Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tumsaidie Rais Magufuli kueneza ukweli kuhusu Dreamliner, Air Bus

33612 Edo+Kumwembe Tanzania Web Photo

Thu, 27 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unapokuja mjadala wa umuhimu wa ndege ambazo Namba Moja na Serikali yake wamenunua kwa sasa nadhani hatusaidii kueneza ukweli sahihi. Mwenyewe amewahi kugusia lakini hakuzama kiundani sana.

Kuna wanaoamini kwamba ni hasara. Ni kwa mlengo wa nauli za abiria kuweza kurudisha fedha za ununuzi wake na gharama za uendeshaji.

Upande mwingine muhimu ambao nadhani hatumsaidii sana Namba Moja na ambao nadhani kwa kiasi fulani una ukweli mkubwa ni ule wa mtazamo kuwa ndege hizo zinaweza kuleta watalii wengi moja kwa moja kutoka pande mbalimbali za dunia. Fedha ambazo watalii watazitumia na kuacha nchini zinaweza kuwa nyingi kuliko nauli wanazolipa.

Pia, ndege hizi zinaweza kuongeza mwingiliano mkubwa wa wafanyabiashara na watalii ambao utaongeza mzunguko wa fedha. Ukweli huu ulipaswa kuimbwa kuliko ule wa kwamba nauli za abiria zitarudisha fedha hizi kwa haraka.

Kuna mashirika mengi ya ndege ambayo yanapewa ruzuku na serikali zao kwa sababu yanachangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa kupitia ongezeko la watalii na wafanyabiashara ndani ya nchi husika. Huu ndio ukweli ambao unapaswa kuimbwa zaidi.

Jirani yetu Paul Kagame aliwekeza nguvu zake katika hili. Kwa sasa anatangaza zaidi watalii kutua Rwanda kwa sababu inamuongezea pato la kigeni. Ameilipa klabu ya Arsenal kuitangaza nchi yake ya Rwanda na sasa begani mwa jezi ya Arsenal kuna maandishi yaliyoandikwa ‘Visit Rwanda’.

Hakuna ubaya kwa ndege hizi kununuliwa kama tukijaribu kuandaa mazingira mazuri kwa watalii na wafanyabiara ili kuamsha baadhi ya majiji katika shughuli za kiuchumi. Tatizo litakuja pale ambapo tutaendelea kufufua shirika huku tukishindwa kuandaa mazingira.

Kwa mfano, watalii na wafanyabiashara hawawezi kurudi tena kama watajikuta wameingia katika nchi yenye urasimu. Ni tatizo letu la msingi. Hivi majuzi tu Namba Moja aliliongelea sana suala hilo. Tatizo letu ni lile lile.

Wasaidizi wengi wa Namba Moja wanabeba kila kitu kisiasa zaidi na majigambo juu baada ya kueneza ukweli kuhusu ununuzi wa ndege hizi. Labda wangeweka wazi namna ambavyo mashirika mengi ya ndege hayaendeshwi kifaida kwa mtazamo wa nauli za abiria na badala yake wangebeba mifano ya takwimu za namna ambavyo ndege zinaweza kupandisha idadi ya wataalamu na kiasi fulani cha Dola. Pengine wengi wangemuelewa Namba Moja.



Columnist: mwananchi.co.tz