Watanzania tunalalamika. Mimi pia nimeambiwa mara nyingi kwamba ninaandika makala za kulalamika. Kuna Mheshimiwa mbunge mmoja aliyeniambia kwamba aliacha kusoma makala zangu kwa sababu kila nikiandika ni kulalamika. Aliniomba nitafute namna nyingine ya kuandika bila kulalamika. Ndio maana nilisita kuandika makala hii. Nilikuwa nikitafakari namna ya kuufikisha ujumbe huu; Tunawashukuru sana waliotutunzia fedha zetu benki za nje, sasa wakati umewadia warudishe fedha zetu; nilijua nikiandika, yatakuwa ni yale yale ya “Watanzania wanalalamika”. Nimewasikia wanasiasa wakikemea utamaduni wa kulalamika! Ingawa kwa kukemea kulalamika, wanafanya kitu kilele; ni kulalamika! Wabunge wana kazi ya kutunga sheria na kuisimamia serikali, lakini wakianza kuchangia ni kulalamika tangia mwanzo hadi mwisho.
Orodha ya yale yanayolalamikiwa ni kubwa. Tukisema Watanzania ni wazembe ni kulalamika, tukisema rushwa ni kansa ya taifa letu, ni kulalamika, tukisema wanaouza madawa ya kulevya ni watu wa hatari na hawana upendo na taifa lao, ni kulalamika? Tukitaka fidia ya nyumba zilizovunjwa kupisha ujenzi wa barabara ya njia nane Kimara- Kibaha ni kulalamika. Tukikataa kuwalipa ni kulalamika pia! Yawezekana Watanzania tunapiga kelele kwa Muumba wetu? Yawezekana tunaomboleza? Tukijua wazi kwamba hata tukikaa kimya kwa kuogopa kupachikwa jina la sifa za “kulalamika” hata mawe yatasimama na kuimba sifa za Mungu, aliyeumba mbingu na dunia. Tunajua wazi kwamba tukikaa kimya tutahukumiwa na historia.
Tumesikia habari kwamba kuna Watanzania wameficha fedha nyingi kwenye mabenki ya nje na hasa Uswisi. Na habari hizi si mpya, maana kuna wakati tulisikia kwamba kuna Mtanzania ameficha fedha nyingi kwenye benki ya Afrika Kusini. Habari zote hizi ni mwendelezo wa wimbo uleule wa kulalamika bila kupendekeza hatua za kuchukuliwa. Ndio maana nimeamua kuandika kwa mfumo mwingine wa kuwashukuru wale wote waliotusaidia kutuwekea fedha zetu kwenye benki za nje, tuna imani kwamba fedha hizo sasa hivi zimezaa kiasi cha kutosha, wakati umefika fedha hizo wazirudishe nyumbani ili tujenge taifa letu changa.
Ingawa hakuna mwenye kujua fedha hizo ni kiasi gani, lakini zinaweza kusaidia kulipa mishahara ya walimu, kulipia elimu ya juu, kununua vifaa vya kisasa kwenye hospitali zetu, kulipa mishahara ya madaktari na kusaidia kiasi fulani kuendesha bajeti ya serikali yetu.
Tushirikiane kupiga kelele na kushinikiza hadi fedha zetu hizi zilizowekwa kwenye mabenki ya Ulaya zirudishwe haraka iwezekanavyo.
Waliokuwa wanalalamikia serikali yetu kutokuwa na fedha, watagundua ukweli ambao siku zote tuliusimamia kwamba nchi yetu si maskini. Rais wetu akifanikisha zoezi hili la kurudisha fedha zetu zilizowekwa nje ya nchi kwa kutumia madaraka yote aliyonayo, atakumbukwa milele! Heri ya Mwaka mpya 2019.
Wazungu hawa wanashinikiza demokrasia na utawala bora; wanasisitiza uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma, Wazungu wamependekeza mipango mingi ambayo inaweza kuisaidia Tanzania kupiga hatua kubwa ya manedeleo. Itakuwaje wazungu hawa hawa wakae kimya wakiona fedha nyingi zinachotwa Afrika na kuwekezwa kwenye mabenki ya Nje? Ina maana wazungu hawa wanaamini kwamba wale wanaoweka fedha kwenye benki zao wanakuwa wamezitafuta fedha hizo kwa jasho lao? Inawezekana wana kaa kimya kulinda uchumi wa nchi zao? Inawezekana ni wao wanawashawishi watu wetu kuficha fedha hizo kwenye benki zao?
