Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHAMBUZI: Kipigo cha Simba ni taswira ya soka Tanzania?

40083 Angetile+osiah UCHAMBUZI: Kipigo cha Simba ni taswira ya soka Tanzania?

Tue, 5 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nchi bado imeduwaa. Hadi sasa hakuna aliyezinduka kutoka katika butwaa la kipigo cha mabao 5-0 ambacho wawakilishi wetu kwenye Ligi ya Mabingwa wa Afrika, Simba walipewa na wababe wa soka barani Afrika, Al Ahly ya Misri.

Si kwamba Wamisri hao hawawezi kushinda kwa kiwango hicho cha mabao-- kwa kuwa wameshawahi kufanya hivyo--, bali kwa sababu inaonekana kama Simba haijifunzi kutokana na mechi zilizopita.

Na kibaya zaidi ni kwamba sasa huwezi kuweka dau kwamba Simba itashinda mchezo unaofuata au la kwa kuwa hakuna vidokezo vyovyote vinavyoweza kukuambia kuwa kuna mwelekeo wa kuimarika. Kwa kifupi huwezi kubeti matokeo ya Simba kwa sababu haieleweki.

Wakati tukijadili hayo, mmoja wetu akasema matokeo ya Simba yasichukuliwe kama “msiba wa Taifa” bali ni kipigo cha timu moja.

Kwa kiasi fulani alionekana kama si mzalendo, lakini kadri nilivyotafakari nikaona alikuwa na hoja.

Hebu tuangalie safari ya Simba kwenye michuano hiyo mikubwa ya klabu barani Afrika.

 

Matokeo tofauti

Simba iliyoishinda Nkana Red Devils ilikuwa na makosa mengi ambayo yalisahaulika baada ya lile bao la tatu, ambalo ‘muvu’ yake ilianza wakati wachezaji wa Zambia wakibishana na mwamuzi na kujikuta wakitoa mwanya kwa Simba kuanza mpira harakaharaka na hivyo kukuta Wazambia hawajajipanga vizuri.

Lakini Simba ilikuwa tofauti ilipokuja kucheza mechi ya kwanza ya hatua ya makundi dhidi ya AJ Soura ya Algeria. Ilionyesha kiwango cha juu cha soka. Umakini, umiliki wa mpira, ujanja kwa washambuliaji hasa kwenye mitego ya kuotea na uwezo wa wachezaji kuutafuta mpira kwa nguvu kila walipoupoteza.

Kwa hiyo ushindi wa mabao 3-0 ulinogesha tu burudani safi kwa mashabiki ambao tayari walisharidhishwa na kiwango bora cha wachezaji wao siku hiyo.

Lakini Simba iliyowadhibiti Waarabu hao kwa kila hali, kiasi cha kocha wao kulalamikia vyombo vya habari vilivyowapachika mabingwa hao wa Tanzania hadhi ya “under dog”, haikuwa ile iliyopambana na AS Vita nchini Congo.

Ubora wote ulioonyeshwa Uwanja wa Taifa, haukuonekana hata chembe yake mbele ya wakongwe hao wa Congo. Mabeki hawakuwa wakijipanga kimkakati kila waliposhambuliwa, mipira ya kona ilikuwa nusu goli na ilizaa mabao mawili.

Katika mabao hayo mawili, wachezaji wa Vita walicheza kwa maelekezo. Walipopata kona walienda kusimama mbele ya kipa Aishi Manula. Mabeki wa Simba hawakuona kuwa hilo ni tatizo. Badala ya kwenda kuwaondoa wale wachezaji wa Vita, walikwenda kujipanga kusubiri kona na wakasahau kuwachunga wale waliojipanga nje ya miguu 12.

Na mara zote waliacha shimo lililotumiwa na Vita kufunga mabao ya kichwa bila bughudha.

Pia mara zote viungo walionekana kuchelewa kurejea kusaidia safu ya ulinzi kila walipopokonywa mpira. Na mara nyingi Wakongo walipitishia mipira katikati wakati wakishambulia, hali iliyoonyesha viungo hawakuwa wakijipanga vyema mbele ya mabeki kubana mianya.

