Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tusiishie kukusanya takwimu tu, matumizi yanahitajika pia

9794 Joseph+alphonce TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serikali inafanya kazi kubwa katika kubuni, kuendeleza na kusimamia miundombinu ya ukusanyaji wa takwimu nchini.

Upatikanaji wa takwimu kwa kiasi kikubwa si changamoto tena. Idara za Tehama katika taasisi nyingi zimeimarisha mifumo ya ukusanyaji wa takwimu kuanzia ngazi ya chini kabisa.

Umuhimu wa takwimu sio ajenda tena, wengi wanatambua umuhimu wa takwimu katika kupanga mipango ya maendeleo na mgawanyo wa rasilimali.

Swali, je ni taasisi ngapi zinatumia takwimu kama nyenzo ya kufanyia uamuzi?

Taasisi mbalimbali za Serikali na sekta binafsi zinatumia kiasi kikubwa cha fedha kukusanya takwimu kila mwaka.

Hii inahusisha takwimu zinazokusanywa wakati wa sensa na tafiti mbalimbali.

Mbali na kutumia kiasi kikubwa cha fedha kuwekeza kwenye miundombinu ya ukusanyaji wa takwimu ikiwemo kuandaa madodoso, mifumo ya Tehama, vyombo vya usafiri, posho, shajala na gharama nyingine, matumizi ya takwimu bado ni changamoto katika taasisi mbalimbali.

Mwaka 2015 Marekani inatajwa kutumia takwimu za ofisi ya sensa ya nchi hiyo kufanya uamuzi wa kutumia kiasi cha dola 675 bilioni katika kutekeleza programu 132, mwaka 2009 lilitumia dola 400 bilioni.

Dunia sasa haishii tu kwenye kukusanya takwimu, bali inawekeza zaidi kwenye matumizi ya takwimu.

Zipo taasisi nyingi ambazo zina idadi kubwa ya takwimu lakini hazitumiki kama nyenzo ya kufanya uamuzi sahihi.

Sheria ya takwimu ya mwaka 2015 kifungu cha 6(b) kinaeleza moja ya majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ni kuishauri Serikali na jamii kwa ujumla katika masuala yote yahusuyo takwimu rasmi.

Serikali na jamii kwa ujumla haipaswi kufanya uamuzi wa kutekeleza mradi au programu bila kuwa na takwimu sahihi kutoka kwenye mamlaka iliyopewa jukumu hilo kisheria.

Matumizi ya takwimu ni muhimu sana katika kupanga, kutoa au kutotoa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi.

Serikali inapotaka kutoa fedha kwa ajili ya kutoa huduma ya kijamii au uchumi katika eneo fulani ni vema takwimu zikatumika kuwa nyenzo ya kufikia uamuzi.

Endapo utafikiwa uamuzi wa kutoa fedha, utoaji wa fedha kwa taasisi unapaswa kufikiwa kwa kutumia takwimu pia.

Takwimu zitaonyesha uadilifu na uamini wa taasisi husika.

Matumizi ya takwimu pia yanasaidia katika kufanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi au programu mbalimbali za Serikali.

Serikali ina mifumo mingi ya kukusanya takwimu, kwa muktadha huu nitaitaja michache.

Mfumo wa kukusanya takwimu za elimu msingi (BEMIS), mfumo wa kukusanya mapato ya ndani ya Halmashauri (LGRCIS), mfumo wa kusimamia hospitali za Serikali (GoT-HoMIS).

Aidha, ina mfumo wa kusimamia rasilimali watu Serikalini (HCMIS-Lawson), mfumo wa taarifa za shule (SIS), mfumo wa fedha na ripoti kwa vituo vya kutolea huduma (FFARS), na mfumo wa kusimamia sekta ya maji (WSMIS).

Mifumo niliyoitaja na mingine mingi ambayo sijaitaja inahusika na kukusanya au kusimamia takwimu. Swali, je taasisi husika zinatumia takwimu zinazokusanya au kusimamia katika kufanya maamuzi?

Ipo mifumo inayokusanya takwimu kuanzia ngazi ya kituo; elimu na afya.

Mifumo hiyo inapaswa imuwezeshe mkuu wa taasisi kutumia takwimu anazokusanya katika kupanga mipango ya maendeleo na mgawanyo wa rasilimali katika taasisi yake.

Hivyo hivyo kwa ngazi ya Halmashauri na mikoa.

Moja ya changamoto inayodhoofisha upatikanaji wa takwimu sahihi ni kwa mkusanyaji au mtoa takwimu kutokuwa na uwezo wa kutumia takwimu anazokusanya katika kufanya maamuzi.

Wataalamu wanasema; umuhimu wa takwimu unaonekana pale takwimu zinapotumika, sio kukusanywa.

Afrika ya kusini kwa kuona umuhimu wa kukusanya na kutumia takwimu, sheria ya takwimu ya mwaka 1999 iliekeza sensa ya watu na makazi ifanyike kila baada ya miaka 5 kuanzia mwaka 2001.

Haituwa na tija sana na wala haitaleta maana endapo Serikali itaendelea kuwekeza rasilimali ikiwemo fedha na watu katika kukusanya tu takwimu bila kuhakikisha zinatumika katika ngazi mbalimbali kwa ajili ya kufanya maamuzi sahihi.

Matumizi ya takwimu ni nyenzo ya kutuonesha endapo tutafikia uchumi wa kati kabla au ifikapo 2025 na pia kupima mwenendo wa viashiria vingine vya kiuchumi na kijamii.

Mwandishi ni Mtakwimu – ofisi ya Rais - Tamisemi.

Columnist: mwananchi.co.tz