Ndoto za vijana wengi wanaoingia kwenye siasa ni ajira. Kijana msomi baada ya kumaliza chuo, ama kwa kuona ajira ngumu au kwa mapokeo kuwa siasa ni kazi inayolipa zaidi, wanaamua kujiunga na vyama ili wapate fursa za uongozi.
Kutokana na ugumu wa nafasi za kuchaguliwa, vijana wanaongia kwenye vyama huamua kuwa wapambe wa wanasiasa waandamizi au hata wazee ili waonekane, angalau wapate japo uteuzi, kisha mbele ya safari wazifikie nafasi za kuchaguliwa.
Kutokana na wito huo wa vijana kuingia kwenye siasa ili kusaka ajira, imekuwa sababu ya kuwa na kasoro zifuatazo.
Mosi, vijana waliopo mstari wa mbele kwenye uongozi hawana vipaji. Pili, wenye vipaji hawajitokezi. Tatu, vijana badala ya kuwa viongozi katika kizazi chao, wanageuka wapambe wa viongozi wazee. Nne, maandalizi ya uongozi kwa vijana hakuna.
Wimbi la kauli za kukurupuka kutoka kwa viongozi vijana ni alama kwamba hawakuandaliwa kuwa viongozi. Makundi mengi ya vijana mitandaoni wakitukana watu ili kuwatetea au kuwasifia viongozi walio nyuma yao, ni kielelezo cha kutumika kwao ili siku zijazo wakumbukwe.
Vijana wenye vipaji vya uongozi ambao wanajiheshimu na hawataki kujipendekeza. Hawataki kuingia kwenye mkumbo wa matusi mitandaoni na kusifia tu au kukosoa tu kama akili imehama, hawawezi kuonekana. Mwisho, Taifa linapata viongozi vijana wasio na sifa.
Wenye sifa wanaishia kuwa viongozi wazuri kwenye familia zao au katika taasisi zao za kazi.
Wakati uongozi safi wa vijana unasalitiwa na vijana wasaka ajira wanaokimbilia siasa, upande wa pili, wastaafu wanabana nafasi kwa kuona kuwa uongozi wa kisiasa ni kimbilio la pensheni.
Hivi leo kuna wabunge na mawaziri waliokuwa watumishi wa umma na wakastaafu. Wengine walipoona muda unakwenda na wanakaribia kustaafu ndipo wakakimbilia kwenye siasa.
Hatua ya tatu
Vijana wa zamani ambao nyakati zao walijisifu kuwa ni viongozi vijana, huamini kwamba uongozi wa siasa ni ajira ya kudumu.
Mtu anakuwa mbunge vipindi vitano na bado anataka kuendelea. Alipokuwa kijana alifanya kampeni kuwa ni zamu ya vijana. Muda unafika naye awaachie kizazi kipya lakini anagangamala abaki.
Wastani wa wanasiasa wanaoamua kuinua mikono juu na kuacha ubunge ni miaka 60 mpaka 70, tena baada ya kushindwa kwenye kura za maoni ndani ya vyama vyao.
Wapo ambao walikuwa wabunge mpaka wakajishtukia, maana walikaa kwenye uongozi wa siasa kwa zaidi ya miaka 40. Mfano ni Paul Kimiti, Chrisant Mzindakaya na wengine. Tena baada ya kuachia ubunge wakateuliwa kuwa wenyeviti wa bodi za mashirika ya umma.
Wapo waliong’olewa kwa nguvu. Mfano ni Stephen Wasira ambaye alishindwa ubunge jimbo la Bunda Mjini, alipogombea na Ester Bulaya wa Chadema mwaka 2015.
Wasira ni mbunge tangu mwaka 1970. Miaka 45 baadaye aliposhindwa ubunge wafuasi wake walikwenda mahakamani ambako nako walishindwa.
Hatma ya taifa lolote hutakiwa lijengwe na maono yenye kuakisi matarajio ya vijana. Maana vijana ndiyo tabaka la kati lenye kuunganisha watoto na wazee.
Vijana wanauishi ujana ambao wazee wameshaupitia. Vijana wanauishi ujana ambao watoto wataufikia. Zaidi vijana ndiyo tabaka kubwa lenye watu wengi katika vipindi vyote vya kimaisha.
Mwisho kabisa, vijana ndiyo tabaka lenye watu wenye nguvu, walio na akili inayofanya kazi zaidi kwa haraka. Vijana ndiyo taifa.
Haimaanishi kuwa wazee hawafai, la! Wazee ni muhimu kwa ujenzi wa viongozi vijana, maana wao walishauvuka ujana. Hata hivyo, wazee hawafahamu mahitaji ya vijana.
Mzee mwenye umri wa miaka 70, alikuwa kijana miaka 40 iliyopita. Kwa hiyo alikuwa kijana miaka ya 1970. Fikra za vijana wa miaka ya 1970 ni tofauti na sasa palipo na ukuaji mkubwa wa teknolojia.