Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tusimkaribishe mtu nyumbani mlango ukiwa umefungwa

15773 Salim+said+salim TanzaniaWeb

Thu, 6 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Siku hizi haipiti muda mrefu utasikia imefanyika mikutano au makongamano hapa nyumbani au nje ya nchi ya kuwakumbusha Watanzania wanaoishi ughaibuni ‘kwamba “mtu kwao”.

Hapo tena hubwagwa taarifa za kuandaliwa mazingira mazuri kwa hao wanaoishi nje ya nchi kusaidia maendeleo ya nyumbani na kuwataka wawekeze vitega uchumi.

Mkutano wa namna hiyo ulifanyika Dar es Salaam hivi karibuni, miezi mitatu tu tokea Zanzibar kuzindua rasmi sera yake ya Diaspora inayotarajiwa kuwavutia watu wa Visiwani wanaoishi ughaibuni kushiriki na kutoa mchango wao kwa maendeleo ya Zanzibar.

Lengo la mpango huo linaenda sambamba na kama zinavyofanya nchi nyingi siku hiki na hatimaye kufaidika na mchango wa watu wake wanaoishi nje kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo za kisiasa na maisha.

Mara nyingi nimeelezea kuwa na sera na sheria nzuri sio hoja. Lilio muhimu ni sera iwe na mvuto na sheria iwe nzuri na zifuatiliwe na utekelezaji mzuri, isiwe sawa na kumwambia mtu ‘Karibu’ huku mlango umetiwa komeo au nafasi iliyowachwa wazi ni nyembamba na ambayo aliyenona kidogo tu hawezi kupenya kuingia ndani.

Ni vizuri tukahakikisha sera na sheria zetu zinakwenda sambamba na mahitaji ya ulimwengu wa leo na kuonyesha kweli waliokuwa ughaibuni sio tu wanakaribishwa, bali pia wanathaminiwa.

Tusiukatae ukweli kuwa Zanzibar, kama zilivyo nchi nyingi za Bara la Afrika na Asia, imeathirika sana kwa wataalamu wake wengi kuhama na kwenda kutumikia nchi za Arabuni, Ulaya, Asia, Canada na hata Australia, ukiachilia mamia waliopo nchi za jirani. Baadhi yao waliondoka wakiwa na hasira na hata kusema wasingefikiria kurudi kutokana na mambo yaliyowakuta.

Baadhi ya watu hawa wameneemeka na kutambulika katika hizo nchi walizopo na wengi kupewa uraia na nyadhifa za juu za uongozi kama mawaziri na mabalozi wa hizo nchi walikokimbilia wao au wazee wao.

Mtu kwao

Lakini kweli ‘mtu kwao’. Wengi wa watu hawa waliohama Zanzibar, baadhi yao kwa masikitiko ya kuona walifukuzwa kama mbwa, bado wanavipenda visiwa hivi na wapo walioonyesha hamu ya kurudi au kuwekeza kwao.

Unapoiangalia sera ya watu wanaoishi ughaibuni ni nzuri, lakini ukiyasikia hapa na pale yanayowakuta hao wanaotoka ughaibuni kuja kujipatia hati za usafiri na namna wanavyozungushwa na masuala wanayoulizwa utabaki unajiuliza: Je, hizo ndio njia za kuwaambia mtu Karibu nyumbani?

Kwa Afrika mchango wa watu waliopo ughaibuni unaoonekana kwa urahisi ni wa wacheza kandanda wa kimataifa wa kulipwa waliotapakaa katika nchi za Ulaya, wakiwemo wale waliopewa uraia na wengine kuwa na uraia pacha.

Vigezo vinavyopewa umuhimu ni ya kuwaonyesha uhakika watu hao kuwa si tu wanajulikana kuwepo kwao na kuthaminiwa ni vingi.

Miongoni mwao ni kutopata shida wanapochukua hati mpya za usafiri na kupewa haki zinazostahiki na fursa kama raia wengine wa nchi.

Ugumu wa vigezo

Tujiulize, je, sisi Tanzania tupo hivyo na zaidi nauliza hali ya Zanzibar kwa sasa ipo vipi?

Kwanza tuliangalie hili suala la uraia pacha liliopigiwa debe miaka michache iliyopita na kupotea angani kama moshi. Kama nchi nyingi hazioni shida hiyo na hata baadhi ya nchi duniani kuwa na marais wenye uraia pacha, kipi kinachotupa taabu Tanzania kwenda na hali ya ulimwengu wa leo?

Afrika Kusini, mara baada ya ukombozi uliouweka kando utawala wa kibaguzi wa makaburi ilitoa haki kwa watu wake kupiga kura wakiwa hukohuko ughaibuni. Hivi sasa nchi nyingi za Afrika zikiwemo za majirani zetu zinafanya hivyo.

Lakini, kwa Zanzibar tunaona inakuwa mbinde kuipata haki ya kupiga kura kwa maelfu ya watu ambao wao na mababu zao wamezaliwa Zanzibar.

Sasa unapomwambia waliopo ughaibuni ‘Mtu kwa’ kidogo ipo taabu kuamini kwamba atathaminiwa.

Unapozungumzia masuala ya uraia pacha au wa Watanzania waliopo nje kupewa haki ya kupiga kura unaonekana kama unazungumzia jambo ambalo haliingii akilini.

Kama kweli serikali zetu, za Muungano na Zanzibar zinataka ziaminiwe na Watanzania wanaoishi ughaibuni na waone zinawathamini, basi hayo mazingira mazuri tunayosema yanatayarisha ya kuwakaribisha nyumbani yajumuishe haki ya kupiga kura kama inavyofanywa na nchi nyengine duniani.

Ni kweli inakuwa vigumu kwa watu hawa kushiriki chaguzi za wabunge, wawakilishi au madiwani, lakini hapana sababu ya kutoweza kushiriki katika uchaguzi wa Rais.

Kwa Zanzibar panaweza kusikika kisingizio cha sheria ya ukazi inayotaka mtu awe amekaa eneo moja kwa kipindi kirefu ndiyo aweze kuandikishwa kuwa mpiga kura.

Sasa vipi utamwambia mtu aliyepo ughaibuni ‘mtu kwao’ na atathaminiwa wakati huu haki ya kushiriki hata katika uchaguzi wa Rais hakauna?

Hicho ndicho kile nilichoeleza cha kuwa sawa na kumwambia mtu karibu nyumbani huku mlango umetia komeo.

Mtu anaponyimwa haki ya kupiga kura, iwe yupo nyumbani au nje hujiona sawasawa na mkimbizi. Tubadilike na kwenda na wakati, vinginevyo wakati utatubakisha nyuma na kupelekea ndugu zetu waliopo ughaibuni kujiona wanatengwa kushiriki katika kuijenga nchi yao.

Columnist: mwananchi.co.tz