Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tutake tusitake mabadiliko ni lazima

65468 Mabadiliko+pic

Thu, 4 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hakuna ubishi kwamba Mwalimu Julius Nyerere, ni kati ya wanasiasa na wanazuoni waliotamani mabadiliko na kufanya kazi kubwa kuyaleta. Aliyataka ndani ya nchi yake Tanzania, Afrika na dunia nzima.

Lakini mjadala wowote juu ya Mwalimu unakuwa tishio kwa wanasiasa wengi ambao nafsi inawashtaki kumsaliti na kusaliti mawazo. Wale walioukumbatia mfumo wa kibeberu na kuishi kwa ufadhili wa fikra na fedha za mabeberu. Wale wanaofikiri ujamaa ni mfumo wa maisha uliopitwa na wakati na utandawazi ni mfumo wa kisasa usioepukika.

Asilimia kubwa ya Watanzania na hasa vijana wa mijini na vijijini wanataka mabadiliko. Kwa vile mabadiliko ni ya aina nyingi, ni muhimu kusisitiza kwamba mjadala wetu umejikita zaidi kwenye mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kifkra.

Viongozi wetu wanatuelekeza upande wa kibepari, baadhi ya Watanzania na hasa vijana wanaosoma kwa shida, wakulima na wafanyakazi wanaonyonywa jasho lao; mjadala mzito juu ya Mwalimu, ujamaa na ubeberu ni hatari kwa malengo ya ‘watandawizi’.

Lakini, kwa vile ni dhambi kuikimbia historia yetu, ni lazima wachache tujitose kuyajadili yale ambayo masikio hayataki kusikia. Wasiopenda kusikia leo, watayasoma kesho au yatasomwa na vizazi vijavyo.

Maisha yake yote Mwalimu alipambana na maadui waliotishia uhuru na utu wetu. Aliongoza mapambano dhidi ya ujinga, umaskini, maradhi, rushwa ubeberu na ubaguzi kwa uaminifu na uadilifu.

Pia Soma

Siasa ya ujamaa na kujitegemea ilizaliwa kutokana na lengo lake kuu la kujenga jamii iliyo huru na inayoheshimika. Makosa ya hapa na pale yalijitokeza wakati wa kuitekeleza, mfano kuwahamishia watu kwenye vijiji vya ujamaa bila mipango mizuri, lakini kwa ujumla wake malengo yalikuwa mazuri.

Ingawa sasa hivi makosa haya yanaligharimu Taifa letu, lakini yalifanyika kwa nia njema, haya yanaitwa makosa yenye heri.

Kama tunavyokumbuka Mwalimu, aliungama dhambi mbili katika maisha yake. Na alisema angepata nafasi ya kuiongoza tena Tanzania, angefanya chini juu kusahihisha makosa ya “Kudhoofisha Serikali za mitaa na kudhoofisha vyama vya ushirika”. Lakini, pia akaacha wasia kwamba bila umoja wa kisiasa, ‘vinchi’ vyote vya Afrika vingesambaratika na bila Muungano imara jamii za Zanzibar na Tanganyika zitasambaratika.

Mwalimu alituomba kuacha mabaya yake na kuyachukua mazuri yake. Ni kiasi gani tumeyaacha mabaya yake? Ni kiasi gani haturudii makosa kama aliyoyafanya? Ni mikakati gani ya vyama vinavyotafuta ridhaa ya kuitawala Tanzania vinapigania mabadiliko katika mfumo wa Serikali za mitaa ili ziwe imara na ziweze kujiendesha bila kuingiliwa na Serikali kuu?

Ni kiasi gani hadi leo hii Serikali inawajibika kwa wananchi? Je, wananchi wanajua kwamba wao ndio msingi wa mamlaka yote na madaraka katika nchi?

Ni mipango mingapi ya Serikali imefanyika kwa kuzingatia ustawi wa wananchi wake? Ni kiasi gani wananchi wamekuwa wakishirikishwa shughuli za Serikali yao? Ni wananchi wangapi wanafahamu kwamba Serikali inawajibika kwao?

Kuna mabadiliko katika taratibu za kusimamia na kuendesha shughuli za Serikali za Mitaa? Ubora wa Serikali za mitaa, demokrasia, upelekaji madaraka kwa wananchi ukoje?

Haya hatuyasikii yakijadiliwa na kufafanuliwa na vyama vya siasa. Je, viongozi wetu wanataka kurudia makosa aliyoyafanya Baba wa Taifa? Au wana tamaa ya kutaka kutwaa mamlaka ya dola, bila kuwa na dira ya wapi tunataka kwenda?

Mwalimu alituachia wasia wa Umoja wa Afrika. Ni kiasi gani Tanzania tunaufanyika kazi wasia huu. Tumekuwa vinara wa kuogopa hata ushirikiano wa Afrika Mashariki. Hoja zetu zinalenga kuonyesha kwamba sisi tunaishi kwenye kisiwa; tunajitahidi tusimezwe na Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini. Tunafikiri tukifungua milango yetu, kazi zote zitakwenda kwa wageni.

Muungano wetu si salama sana na hata wanasiasa wanakiri kuwa zipo kero za muungano zinazopaswa kushughulikiwa haraka. Hata hivyo ushiriki wa wananchi katika kujadili namna bora ya kudumisha muungano wetu ni wa kiwango cha chini.

Mjadala wa kuimarisha muungano umehodhiwa na wanasiasa katika ngazi ya kitaifa. Kama kweli tunataka mabadiliko, tuna mkakati gani wa kuhakikisha kuwa Muungano wetu unaimarika zaidi na mjadala wa kuuimarisha unapanuliwa ili wananchi wengi waweze kuchangia mawazo yao?

Hata Hivyo, tunataka tusitake, mabadiliko ni lazima na muda si rafiki yetu tena.

Columnist: mwananchi.co.tz