Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHAMBUZI: Ndugai angetumia kanuni tatu kumjibu CAG Asaad

Thu, 17 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati fulani, Rais wa nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete aliwahi kuwauliza wana CCM kwenye mkutano wa chama: “Mnataka wakisema hatujafanya kitu tuwatume polisi wawakamate?”

Hili ni swali lililotokana na lawama kutoka kwa makada wa CCM, waliokuwa wanachukizwa na maneno ya wapinzani kuwa chama hicho hakijafanya lolote licha ya kuongoza Serikali tangu nchi ilipopata uhuru.

Kikwete aliwaambia wana CCM: “Wakisema hatujafanya kitu, ni jukumu lenu kuwajibu kuwa tumejenga barabara, tumejenga madaraja. Nataka niwaambieni, tukitegemea polisi tutakwisha.”

Hekima ya JK ni kwamba mtu akisema hujafanya kitu, mjibu kwa kueleza yale ambayo umefanya. Siyo kutumia mabavu. Mpinzani akisema hujajenga barabara, halafu ukamweka kizuizini, hapo ndiyo unakuwa umemjibu? Onyesha barabara uliyojenga.

Hivi karibuni umeibuka mvutano usio na afya kwa nchi. Chanzo cha mvutano ni kauli aliyoitoa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, kwamba Bunge limekuwa likionyesha udhaifu kwa kutoibana Serikali kuhusu ubadhirifu unaoonyeshwa na ripoti za ofisi yake.

CAG alizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kuwa wajibu wa ofisi yake ni kufanya ukaguzi na kuandika ripoti. Baada ya hapo ni kazi ya Bunge kuibana Serikali mahali palipo na ubadhirifu

Kwa kutumia kanuni ya Kikwete, jibu ambalo lilipaswa kutoka bungeni kwenda kwa CAG, ni hili; kwamba Bunge si dhaifu, kwani limeshafanya kadha wa kadha, kwa kuorodhesha jinsi ambavyo Bunge limeshatekeleza kazi ya kuibana Serikali.

Mathalan, CAG alisema ripoti zake huonyesha kuna ubadhirifu lakini Bunge huwa halichukui hatua. Majibu ya Bunge yalitakiwa kuwa ama hakuna ubadhirifu ulioonyeshwa au kueleza hatua za kibunge zilizochukuliwa kuibana Serikali.

Mfano; Bunge la 10, Spika Anna Makinda, angeambiwa Bunge lake ni dhaifu, angejibu jinsi lilivyoiwajibisha Serikali kupitia kashfa ya uchotaji fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, Tokomeza Ujangili, kung’oka kwa mawaziri sita mwaka 2012 kupitia madudu yaliyooneshwa na ripoti ya CAG na kadhalika.

Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta, ungemwambia Bunge lake ni dhaifu, angecheka, kisha angejibu jinsi lilivyoiwajibisha Serikali katika kashfa ya Richmond mwaka 2008.

Kanuni ya William Ward

Kwa kumnukuu mwandishi wa Marekani, William Ward wa Karne ya 20, alipata kusema: “Ni busara kuelekeza hasira zako kwenye matatizo- siyo watu; shabaha ya nguvu zako iwe kwenye majibu- badala ya visingizio.

Hii ni kanuni ya pili ambayo Ndugai angeitumia, angemjibu vizuri CAG Assad. Tatizo lililozungumzwa ni Bunge kutowajibika. Ndugai alipaswa kujielekeza hapo, siyo kuelekeza hasira kwa msema tatizo.

Pili; matumizi ya nguvu shabaha yake iwe kwenye majibu, siyo visingizio. Ndugai alitoa wito kuwa CAG Assad afike kwenye Kamati ya Maadili la angepelekwa kwa pingu.

Ndugai amechagua kuwa mkali, ndiyo maana ‘amechimba mkwara’ .

Kanuni ya William Burroughs

Mwandishi mwingine wa Marekani pia wa Karne ya 20, William Burroughs, alipata kusema: “Ubongo wako utajibu maswali vizuri kama utajifunza kutulia na kusubiri jawabu.

Kanuni hii ya tatu, kama Ndugai angeitumia, angegundua yafuatayo; Mosi, Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, kifungu cha 14 (I), inataka wito wa Bunge uwe wa maandishi na anayeitwa aupokee, si kupitia vyombo vya habari. Hata kama barua ilifuata, hakukuwa na sababu ya wito wa hadhara.

Pili, sheria hiyo inatamka Bunge au Kamati ndiyo huamua kumwita mtu atoe ushahidi, si Spika kujiamulia.

Tatu, Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, kifungu cha 18, inauawa na Ibara ya 143 (6) ya Katiba, inayozuia CAG kufuata amri za yeyote, isipokuwa Mahakama.

Columnist: mwananchi.co.tz