Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tuna digrii nyingi zisizo na kazi

60945 DIGRII+PIC

Mon, 3 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ukipita mtaani, vijijini na mijini kilio kikubwa cha wananchi, hasa vijana, ni ajira. Ajira! Ajira! Ajira! Ukifanya uchunguzi mkubwa zaidi unagundua kuwa wanaolia ajira ni vijana waliohitimu vyuo vikuu. Japokuwa wale ambao wana elimu za kawaida za vyuo vya kati na wao wanalia kilio hichohicho.

Tatizo la ajira ni la kidunia, si tatizo lililoanza jana, ni tatizo la muda mrefu na kila zama linazidi kukua hasa katika nchi za Afrika.

Mtazamo wa Obasanjo

Katika kitabu cha “Making Africa Work” (kuifanya Afrika ijitambue), tafsiri ni yangu, Olusegun Obasanjo na waandishi wenzake wameeleza hatari ambazo zinaikabili Afrika ikiwa nchi mojamoja haitawekeza juhudi za kupambana na ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.

Watunzi wa kitabu hicho wameonesha kuwa Afrika ya siku za mbele itajaa vurugu na kutotawalika kwa sababu kutakuwa na mamilioni ya vijana wasio na ajira lakini wakiwa na simu mikononi mwao.

Waandishi hao wanasisitiza kuwa simu za mkononi ni silaha hatari kuliko kitu kingine kilichowahi kutokea duniani, kwani zinawaunganisha binadamu kuamua hatima yao ikiwa mifumo yao haifanyi kazi. Usishtuke!

Pia Soma

Kitabu hicho kimesisitiza kuwa, kwa kadri ambavyo viongozi wa Afrika wanavyozidi kuchelewa kuchukua hatua, ndivyo ambavyo tatizo la ajira linazidi kuwa kubwa, ukizingatia hoja nyingine kubwa ya kwamba Afrika ndiyo eneo la pekee duniani ambalo lina ongezeko kubwa la watu.

Tafiti kuhusu ajira

Wataalamu wengi wamefanya tafiti mbalimbali kuhusu ukosefu wa ajira, wengi wao wakisisitiza juu ya nchi kuwekeza kwenye mifumo ya mitaji na ujasiriamali kwa vijana. Kwa bahati mbaya tafiti hizi hazijengi misingi ya mwisho na hazisemi hali halisi ambayo inayakabili mataifa ya Afrika katika eneo la ajira.

Tafiti nyingi kuhusu ajira zimekaa kimkakati, kipropaganda na hazitaki kutatua tatizo la msingi linalotokana na uwezo wa mwanadamu kupambana na mazingira aliyopo na kutumia vipaji alivyopewa. Vipaji hujengwa kwa kuzaliwa au kujifunza katika hatua fulani ya maisha na huendelezwa kwa njia za kufanya jambo lilelile ambalo mhusika alifundishwa au analipenda au anajikuta analifanya kwa sababu limo rohoni mwake na akilini mwake kila mara.

Tafiti nyingi kuhusu ajira hazijafanya kazi kubwa ya kuoanisha utashi na uwezo wa mwanadamu dhidi ya mazingira aliyomo wala kuhuisha uwezo huo wa mwanadamu katika kutawala mazingira hayo.

Uwekezaji katika ujuzi

Nchi nyingi za Afrika zinaweza kutatua tatizo la ajira kwa kuwekeza kwenye ujuzi na kujenga wataalamu wenye kiwango cha kati (mafundi mchundo) kuliko kujenga watu wenye digrii nyingi zisizo na kazi.

Kwa Tanzania mathalani, uamuzi wa kuwekeza kwenye ujenzi wa shule katika kila kata ulifanywa kwa mafanikio makubwa, lakini uamuzi ule ulikuwa na maana ya kujenga taifa lenye watu walioelimika na kustaarabika kuliko kujenga taifa lenye watu wenye ajira.

Hoja ya ujenzi wa shule za kata haikwepeki na ilifanywa kwa manufaa na faida kubwa kwa taifa letu, lakini hoja ya ukosefu wa ajira kwenye taifa letu kama yalivyo mataifa mengine ya Afrika inataka hatua za dharura na za haraka kama walivyosema kina Obasanjo kwenye kitabu chao.

Serikali za Afrika na serikali ya Tanzania, hazina muda wa kusubiri, muda haupo, muda wa utatuzi wa tatizo la ajira ni sasa, siyo kesho. Utatuzi wa ajira unahitaji uwekezaji mkubwa kwenye ujuzi wa vijana na kutumia vipaji vya vijana hao kama nyenzo ya kuwafanya wajiajiri. Kwa wale wasio na vipaji ni lazima wafundishwe ujuzi ambao unaweza kutumika kutoa huduma au bidhaa kwa taifa.

Vyuo vya ufundi

Kama tuliweza kujenga shule za sekondari katika kila kata, hatuwezi kushindwa kujenga vyuo vya ufundi kila tarafa.

Tarafa za Tanzania ni chache mno, unakuta wilaya moja ina kata 25 lakini ziko kwenye tarafa nne, kama tuliweza kujenga shule 25 za kata katika wilaya moja, hatushindwi kujenga vyuo vinne vya ufundi katika wilaya hiyo.

Vyuo hivi vya ufundi vitakuwa kimbilio la vijana wengi wanaohitimu darasa la saba, elimu ya sekondari na vyuo vikuu. Utashangaa kuwa wanafunzi wengi waliohitimu masomo yao vyuo vikuu, badala ya kukaa mtaani miaka mitano wakitafuta ajira, watakimbilia kwenye vyuo hivi kujifunza kutengeneza kompyuta, majokofu, ujenzi, utengenezaji wa magari, ushonaji na aina nyingine za ujuzi.

Taifa lolote ambalo halihitaji matatizo ya vijana mbele ya safari, halitakwepa kuwapa ujuzi. Elimu ya sekondari kwa nchi kama Tanzania ifanywe ya msingi na baada ya hapo tupate wataalamu wa kati wenye ujuzi kuliko kuzalisha wengi wenye digrii na ambao hawajui watakwenda wapi baadaye.

Columnist: mwananchi.co.tz