Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHAMBUZI; Jaji Warioba, ni kweli Tume yako iliishia kusikitika tu kifo cha Dk Mvungi?

33495 Pic+warioba Tanzania Web Photo

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Jaji Joseph Warioba ni miongoni mwa watu waliomfahamu vyema Dk Sengondo Mvungi na alibahatika kuwa miongoni mwa watu wa mwisho kufanya naye kazi. Dk Mvungi alikuwa mbobezi katika masuala ya Katiba. Mzee Warioba anajua umuhimu wa kuwa na Katiba Mpya katika nchi yetu na umuhimu wa watu kama Dk Mvungi katika nchi yoyote. Alikuwa ni mwenye kutaka sana maridhiano na hiyo ndiyo maana hasa ya Katiba ya nchi yoyote ambayo tunajua aliipigania sana. Kaulimbiu “Katiba ni Maridhiano” imeasisiwa na Dk Mvungi. Katiba ni maridhiano kati ya kiongozi na anaowaongoza, wananchi. Kwamba ataongoza kwa mujibu wa misingi waliyoiweka wao wananchi kwani kiongozi huyo anapata mamlaka hiyo kutoka kwao. Anawajibu wa kuwaheshimu tofauti na ilivyo leo.

Imani yangu ni kwamba, Wazee (kwa heshima ya nafasi zao si kwa umri) kama Jaji Warioba na wengine kibinadamu wanatamani sana siku moja ambayo ni hakika itakuja, waenziwe vyema. Binafsi najiuliza sana; kwa lipi? Maana mambo mengi waliyoyafanya kwa nafasi kubwa walizopata kushika katika nchi yetu ni ya kawaida sana kwa mzalendo yeyote kwa nchi yake. Ndiyo, Dk Mvungi alikuwa mzalendo kama wengine lakini si wa kawaida tu na hiyo inathibitishwa na Jaji Warioba mwenyewe, anasema katika kitabu cha rambirambi; “ Dk Sengondo Mvungi Anapumua Katiba”, uk 22 nanukuu;

“Tumempoteza mwenzetu , kwa hali ya kawaida anaonekana ni mtu mmoja amepotea, lakini kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Dk Mvungi alikuwa na umuhimu mkubwa. Dk Mvungi alikuwa na ya ziada.”

Tunashuhudia miswada mbalimbali kandamizi, mfano, juu ya sheria inayotarajiwa kuhusu vyama vya siasa na sheria nyingine zilizopitishwa na kusainiwa tayari kama ya habari na mitandao.

Katiba ni haki yetu na mchakato wake unapaswa kuhitimishwa kwani umeligharimu taifa rasilimali nyingi ambazo si za mtu fulani ambaye anaweza tu kuamua atupe au la. Kusema kweli, ili mje kustahili heshima mnayoitamani sana mnapaswa kwenda mbali zaidi ya hapo. Wazee wataondoka huku wakijua wanatuachia balaa la Katiba, kwa bahati nzuri walipewa nafasi ya kulirekebisha na kuwaachia Watanzania na vizazi vyao ‘andiko la maridhiano’ (Katiba) la uhakika na makini katika uendeshaji wa nchi yetu, kutuondolea utamaduni unaoendelea kuota mizizi wa kuendesha nchi kwa misingi ya utashi wa mtu mmoja. Shabaha ya wananchi ya kudai andiko la maridhiano kama alivyosisitiza Dk Mvungi na wale watakao omba ridhaa ya kutuongoza hata kuanzishwa kwa mchakato kwa kuundwa Tume ya Marekebisho ya Katiba (Tume ya Warioba) ilikuwa ni kupata Katiba Mpya. Ni muhimu Rais John Magufuli akatafakari mtazamo wake kuhusu Katiba kama hitaji la wananchi badala ya kuwaambia kuwa hakuwahi kuinadi wala kuwa moja ya vipaumbele vyake.

Dk Mvungi aliuawa akipigania Katiba. Alishambuliwa Novemba 11, 2013 nyumbani kwake Mpiji Magoe na kuaga dunia kufuatia majeraha aliyoyapata Novemba 12, 2013 hospitali ya Milpark nchini Afrika Kusini na hatimaye kuhifadhiwa kwenye nyumba yake ya milele Novemba 18, 2013 kijijini kwao Mwanga mkoani Kilimanjaro. Alizaliwa siku ya watakatifu wote Novemba 1, 1952 kitongoji cha Chamakera, Kilimanjaro. Ni miaka mitano imetimia na Tume ya Warioba ambayo tayari imevunjwa na Serikali baada ya kumaliza kazi yake haijawahi kumuenzi. Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi na ambaye alikuwa miongoni mwa marafiki wa karibu sana wakimtambua kama “nguto” yaani “chui”.

Katika kuhitimisha rambirambi yake Profesa Kabudi anasema uk. 145, nanukuu;

“Huzuni iliyoje kuwa mtetezi huyu aliyetumia maisha yake kuondoa dhuluma, leo tunamuaga akiwa mshirika wa mfumo wa dhuluma uliotanda, mfumo aliopambana kwa hali na mali kuuondoa. Dk Mvungi asingetaka tumlilie, bali angetuasa tuendeleze mapambano na kuhakikisha kuwa utu na heshima ya mwanadamu unakuwa ndio utamaduni wa Mtanzania.”

Niwatie moyo, hatujachelewa bado. Tunayo nafasi ya kukamilisha na kuhitimisha mchakato wa Katiba na hivyo kuwapatia Watanzania andiko la maridhiano kwa mustakabali mwema na ustawi wa nchi yetu.

Gregory Urima; 0789 213 141 au 0714 487 789: Barua pepe; [email protected]



Columnist: mwananchi.co.tz