Tanzania inatumia mfumo gani wa kisiasa? Hilo ni swali ambalo halikupata jibu miongoni mwa wasomi na kuibua mawazo kinzani juu ya mfumo unaotumika – ni ama ujamaa au ubepari utakaosaidia kufanikisha maendeleo yatakayowagusa wananchi wa chini?
Katika mhadhara wa tano wa Kavazi la Mwalimu Nyerere wa mwaka huu, uliowakutanisha wasomi wa ndani na nje ya nchi walitumia muda mwingi kutathmini juu ya mfumo gani ambao nchi hii inautumia kwa sasa na endapo una tija kwa wananchi.
Mhadhara huo ulihutubiwa na mtaalamu wa siasa kutoka nchini India, Profesa Prabhat Patnik ambaye alianza kwa kuchambua mifumo mikuu miwili, ujamaa na ubepari ambayo kwa vipindi tofauti, ilishika hatamu mara baada ya nchi za Afrika kupata uhuru.
Profesa Patnik ambaye ni muumini wa siasa za mrengo wa kijamaa, anasema mfumo wa uchumi wa kibepari ambao ndio ulikuwa mbadala kwa nchi nyingi, haujarandana na matarajio ya nchi za Afrika, katika kuwaletea maendeleo watu wake wakiwamo wakulima wadogo.
Anasema mfumo huo ni kandamizi kwa wazalishaji wadogo kwa kuwapoka ardhi ambayo ndiyo nyenzo muhimu ya uzalishaji. Anabainisha kuwa ardhi hutolewa kwa wawekezaji wakubwa huku wadogo wakibaki vibarua.
Tofauti na ubepari, anasema mfumo wa kijamaa unahimiza katika kulinda na kusimamia maslahi ya wananchi hususan kwa kuwapa mamlaka ya kumiliki nyenzo za uzalishaji ili wawe kiungo kikuu cha kuleta maendeleo ya kweli.
Tanzania baada ya kupata uhuru iliamua kuingia katika mfumo wa kijamii ukiratibiwa na Azimio la Arusha la mwaka 1967 chini ya chama cha Tanu. Moja ya misingi yake ilikuwa ni wananchi kumiliki nyanja za uzalishaji pamoja na kuleta misingi ya usawa.
Hata hivyo, mfumo huo haukufua dafu baada ya athari za kiuchumi zilizojitokeza kwenye mataifa ya kijamaa yakiongozwa na Urusi miaka ya 1980.
Mtaalamu huyo anasema nchi zilizoamua kuchukua mfumo wa kibepari zimeendelea kuwa nyuma kimaendeleo kutokana na mfumo huo kutowapa mamlaka watu wa chini kujenga uchumi wao, badala yake wanageuzwa kuwa tegemezi kwenye mashirika ya kigeni.
“Kampuni zinapokuja kuwekeza, zinachukua ardhi kwa wazawa na kuwalipa fidia ambayo si endelevu, hakuna faida ambayo mkulima ataipata kutokana na uwekezaji, badala yake wanaondolewa kwenye maeneo yao na kugeuka vibarua,” anatahadharisha.
Anaongeza, “Ujio wa ukoloni mamboleo umeibua matatizo mengi kwa wakulima wadogo na kufifisha uwezo wa taasisi za tafiti za ndani,” anasema.
Hata uhaba wa chakula kwenye mataifa ya Kiafrika, msomi huyo anasema umetokana na mifumo kandamizi inayowalazimisha wakulima kulima mazao ya kibiashara na kusahau mahitaji yao ya chakula.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, Tanzania na nchi nyingine za Kiafrika haziwezi kumaliza umasikini kama zitaendelea na mifumo ya kibepari inayowapuuza wakulima wadogo.
Wakati akisema hayo, swali kubwa lililoibuka ni je, Tanzania ipo katika mfumo gani? Swali ambalo liliibua mvutano miongoni mwa wachangiaji wa mjadala katika ukumbi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech).
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa Issa Shivji anasema ‘bila kumung’unya’ maneno kuwa Tanzania ipo katika mfumo wa ubepari, lakini akionyesha shaka juu ya namna mfumo huo unavyoendeshwa.
“Mfumo tunaofuata ni mfumo wa kibepari, isipokuwa ubepari huo unaozungumziwa ni ubepari uchwara, sio ubepari wa Kitaifa. Uwezekano wa kujenga ubepari wa kitaifa haupo,” anasema.
Anataja sababu za kukwama kwa mfumo huo kuwa ni kushindwa kujenga soko huria ambalo kimsingi wazawa hawanufaiki na pili ni kushindwa kujiendesha kwa sekta binafsi hususan viwanda ambavyo awali vilikuwa chini ya Serikali.
“Tukazungumza uchangiaji wa huduma za jamii lakini elimu imeshuka, afya imeshuka, maji hayapatikani. Ndio hali halisi tuliyonayo sisi. Vijana wa mjini zaidi ya 30,000 ni machinga, ndio ubepari huo,” anasema.
Anaongeza kuwa kupitia ubepari, umasikini umezidi kuongezeka huku uchangiaji wa pato la Taifa kwa watu wa chini ukizidi kushuka.
Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa wa UDSM, Dk Ng’wanza Kamata anasema kuna haja ya kuhuisha misingi ya Azimio la Arusha kwa ajili ya kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wanyonge.
Hata hivyo, baadhi ya wachangiaji wanahoji endapo Tanzania inaweza kuachana na ubepari na kuanza kufuata misingi ya kijamaa, jambo ambalo linaonekana kuwa gumu kutokana na mazingira ya kiuchumi duniani.
Profesa Patnik anahitimisha kwa kueleza kuwa kujenga mfumo wa kijamii si jambo la siku moja. Ni mchakato mrefu ambao unahitaji utayari wa wananchi.