Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHAMBUZI: TRA iamke, ijifunze, ibadilike

Mon, 7 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tangu enzi za uhuru tulikuwa tukifundishwa kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa Tanzania. Kwa kadri tukuavyo na tuendavyo kwenye zama mpya za dunia tunazidi kujidhihirishia kuwa kodi ndiyo uti wa mgongo wa taifa na kwamba taifa lisilokusanya kodi ipasavyo na kwa uhakika ni taifa mfu.

Tangu Rais John Magufuli aingie madarakani, mapato yanayotokana na kodi yamepanda kutoka Sh800 bilioni hadi Sh1.2 trilioni. Bila shaka tunayo kila sababu ya kuwapongeza sana wakusanya kodi kwa maana ya mamlaka ya ukusanyaji kodi TRA na serikali kwa ujumla.

Hata hivyo, ni wazi kuwa upandaji wa mapato bado hauakisi vyanzo vingi vya mapato ambavyo vimetapakaa kila mahali na havijafanyiwa kazi kama inavyopaswa kuwa. Mathalani, katika muongo huu wa sasa, ukitembelea nchi kama Denmark, Marekani, Norway na kwingineko, utaona namna ambavyo serikali zimejizatiti katika ukusanyaji kodi na karibia kila kinachofanyika mahali popote kinalipiwa kodi.

Ni kweli kwamba nchi yetu ni masikini sana, kwa maana ya umasikini unaotafsiriwa na vyombo vya kifedha vya kimataifa, lakini hiyo haiondoi ukweli kuwa tuna kila sababu ya kujifunza kwa wenzetu kwa namna wanavyosimamia masuala ya kikodi kwa mafanikio makubwa. TRA ya kwetu hapa ina kazi ya ziada, inajiendesha kimazoea sana hasa kwa ngazi za chini na inakosa mbinu za kutosha za kukusanya kodi.

TRA na wafanyabiashara

Hata hivyo, hakuna mawasiliano mazuri na hata mahusiano yenye tija kati ya wafanyabiashara na TRA. Ukifanya utafiti mitaani utajiridhisha kuwa wafanyabiashara wengi wanawaona TRA kama maadui. Natambua kuwa hata Marekani mamlaka za kukusanya kodi zinaonekana chungu kwa raia, lakini hapa kwetu TRA inaonekana kama joka linalotaka kumeza biashara za watu.

Wakati fulani Rais JPM aliwaelekeza TRA wabadilike, akawataka waongeze juhudi katika kukusanya mapato kwa njia za kisasa zaidi. Hivi majuzi nimemsikia Waziri wa Fedha, Dk Phillip Mpango akiwataka TRA wafanye kila wawezalo kuwasaidia wafanyabiashara wasio wadaiwa sugu wasifikie hatua ya kufunga biashara zao na kukimbia.

Kauli hizo za Rais na Waziri Mpango zina maana kuwa TRA iendelee kujitafakari na ichukue hatua. Moja ya hatua hizo ni kuimarisha mawasiliano na mahusiano yake na wafanyabiashara. Tunajua kuwa TRA ina kumbukumbu za namba za simu, barua pepe na mawasiliano mengine ya wateja wake, hayo yawe mwanzo wa kurejesha mahusiano na mawasiliano.

Kitengo cha mawasiliano kwa mlipa kodi kifanye kazi usiku na mchana kuwasiliana na wafanyabiashara mbalimbali na kujua changamoto zao, kutatua zile zinazowezekana na kufanyia kazi maombi mbalimbali kutoka kwao. Kitengo hicho kiwezeshwe kuwakumbusha wafanyabiashara lini wanapaswa kulipa kodi zao na lini zitakamilika. Kitengo hicho kiwe roho ya TRA.

Wafanyabiashara wengi hupenda kufuatwa na kufikiwa bila kutishwa, hupenda kupewa muda kukamilisha makosa yao ya kikodi ndani ya muda fulani, wafanyabiashara wote hupenda kusaidiwa na kushauriwa na mamlaka inayokusanya kodi kutoka kwao, hakuna mfanyabiashara ambaye anapenda agombane na mamlaka ya kukusanya kodi. TRA ijielekeze kwenye mbinu hizi na iajiri wataalamu wengi wenye uwezo wa kufundisha maafisa wa mamlaka hiyo namna ya kuwafikia watu na kuwashawishi walipe kodi.

Kodi za kubambikiza

Ugonjwa mwingine ambao unaizonga TRA ni baadhi ya maofisa wake kubambikiza kodi kwa wafanyabiashara. Hili ni tatizo kubwa. Kumekuwa na makadirio yanayoshangaza ya kodi, na haya huwakumba wafanyabiashara wanaofanya biashara zenye mtaji unaolingana.

Nilitembelea duka la rafiki yangu Kariakoo, anauza nguo za ndani za kina mama na kina baba kwa rejareja, na jirani yake kuna duka kubwa zaidi la rejareja la nguo hizo hizo. Alinishangaza sana pale aliponieleza kuwa kodi aliyotozwa yeye ni kubwa mno kuliko ya yule mwenye duka kubwa zaidi. Nilipofuatilia taarifa zile nikajiridhisha kuwa ni za kweli.

Kuwabambikia wafanyabiashara kodi kubwa wasizostahili ni kuwafukuza, ni kuwafanya wafunge maduka yao na kukimbilia maeneo mengine ambako wanaweza kukirimiwa na kutendewa haki.

Suala hili la kodi za kubambikiza lilizungumzwa pia na JPM akiwa jijini Arusha, lakini hadi tuzungumzavyo bado maofisa wa TRA wanapanga kodi kwa uwiano unaotia shaka baina ya mfanyabiashara mmoja na mwingine.

Hoja ambayo huzuka mara nyingi ni kuleta ushahidi wa masuala haya. Ushahidi wa kwanza ni rufaa nyingi ambazo wafanyabiashara wanakata wakipinga au kuomba wapunguziwe kodi kwa sababu za kibiashara. Wafanyabiashara hawa si vichaa, haiwezekani mtu anunue bidhaa kwa bei ya jumla ya Sh1 milioni na anapanga kupata faida ya Sh200,000 halafu TRA inaenda kudai kodi ya Sh150,000, yaani ina maana huyu mfanyabiashara anaifanyia TRA biashara, hilo haliwezekani hata kidogo.

Ni lazima TRA ijifunze zaidi na iendelee kubadilika kwa kasi maana inazo kazi za ziada nyingi kushinda ambavyo watendaji wa TRA yenyewe wanadhani. Mathalani hadi sasa nimeeleza, uwezo wa nchi yetu kubuni vyanzo vipya vya mapato unasuasua sana, na kazi hii ya kubuni vyanzo vipya vya mapato inawahusu sana wao.

Pamoja na changamoto nyingi za kiutendaji ambazo zinaweza kuwa zinaiathiri mamlaka hii, bado inao wajibu wa kukusanya kodi kitaalamu, kisasa, kiteknolojia na kwa kuwahamasisha zaidi wafanyabiashara kuliko kuwatisha.

Julius Mtatiro ni mchambuzi wa mfuatiliaji wa utendaji wa Serikali barani Afrika; ni mtaalamu mshauri wa miradi, utawala na sera na ni mtafiti, mfasiri na mwanasheria. Simu; +255787536759. Barua Pepe; [email protected])



Columnist: mwananchi.co.tz