Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHAGUZI MKUU 2020: Wagombea 58 Tanu wapita bila kupingwa mwaka 1960

99274 Tanu+pic UCHAGUZI MKUU 2020: Wagombea 58 Tanu wapita bila kupingwa mwaka 1960

Tue, 17 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika Uchaguzi Mkuu wa pili wa mfumo wa vyama vingi uliofanyika Jumanne ya Agosti 30, 1960, chama cha Tanganyika African National Union (Tanu), kiliwapitisha wagombea wake 58 bila kupingwa. Walikuwamo Wazungu wanane, Waasia 11 na Waafrika 39.

Kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa mwaka 1958/59, vyama vingi vilishiriki uchaguzi huo.

Chama kilichoshindana na Tanu ni cha African National Congress (ANC) kilichokuwa kikiongozwa na Zuberi Mtemvu.

Hata hivyo, tangu kuanzishwa kwake Julai 7, 1954, Tanu ilionyesha shauku ya kushinda katika chaguzi mbalimbali zikiwamo zile za 1958 na 1960 na kisha kuunda serikali ya kwanza ya Tanganyika huru.

Ingawa ushindi kwa Tanu ulikuwa mkubwa kuliko ilivyotarajiwa awali, kiongozi wa ANC, Mtemvu alilaumu matumizi ya utaratibu wa kikoloni kuchagua viongozi wa Kiafrika na kuwataka wote waliochaguliwa wajiuzulu nyadhifa zao.

Kwa mujibu wa mwandishi Ronald Aminzade ‘Race, Nation, and Citizenship in Postcolonial Africa: The Case of Tanzania’ (uk. 74), Waasia na Wazungu 21 walioingia katika Bunge hilo hawakukubaliwa kujiunga na Tanu ingawa chama kiliwaunga mkono katika kugombea kwao.

Pia Soma

Advertisement
Wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka huo, kulikuwa na vitisho kwa wageni waliokuwa Tanganyika, lakini Kiongozi wa Tanu, Mwalimu Julius Nyerere alizunguka nchi nzima kufanya kampeni na kuwakumbusha wafuasi wake kwamba uwekezaji wa wageni ulitegemea hali ya utulivu na amani ya nchi na kuwahakikishia Wazungu na Wahindi kuwa Tanganyika haitakuwa kama Congo.

Kipindi hicho kulikuwa na machafuko ya kisiasa yaliyosababisha mauaji ya aliyekuwa Waziri Mkuu wake, Patrice Lumumba.

Taarifa hizo za Mwalimu Nyerere zilichapishwa katika Gazeti la ‘Mwafrika’ la Agosti 15, 16, 25, mwaka 1960 na katika Gazeti la Ngurumo la Agosti 20, 1960.

Kazi ya gazeti la Mwafrika ilikuwa ni kueleza maoni ya Tanu kwa wananchi na watu wa Tanganyika. Kutangaza matukio muhimu ya Tanu na kuwaandaa watu wa Tanganyika chini ya chama hicho.

Hofu ya kushambuliwa kwa wazungu na Wahindi ilisababisha kuzushwa kwa uvumi kwamba watumishi wengi wa Serikali wa asili hiyo walikuwa wakiondoa familia zao nchini kwa hofu ya kutokea kile kilichotokea Congo.

Hata hivyo, Nyerere aliwahakikishia watumishi hao kuwa jambo kama hilo halitatokea.

Gazeti la Tanganyika Standard toleo la Agosti 5, 1960 lilimkariri Mwalimu Nyerere akisema mambo ya Congo hayataweza kamwe kufanyika Tanganyika na kwamba, “wahuni wanaowatishia watu” kwa namna yoyote hawatavumiliwa.

Katika maeneo yaliyokuwa na wagombea 25 kati yao 11 walisimamishwa na Tanu na wote walishinda isipokuwa mmoja tu wa kiti cha Mbulu ambako Chief Amri Dodo, aliyekuwa mgombea wa Tanu, alishindwa na Herman Elias Sarwatt ambaye alikuwa mgombea binafsi.

Viti 50 vilikuwa wazi kwa wagombea wote, lakini viti 10 vilikuwa kwa ajili ya Wahindi na 10 vya wazungu.

Ili kupiga kura ilikuwa sharti uwe na uwezo wa kusoma na kuandika kwa Kiswahili au Kiingereza.

Na mgombea ilikuwa awe na kipato cha angalau dola 210 (Sh479,850/- kwa kiwango cha sasa).

Kwa mujibu wa mwandishi Henry Bienen katika ukurasa wa 55 wa kitabu Tanzania: Party Transformation and Economic Development,’ kulikuwa na wapiga kura 885,000 waliokuwa wamejiandikisha. Wagombea 58 wa Tanu walipita bila kupingwa. Miongoni mwao, 39 walikuwa Waafrika.

