Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tunajifanya hatuoni watoto wa kiume wanavyoharibikiwa

11475 Watot+pic TanzaniaWeb

Mon, 16 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanzo ilikuwa kwamba ukitaka kupeleka taarifa kwa mjomba wako wa Matyazo Kigoma kwamba mkeo kajifungua mtoto wa kike, ilikuwa unatafuta basi lililoleta migebuka Dar es Salaam. Unampa dereva barua yako aipeleke wakati anarudi na unamlipa vipesa kidogo.

Ikaendaenda Wazungu wakaleta simu za mezani, ikawa sasa nafuu kwa watu wanaoweza kumudu. Wakawa wanazungumza na wakwe zao wa Bitaraguru, Musoma wakiwa Mtwara bila shida kama wameketi sebule moja hivi.

Tena kwa mara nyingine Wazungu wakalala - wakaamka, wakaja na uvumbuzi bab’kubwa zaidi, wakavumbua kadubwana ambako kanafanya kazi kama simu ya mezani, lakini haka wakakawekea uwezo wa kutembea nako kokote kakaitwa simu ya mkononi.

Mvumbuzi ni nani hata aishie hapo? Akasema hii haitoshi, akaleta simu zenye akili zaidi, zenye uwezo wa kufanya mambo mengi zaidi ya mawasiliano hiyo ilikuwa ni miaka ya 2000 na wakaziita smartphone.

Sasa, kwa kasi ya mabadiliko namna hiyo, kama kuna mtu maisha yake yaliishia mwaka 2005, bila shaka huko alipo anaamini kwamba siku akirudi duniani atakuta teknojia za ajabu zaidi.

Ubaya ni kwamba kama tungemrudisha katikati ya wiki hii. Angekutana na habari ya kwamba siku hizi wanafunzi wa madada poa huko Katavi ni wanafunzi wa sekondari, maendeleo ya kushangaza.

Wakati upande mwengine tunapambana kuhakikisha madada poa hawamalizi nguvu ya kazi ya leo, wao wanaboresha njia zao za kuitetekeza dunia ya kesho leo hii.

Ni moja ya habari za kushtua hasa ukizingatia wanafunzi wa sekondari siku hizi ni watoto wadogo tu. Miaka 14 hadi 17 ni umri mdogo sana wa mwanaume kuwa na ujasiri wa kuvuka mitaa yote, na kuingia kwenye danguro kwa ajili ya kupata ngono ya kununua.

Ukiwa na mtoto mwenye ujasiri wa kiasi hicho unaweza hata kumuachia familia yenye wategemezi sita na akawa na ujasiri wa kuilisha, ni ujasiri wa kiasi kikubwa.

Ila hii ni matokeo ya kuona watoto wa kike pekee ndiyo wanaoharibikiwa. Kila kampeni redioni inazungumzia mimba za utotoni, kila televisheni inaonesha kuhusu mafataki wa kiume na kila gazeti linaandika kuhusu namna ya kuwapa elimu watoto wa kike waelewe kuhusu afya ya uzazi ambayo inagusua masuala ya zinaa moja kwa moja.

Watoto wa kiume wanaharibika pia, tena kila siku idadi yao inaongezeaka kwa sababu hakuna anayewaangalia kwa jicho la kwamba pia wanahitaji msaada. Tena inawezekana, maharibiko yao ni makuu kuliko ya watoto wa kike, hapa hatuna maana

kwamba ni bora wao waharibike. Tunachosema ni kwamba wote wanahitaji jicho moja. Wote wanaharibikiwa.

Columnist: mwananchi.co.tz