Kama walioficha fedha hizi ni wafanyabiashara, ambao wanajulikana kwa kufanya kazi kwa bidii na kuzalisha ziada, wafanyabiashara ambao wanalipa ushuru wao kwa uaminifu, ni lazima Rais wetu awe na kigugumizi cha kuchukua hatua dhidi ya watu hawa walioficha fedha kwenye benki za nje. Lakini kama wenye fedha hizi ni waajiriwa wa serikali ambao kipato chao kinategemea mshahara na posho, kwa nini Rais wetu awe na kigugumizi? Mfanyakazi wa umma atapata wapi fedha nyingi hivyo? Haiwezekani ukawa ni mshahara wake.
Ili kumsaidia Rais wetu abaki kwenye mstari wa kuhakikisha haki inatendeka, mstari wa kuhakikisha hakuna anayeonewa, wale watakaoweza kuhakikisha njia walizozitumia kujipatia kuyapata mamilioni hayo, basi waachiwe asilimia kidogo ya fedha hizo ili waweze kuendesha maisha yao na kufurahia matunda ya kazi zao. Lakini kama fedha hizi wamezipata Serikalini, zichukuliwe zote bila ya huruma yoyote ile. Washitakiwe kama wahujumu uchumi na sheria ifuate mkondo wake.
Naandika makala hii kupiga kelele juu mbinguni! Naandika makala hii kukukaribisha wewe msomaji wangu kuniunga mkono tukashirikiana kupiga kelele.
Tushirikiane kupiga kelele na kushinikiza hadi fedha zetu hizi zilizowekwa kwenye mabenki ya Ulaya, zirudishwe haraka iwezekanavyo. Wakati wa maneno umekwisha, enzi hizi ni za kuchukua hatua, ni enzi za kufanya maamuzi magumu.
Ingawa fedha hizi zilizofichwa nje ya nchi haziwezi kumaliza matatizo yetu yote; Hatua itakuwa imepigwa uongo na ukweli vitakuwa vimejitenga! Waliokuwa wanalalamikia serikali yetu kutokuwa na fedha, watagundua ukweli ambao siku zote tuliusimamia kwamba nchi yetu si maskini. Rais wetu akifanikisha zoezi hili la kurudisha fedha zetu zilizowekwa nje ya nchi kwa kutumia madaraka yote aliyonayo, atakumbukwa milele! Heri ya Mwaka mpya 2019.
Wakati wa siasa za kuchafuana umepita; wakati wa siasa za kugombania kuingia Ikulu kwa gharama yoyote ile unaelekea mwisho na wala hauna faida yoyote ile kwa maendeleo ya watanzania. Ni enzi za kutanguliza taifa letu badala ya kutanguliza matumbo yetu. Ni enzi za kulitanguliza Taifa letu badala ya kuvitanguliza vyama vyetu vya siasa, si wakati tena wa kujenga na kutafuta sifa za mtu mmoja mmoja, ni wakati wa kujenga jina la taifa letu la Tanzania. Ni enzi za kulitanguliza taifa letu badala ya kutanguliza mambo mengine yasiyokuwa ya msingi.
Ingawa fedha hizi zilizofichwa nje ya nchi haziwezi kumaliza matatizo yetu yote; Hatua itakuwa imepigwa uongo na ukweli vitakuwa vimejitenga! Waliokuwa wanalalamikia serikali yetu kutokuwa na fedha, watagundua ukweli ambao siku zote tuliusimamia kwamba nchi yetu si maskini. Rais wetu akifanikisha zoezi hili la kurudisha fedha zetu zilizowekwa nje ya nchi kwa kutumia madaraka yote aliyonayo, atakumbukwa milele! Heri ya Mwaka mpya 2019.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 6331 22.
[email protected]