Pia kasi ilikuwa ndogo na wachezaji walitaka kupiga pasi nyingi wakati wakielekea golini, jambo ambalo Vita walilichukulia kuwa jema kwao na hivyo kupata nafasi ya kurudi mapema kuongeza idadi ya watu mbele ya lango.

Na hayo ndiyo yaliyotokea Jumamosi. Makosa mengi yalijirudia na yakaadhibiwa na Wamisri.

Wakati mshambuliaji wa Al Ahly anapokea kona fupi na kugeuka na mpira, kulikuwa na wachezaji nane wa Simba ndani ya eneo la miguu 18, au la penati, dhidi ya wachezaji watano wa Al Ahly. Lakini watano walijilundika kwenye mstari ndasni ya kiboksi cha miguu sita huku wakimkodolea macho mchezaji wa Ahly aliyekuwa akitafuta jinsi ya kupiga krosi kwa wenzake waliojipanga kimkakati nje ya alama ya kupigia penati wakichungwa na mchezaji mmoja wa Simba.

Kwa hiyo ilikuwa rahisi kwao kumuondoa huyo mchezaji mmoja eneo hilo na hivyo kuacha shimo lililotumiwa kupiga kichwa kufunga bao hilo. Wachezaji wote wa Simba waliokuwa eneo hilo walikuwa wanaangalia mpira badala ya kuchunga wachezaji waliokuwa hawana mpira.

Hata bao la pili lilifungwa wakati wachezaji sita wa Simba wakiwa ndani ya eneo la penati, lakini ni mmoja tu aliyekuwa karibu na mpira na hivyo kuwarahisishia Waarabu watatu kugongeana one-two dhidi ya beki mmoja kabla ya kumpa mfungaji ambaye alionekana kama ameotea, kumbe Asante Kwasi aliua offside kwa kuchelewa kutoka golini.

Bao la tatu pia lilifungwa wakati Simba ikiwa na mabeki watano ndani ya eneo la penati. Wote wakiendelea na tatizo la kumkodolea macho mchezaji mwenye mpira na kusahau waliokuwa hawana mpira. Wawa, aliyekuwa kati hakuwa na macho manne kuangalia nani angeweza kuja alipo ili kutafuta mwanya wa kufunga. Alielekeza macho yake kwenye mpira na kustukia Mwarabu akidokolea wavuni krosi ya chini ambayo Wawa alidhani ingemfuata na kuokoa kirahisi.

Hali ilikuwa ile ile kwa bao la nne. Wachezaji sita walikuwa ndani ya eneo la penati wakati winga wa kulia wa Ahly akitafuta mbinu za kumtoka Kwasi. Wenzake Kwasi hawakushughulika wachezaji wa Ahly waliokuwa nje ya eneo hilo. Hadi krosi inapigwa, wachezaji watatu wa Ahly walikuwa wameshaingia ndani ya eneo la hatari na mmoja kuuwahi mpira mbele ya Wawa.

Bao la tano linaonyesha udhaifu wa viungo ambao walimuacha mchezaji wa Ahl aifuate ngome ya Simba hadi alipoikuta iko flat na kumburuzia pasi mshambuliaji aliyetumia shimo lililoachwa wazi na Kwasi, ambaye badala ya kumzonga, kwanza aligeuka kumwangalia mwamuzi msaidizi na alipogeuka, goli lilikuwa limeshafungwa.

Kwa hiyo, makosa ambayo yalijionyesha katika mechi ya Vita ndiyo yaliyojirudia na pengine kuongezeka katika mechi ya Ahly.

Kitu cha kujiuliza ni kwa nini viwango hivyo vya wachezaji wa Simba ni vya vipindi au havidumu? Ni kwa nini makosa yaleyale yanajirudia? Ni kweli kwamba kipigo cha Simba kinamaanisha kiwango duni cha soka la Tanzania au matatizo ya timu moja?

Simba imeondoka kwenda Misri ikiacha tuhuma kibao dhidi ya wachezaji kwamba hawatulii usiku. Muda ambao walipaswa kupumzisha mwili na akili zao, wanautumia kula bata na baadhi wamekuwa sugu hadi wanarejea hotelini alfajiri, wakidhani vipaji walivyojaliwa vitalinda kiwango na si nidhamu ya kuutunza mwili na kuzingatia mazoezi.

