Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHAMBUZI: Katiba Mpya muhimu kulinda wananchi

36918 Elius+Msuya UCHAMBUZI: Katiba Mpya muhimu kulinda wananchi

Thu, 17 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katiba ya Tanzania ibara ya 8 (1) inasema, “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake kutoka kwa wananchi.

Katiba pia inaongeza kuwa, lengo kuu la serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi; Serikali itawajibika kwa wananchi na wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali yao kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.

Pamoja na kuwapo vifungu hivyo, bado kumekuwa na hofu ya kupungua kwa mamlaka ya wananchi. Si ajabu kuona viongozi waliopewa madaraka kupitia uchaguzi ndio wenye madaraka kuliko waliowapa hayo madaraka.

Madaraka ya wananchi yalikuwepo tangu Tanganyika ilipopata uhuru Desemba 9, 1961 wakati ambao hata mfumo wa vyama vingi ulikuwepo. Chama cha Tanu ilipambana na vyama vingine hadi kikashinda uchaguzi ndipo kikaongoza Serikali.

Lakini ilipofika mwaka 1965, madaraka ya wananchi yakaanza kupunguzwa, kwa kuufuta mfumo wa vyama vingi na kuvibakiza vyama vya Tanu na ASP peke yake.

Kwamba hata wagombea urais hawakuwa na upinzani bali waligombea pekee.

Ilipofika mwaka 1975 chama cha Tanu kikashika hatamu za uongozi ambapo idara zote za Serikali zikatakiwa kufanya kazi kwa kutekeleza mwongozo wa chama hicho.

Mwaka 1977 licha ya kupitishwa kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayotumika hadi sasa, vyama vya Tanu na ASP vilipoungana na kuunda CCM, madaraka ya chama pia yakaongezeka.

Hadi mwaka 1992 mfumo wa vyama vingi unarusishwa, bado CCM ilikuwa madaraka makubwa tu na wananchi nao walishalishwa kasumba hiyo. Ndiyo maana hata kwenye matokeo ya Tume ya Jaji Nyalali karibu asilimia 80 ya Watanzania walitaka mfumo wa chama kimoja uendelee.

Lakini Mwalimu Julius Nyerere kwa kujifunza makosa ya mfumo ule, aliwashawishi wenzake waukubali mfumo wa vyama vingi. Haikuwa rahisi kwa viongozi wa CCM kukubaliana na Nyerere, lakini pia hawakuwa na namna ya kumkatalia.

Licha ya mfumo wa vyama vingi kuruhusiwa, bado mambo mengi hayakubadilishwa ili kuridhia mfumo huo.

Pamoja na kuwa Katiba hiyo iliongezewa vifungu vinavyotambulisha Tanzania kama nchi inayofuata mfumo wa vyama vingi, bado iliacha madaraka makubwa kwa Rais kufanya teuzi katika nafasi nyingi, ikiwamo pia wakuu wa Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC).

Nafasi hizo zimeendelea kunufaisha chama kimoja na vyama vya upinzani vimebaki kama watoto yatima. Vilevile kumekuwepo na utungwaji wa sheria zinazolalamikiwa kuminya uhuru wa wananchi kujieleza, kukusanyika na kutoa maoni yao kama sheria ya makosa ya mitandao ya 2015, Sheria ya Takwimu na ya Huduma za Habari.

Kama hiyo haitoshi, sasa unakuja muswada wa sheria ya vyama vya siasa, huo nao unatishia utekelezaji wa demokrasia ya vyama vingi.

Madaraka ya wananchi ndiyo ni haki ya kikatiba, ndiyo maana kuna haja ya kuwa na mabadiliko ya Katiba ili kuipa nguvu zaidi ya kulinda haki za wananchi.



Columnist: mwananchi.co.tz