Kwa ufafanuzi ni kuwa Popish Plot ni uzushi uliotungwa na Mwingereza Titus Oates, ukieleza kuwa Kanisa Katoliki lilipanga kumuua aliyekuwa Mfalme wa England, Charles II, ili mdogo wa Mfalme Charles II, James au Duke wa York arithi Ufalme.

Mgogoro huo ndio ukazaa vyama vya Tories na Whigs, ambavyo vilikuwa vikiingia kwenye uchaguzi ili wananchi waamue upande gani wapo nao.

Inatakiwa wakati wowote vyama vya siasa viachwe huru na vionekane vipo sawa. Tanzania kumekuwa na hali ambayo vyama vya upinzani vinajiona havipo huru. Kipindi ambacho wapinzani wanalaumu kuwa wanabanwa na mazingira, kwamba hawapo huru kufanya shughuli zao, yanakuja mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa ambayo wanalalamikiwa kuwa inazidi kuwaning’iniza.

Hivi karibuni Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta alimshauri Rais John Magufuli kuwa nchi lazima ifuate utawala wa sheria, lakini hizo sheria ziwe zinaangaliwa kama haziingilii uhuru wa watu wengine. Kuna maeneo sheria ya vyama inaonekana kuingilia mamlaka ya vyama ndani ya taasisi zenyewe. Je, ushauri wa Samatta haukuzingatiwa? Msajili wa vyama vya siasa ni mteuliwa wa Rais. Kwa sasa Rais ni Dk Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa CCM.

Halafu msajili anapewa mamlaka makubwa kwenye vyama vyote. Huo usawa upo wapi? Inapendeza vyama viachwe huru na visidhibitiwe ila vipewe mipaka. Katika majukwaa ya kisiasa, vyama vyote viwe sawa.



Columnist: mwananchi.co.tz