Habari zilisema kuwa ukaguzi uliofanywa na viongozi kambini, ulikuta ni wachezaji saba tu waliokuwa wamepumzisha miili yao hotelini. Hawa watawezaje kutunza afya zao kwa ajili ya kukabiliana na timu kama Al Ahly?

 

Nyingine zinaimarika, Simba inadoda

Wakati timu nyingine kwenye kundi; Soura, Ahly na Vita zinakuwa bora kadri zinavyoendelea kucheza, Simba ndiyo inashuka kiwango. Ahly alianza na ushindi finyu dhidi ya Vita na ambao ulipatikana baada ya mchezaji wa kiungo wa Vita kuonyeshwa kadi nyekundu.

Ililazimishwa sare na Soura katika mechi ya pili kabla ya kupata ushindi huo mnono.

Hata Soura ilianza kwa kufungwa mabao 3-0 na Simba jijin I Dar es Salaam na baadaye nusura iizamishe Ahly nchini Algeria kabla ya kulazimishwa sare. Katika mechi ya tatu dhidi ya Vita ililazimisha sare ya mabao 2-2 nchini Congo.

Vita ilianza kwa kipigo tata mbele ya Ahly, ikapata ushindi mnono dhidi ya Simba kabla ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 nyumbani na Soura, wakati Simba ilianza kwa ushindi na imepata vipigo vikubwa katika mechi mbili zilizofuata.

Yaani katika kundi, ni Simba pekee ambayo ilianza vizuri, ikashuka katika mechi mbili zilizofuata. Kwa nini kiwango kisipande hata baada ya wachezaji kukaa pamoja kwa muda wote?

 

Kutocheza mechi za ligi kunaiponza

Kwa kuangalia mechi za ligi za nyumbani, ni Simba pekee ndiyo ina kiporo kikubwa kulinganisha na timu nyingine za kundi lake, yaani cha mechi tisa wakati timu nyingine zina tofauti ya mechi hadi mbili tu kwenye nchi zao. Iweje Simba isifanye vizuri baada ya kupata muda wote huo wa maandalizi?

Kutocheza mechi za ligi ya nyumbani kuna athari kubwa kwa timu inayoshiriki michuano ya kimataifa. Kwanza kocha anakosa kupata uhalisia wa hali ya wachezaji kukabiliana na mechi baada ya mazoezi. Hawezi kupima mipango yake anayowapa wachezaji mazoezini inakubali vipi katika mechi uwanjani.

Hawezi kujua makosa ya wachezaji kwenye mechi kwa kuwa timu haichezi mechi za ligi. Badala yake anakutana na matatizo yote hayo kwenye mechi na anakuwa hana muda wa kuyatatua, kitu ambacho angeweza kuwa anakirekebisha kila baada ya mechi ya ligi na hivyo kwenda kwenye mechi ya kimataifa akiwa ameshughulikia angalau asilimia 70 ya matatizo aliyoyaona kwenye mechi za ligi ya nyumbani.

Na hii imekuwa tabia ya klabu zetu kutaka kutocheza mechi za nyumbani wakati zinaposhiriki michuano ya kimataifa kwa madai kuwa eti zinahitaji muda wa kutosha wa maandalizi. Hii si sawa.

Hata tulipoipeleka timu ya Taifa nchini Afrika Kusini kwa maandalizi ya mechi ya Lesotho, tulifanya kosa. Maandalizi ya siku hizo ni ya siku chache; mbili au tatu. Mchezaji wa Taifa anajiandaa vizuri zaidi anapocheza mechi za ligi akiwa na klabu yake badala ya kufanya mazoezi ya siku kumi bila ya kucheza mechi.

Kwa hiyo, kama alivyosema yule mwenzetu, kipigo hicho cha Simba kinaweza kisibebe taswira nzima ya soka la Tanzania na ndivyo anavyoamini kocha wa Soura. Kwa matatizo niliyoyachambua hapo, inawezekana kabisa kwamba yakirekebishwa Simba inaweza kufanya vizuri mbele ya Ahly na kauli zetu zikabadilika.

Kwa hiyo ni muhimu kuchambua mchezo hadi mchezo kujua matatizo ya mechi ili kupata picha halisi ya nini kimetokea na nini kifanyike.



Columnist: mwananchi.co.tz