Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHAMBUZI: Jifikirie ukikaa katika upande wa upinzani

59802 Pic+upinzani

Sun, 26 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moja ya njia nzuri ya kupima ikiwa unafanya jambo sahihi au la ni kuligeuza lile jambo liwe upande wako, kisha ukajiuliza; likifanyika hivi kwangu nitaridhika?

Mfano, ukiwa unapenda kuchepuka, inabidi ujiulize; mwenzako naye akichepuka na ukagundua utaridhika na kunyamaza?

Kwa kutumia njia na mifano hiyo, sasa tengeneza tukio la kufikirika. Chukulia ni chama tawala cha siasa kimeanguka katika uchaguzi mkuu na kimekuwa chama cha upinzani kama ilivyokuwa Kanu ya Kenya, UNIP ya Zambia na vingine.

Fikiria kwa mazingira ya siasa za Afrika hali itakuwaje.

Tukiwa tumebaki katika nadharia hiyo. Tukichukue mfano wa mazingira ya hapa kwetu, mfano CCM imeanguka na chama kimoja cha upinzani, mfano Chadema kimekaa katika kiti cha utawala.

Kisha yanatokea maamuzi yanayovitokea vyama vya upinzani kama kuzuia mkutano ya kisiasa na kisha viongozi wa Serikali kusifia sera za chama chao kila kukicha na kukipigia chapuo mbele ya mamia au maelfu ya Watanzania katika kila mkoa waendako.

Pia Soma

Wengine, ikiwamo CCM wakitaka kufanya mikutano ya aina hiyo watuhumiwe wanataka kuharibu amani ya nchi. Wakamatwe, washtakiwe kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Polisi wanaolinda mikutano ya chama tawala na ndio haohao watumike kutawanya au kuzuia mikutano ya vyama pinzani.

Fikiria na utaratibu ni uleule wa kufanyika mikutano ya ndani na ile ya wabunge na madiwani tu katika majimbo yao.

Ila baadaye taarifa zinaripoti viongozi kadhaa wa Chadema wamefanya mikutano ya hadhara katika mikoa isiyo hata majimbo yao au maeneo yao ya kazi.

Ila wapinzani ikiwamo CCM wakijaribu kuiga kama alivyofanya viongozi wa Chadema na kufanya mikutano ya hadhara wakamatwe na kushtakiwa au baadaye kuachiwa bila masharti.

Pia, ile mikutano ya ndani ambayo imeruhusiwa, bado wenzao wakitaka kuifanya wanakutana na vigingi vya polisi, wakati mwingine huzuiwa kabisa wasifanye.

Fikiria wakati huo mikutano ya ndani ya Chadema haikutani na kigingi hata cha bahati mbaya.

Kwao amani iwe inatawala mwanzo wa mkutano hadi mwisho. Hakuna purukushani za polisi. Hakamatwi mtu, ila viongozi wa ‘upinzani’ wakamatwe mara kwa mara kutokana na “taarifa za kiintelijensia”.

Iwe kwamba wapinzani wanapotaka kutumia haki yao ya kikatiba kufanya maandamano kupinga zuio hilo na pia kupaza sauti zao wanakutana na katazo jingine kutoka viongozi wa Chadema.

Unadhani, CCM na wapinzani wenzao watakuwa radhi na kuzinyamazia siasa za namna hiyo?

Chukua mfano mwingine. Mahakama kuu hivi karibuni imepitisha uamuzi wa kubatilisha wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, jiji na manispaa kusimamia uchaguzi. Kwa sababu sheria ya kuwaruhusu inakinzana na sheria iliyopo katika Katiba ya nchi.

Baada ya uamuzi huo wa mahakama, serikali inafikiria kuikatia rufaa hukumu hiyo. Unadhani kuna siku CCM wataridhia bila malalamiko wakurugenzi wenye ufuasi wa ACT-Wazalendo, Chadema, CUF, TLP kuwa wasimamizi wa uchaguzi?

Uchaguzi unaotakiwa kuwa huru na haki, unapotokea anayesimamia hayuko huru, maana ni mfuasi wa upande mmoja wa ushindani.

Kweli utamtarajia mtu huyu kusimamia kwa haki shughuli nzima bila kupendelea chama chake?

Hapo ndipo inakuja hoja ya kila mtu kupima anachotenda kwa wengine kama kingeweza kupendeza kwa upande wake.

Naamini uamuzi wa mahakama ulitakiwa kupongezwa na serikali pia, kwani unaonesha mwanzo mzuri wa kuelekea katika chaguzi zilizo huru.

Hapana shaka kwamba Tanzania inahitaji Tume huru ya kusimamia uchaguzi. Huenda hilo likapunguza hii misigano inayotokea nyakati za uchaguzi.

Ukiyaagalia mambo haya ambayo kiukweli yanakinzana uhuru wa kisiasa na demokrasia safi, utaona mengine yamezuka karibuni na mengine yapo kwa muda mrefu ndani ya siasa zetu.

Hayafai kuwepo, kwa sababu yanaigeuza siasa kuwa ya majitaka ambayo haina faida yoyote kwa taifa.

Hapa ndipo wale wanaoamini siasa ni mchezo mchafu, wanapata kinywa kipana cha kusema na kutoa mifano iliyo hai kabisa katika siasa zetu.

Na hapo ndipo, kauli maarufu ya Rais John Magufuli, “maendeleo hayana vyama inatakiwa kuchu

kuliwa kwa uzito, kuzingatiwa na kufanyiwa kazi kwa vitendo.

Yaani mkurugenzi anapokabidhiwa mamlaka ya kusimamia uchaguzi atambue kuwa yeye anastahili kuwa mtu wa kati mwenye kutoa uamuzi wa haki unaoheshimika kwa pande zote.

Anatakiwa atambue kuwa hata yule anayemteua ni kwa mujibu wa Katiba, lakini akishateuliwa anatakiwa kutekeleza majukumu yake kulingana na sheria na Katiba inavyoelekeza. Ndio maana wapo wakurugenzi wanaosimamia majukumu yao bila upendeleo, ingawa kila uamuzi unaangaliwa kwa jicho la maslahi ya kipa upande.

Isiwe kwamba hukumu iliyowanyima fursa hiyo ambayo inatakiwa rufaa, iwe inashangiliwa na wapinzani lakini ionekane haifai kwa wafuasi wa chama tawala na serikali yake.

Columnist: mwananchi.co.tz