Katika kinyang’anyiro hicho, Tanu ilipata viti 12 kati ya 13 vilivyogombewa.

Awali, Sarwatt alikuwa mwana-Tanu na pia alipitishwa na tawi la Mbulu kugombea nafasi hiyo, lakini alikataliwa na makao makuu ya chama.

Tanu ilipata ushindi wa kura 100,581 kati ya 121,445 zilizopigwa, hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 82.8 ya kura zote zilizopigwa. Chama cha ANC kilichokuwa kikiongozwa na Mtemvu kilipata kura 337, sawa na asilimia 0.3 na wagombea binafsi wakapata kura 20,527, sawa na asilimia 16.9.

Sarwatt alipata karibu theluthi moja ya kura zote za wagombea binafsi.

Ingawa walijiandikisha wapigakura 885,000 na wakajitokeza 121,445, ilielezwa kuwa kilichosababisha kukawepo na idadi ndogo ya waliojitokeza kupiga kura ni wagombea wengi wa Tanu kupita bila kupingwa.

Miongoni mwa wabunge waliopita ama bila kupingwa au kwa kugombea na wapinzani wao ni pamoja na Mwalimu Julius Nyerere (Dar es Salaam), Rashidi Mfaume Kawawa (Nachingwea), Derek Noel Maclean Bryceson (Dar es Salaam), Clement George Kahama (Bukoba) ambaye amezoeleka kuitwa kwa jina la Sir George Kahama, Amir Habib Jamal (Morogoro) na Paul Lazaro Bomani (Mwanza).

Wengine walioshinda vni Asanterabi Zephaniah Nsilo Swai (Arusha), Oscar Salathiel Kambona (Morogoro), Tewa Saidi Tewa (Kisarawe), Job Marecela Lusinde (Dodoma), Jeremiah Kasambala (Rungwe), Solomon Nkya Eliufoo (Moshi) na Chifu Abdallah Said Fundikira (Tabora).

Pia alikuwamo Michael Kamaliza (Kilosa), Saidi Ali Maswanya (Kahama), Chifu Erasto Mang’enya (Tanga Coast), Lawi Nangwanda Sijaona (Lindi), Elias Amos Kisenge (Pare), Al Noor Kassum (Dodoma), Isaac Muller Bhoke Munanka (North Mara), Austin Shaba (Mtwara) na Sheikh Amri Kaluta Abeid (Kigoma).

Wengine walioshinda katika uchaguzi huo wa 1960 ni Barugira Edward Munyagi Barongo (Busubi), John Benedict Mugogo Mwakangale (Mbeya), John Anderson (Masasi), Richard Saimura Wambura (Maswa), Samuel Seyid Chamshama (Lushoto), Mtemi Louis Paul Dantes (Ufipa), Ali Saidi Mtaki (Mpwapwa), Waziri Dossa Aziz (Bagamoyo), Kheri Rashid Baghdelleh (Kilwa), A.S.Bajaj (Iringa), na Arthur Leslie Brise Bennett (Moshi).

Pia walikuwamo Nicus Buhatwa (Ukerewe), Lady Chemsham (Iringa), Martin Haule (Kondoa), Mohamedali Natha Hirji (Moshi), Kantilal Laxmichand Jhaveri (Dar es Salaam) na Bi Barbro Cecilia Johansson (Mwanza) ambaye ni mzaliwa wa Sweden katika mji wa Malmo. Aliingia nchini Tanganyika mwaka 1946.

Wengine ni C. M. Kapilima (Ulanga), Mohamed Kihere (Tanga Mjini), Dk Baldev Krishna (Tanga), Rajabu Mahami Kundya (Singida), Aristotle Matsis (Arusha), Philip Mbogo (Mpanda), Frank Mfundo (Handeni), Chief Mhaiki (Songea), John Aaron Mhaville (Njombe), Bibi Titi Mohamed (Rufiji), Francis Vincent Mponji (Tunduru), Samwel Msindai (Iramba) na Karl Tulo Mueller (Lushoto),

Walioshinda pia viti vya ubunge katika uchaguzi huo ni Shell Muhanna (Bukoba), Bartholomew Donai Mwiza (Geita), A. Nazerali (Lindi), Mwami Theresia Ntare (Kasulu), John Godfrey Rupia (Shinyanga) na R. F. Saidi (Newala.

Wengine ni pamoja na John Noli Samaras (Morogoro), A. Shot (Tabora), Dk Leader Dominic Stirling (Mbeya), F. L. Sumar (Tabora) na Godwin Tunze (Kibondo).

Pia alikuwapo Chifu Humbi Ziota (Nzega), Joseph Kizurira Burrito Nyerere (Musoma), Chifu Charles Masanja (Kwimba), Sophia Mustafa (Arusha) na Peter Saidi Siyovelwa (Iringa).

Columnist: mwananchi.co.tz