Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHAMBUZI: Siasa zetu na usahihi kuhusu uzawa, uzalendo

28107 Pic+siasa TanzaniaWeb

Wed, 21 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tunapojadili suala la uzawa, kuna swali la msingi la kujiuliza: Uzawa ni dhambi, ubaguzi au ni kuchanganyikiwa? Je, uzawa na uzalendo ni mapacha? Hili nalo ni swali la msingi. Ni uzawa au ni uzalendo? Kipi kitangulie?

Nimekuwa siwaelewi vizuri wanaoileta hoja ya uzawa kujadiliwa na wale wanaoipinga. Lakini, kwenye mizani, wale wanaoitetea wanaeleweka kidogo kuliko wale wanaoipinga. Kuna haja gani kuwatangazia wazawa kuhusu uzawa wao? Au wazawa kujadili uzawa wao? Hata hivyo, yule anayeutangaza uzawa kwa mzawa ana unafuu wa kueleweka zaidi ya yule anayeukataa uzawa yule anayetaka kuutangazia ulimwengu kwamba hakuna kitu kama uzawa.

Kitu kingine ambacho nimekuwa nikikiona kuwa si cha kawaida katika mjadala huu wa uzawa ni pale hoja ya uzawa inapofananishwa na ukaburu au ubaguzi wa rangi. Huku ni kuchanganya vitu au kuchanganyikiwa. Wazawa wa nchi yoyote ile wanaweza kuwa ni rangi tofauti. Yeyote anayeongelea uzawa akawa na mawazo ya ubaguzi wa rangi anakwenda tenge. Tamko la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu linaeleza jambo hili vizuri sana. Mtu yeyote anayeonyesha aina ya ubaguzi na kuweka binadamu katika makundi ya ubora anapigiwa kelele na dunia nzima.

Nimelazimika kuingia kwenye mjadala huu wa uzawa baada ya kuona dhana nzima ya uzawa inapotoshwa. Na hii ni hatari kubwa katika Taifa letu la Tanzania. Watu wanatanguliza siasa, vyama, vyeo na kusahau kabisa mustakabali wa Taifa letu.

Mwalimu Nyerere, aliwapokea watu wote. Aliangalia mchango wa mtu katika Taifa. Aliangalia mahitaji ya watu. Alielewa vizuri uzawa wa Afrika Mashariki na uzawa wa Afrika nzima. Alikuwa anaona mbali. Alikuwa anaishi karne mbili mbele yetu. Hatukuwai kupata matatizo ya uraia wakati wa Mwalimu.

Kila nchi ina wazawa. Si kazi ngumu kumtambua mzawa. Amir Jamal (marehemu), alikuwa mzawa wa Tanzania. Alilitumikia Taifa letu kwa moyo wote. Lakini leo hii kaburi lake huwezi kuliona hapa Tanzania, liko Canada.

Tunao wazawa wengi wenye asili tofauti. Uchumi wa hapa ukienda vibaya wanahamia Uganda, Kenya na wakati mwingine wanahamia Uingereza. Ni wazawa lakini mara nyingi unawakuta wana utaifa mara mbili au nusu ya familia inaishi hapa, nyingine Kenya na nyingine Uingereza. Wanategeshea upepo.

Naweza kusema kwamba kuna mambo ukianza kuyajadili unaonekana kama kichaa anayekataa kuvaa nguo na kuanza kutembea uchi. Hivyo, suala zima la uzawa ni la utekelezaji. Hili haliko mbali. Mwenye masikio asikie, mwenye macho atazame kwa makini. Uzawa ni kitu ambacho hakiepuki kwa kila Mtanzania.

Padri Privatus Karugendo

+255754633122

[email protected]



Columnist: mwananchi.co.tz