Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tukubali upinzani ni jicho la pili la Serikali

12095 Daniel MjemaTanzaniaWeb

Wed, 15 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika kipindi cha mwaka mmoja sasa, kumekuwapo wimbi la wabunge na madiwani wa vyama vya upinzani kuhamia CCM na hali hii imevunja rekodi tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi 1992.

Si hao tu, wapo viongozi na wanachama wa vyama hivyo vya upinzani, nao wameamua kuachana na vyama vyao na kujiunga na CCM, na kuibua maswali mengi yasiyo na majibu.

Swali la msingi sana la kujiuliza ni je, wanaotoka wanatoka kwa utashi wao binafsi, kushawishiwa kwa namna yoyote ile iwe kwa rushwa au ahadi za madaraka au wanatumia haki yao ya kikatiba?

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 na sheria ya Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa, inataka yeyote anayegombea iwe ubunge au udiwani, apendekezwe na chama cha siasa.

Ibara ya 3(1) ya Katiba hiyo inasema nchi yetu ni ya kidemokrasia yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, lakini inatumika nguvu kubwa kudhoofisha vyama vya upinzani.

Ni kweli pia kuwa ibara ya 71(1) ya Katiba yetu mbunge atakoma kuwa mbunge ikiwa ataacha kuwa mwanachama wa chama alichokuwamo wakati anachaguliwa au kuteuliwa kuwa mbunge.

Nataka nitangulie kusema kuwa kwa ustawi wa demokrasia na uendeshaji bora wa nchi yetu, tunahitaji vyama vya upinzani imara ili viweze kuwa jicho na kioo kwa Serikali iliyoko madarakani.

Tukikubali kuwa na vyama vya upinzani dhaifu, tutabaki kusifia tu hata kama Serikali inafanya ndivyo sivyo. Wasomi, wanasayansi na wanasiasa wote tutajikuta tunasifia kama ile hadithi ya mfalme mmoja.

Hadithi ya mfalme huyo inatufundisha namna alivyoshonewa mavazi ambayo yalimuonyesha utupu, lakini kila mtu aliogopa kumweleza hadi mtoto mdogo alipopaza sauti kuwa yuko uchi.

Novemba 2017 niliwahi kufanya mahojiano maalumu na Katibu wa zamani wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye ambaye alisema wazi kuwa vyama vya upinzani vikiwa dhaifu, CCM itaumia.

“Tukiuua upande mmoja tutajisahau kama ambavyo ninaamini uimara wa vyama vya upinzani ndio uimara wa CCM. Vyama vya upinzani vikiwa dhaifu, CCM itaumia,” alisisitiza Nape na kuongeza;- “CCM itaumia kwa sababu watu wote watang’ang’ania CCM na wataanza kupigana kwa sababu kutakuwa hakuna tishio. Kukiwa na vitisho mnakaa sawa.

Katika makosa makubwa iliyoyafanya Serikali, ni kuzuia mikutano ya hadhara. Kwa sababu hiyo haipati mawazo mbadala kwa sababu waliozunguka wanaieleza kile inachopenda kukisikia.

Kwa wanaolikumbuka sakata la kashfa ya Sh133 bilioni ya akaunti ya madeni ya nje (EPA), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), walioibua hili walikuwa wabunge wa upinzani wakiongozwa na Dk Willibrod Slaa.

Hata kashfa ya akaunti ya Escrow ya karibu Sh300 bilioni, walioibua na kuishikia kidedea walikuwa ni wabunge wa upinzani wakiongozwa na aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila.

Ndio maana nimetangulia kusema ikiwa hiki kinachoendelea sasa (hamahama), kina lengo la kuua upinzani na si kwa utashi binafsi wa madiwani na wabunge, hakika tutafanya kosa kubwa.

Lakini, nafarijika kuwa CCM na Serikali yake, inaweza kutafanikiwa kuua vyama vya siasa vya upinzani lakini si upinzani kama upinzani. Upinzani ulikuwepo tangu ukoloni, umeendelea kuwepo na utaendelea.

Hiki ni kipindi ambacho wasomi wetu wa sayansi ya siasa wanapaswa kufanya tafiti na kuja na majibu ya hili kinachotokea kwamba wanahama kwa utashi wao, ushawishi au wanatumia haki yao ya kikatiba.

Siamini, nasema siamini kama upinzani ni kupinga kila kitu kizuri kinachofanywa na Rais Magufuli, na siamini pia kuwa ili kumuunga mkono ni lazima wote tuhamie CCM. Hili siamini.

Ndio maana nimetangulia kusema, tutafanya kosa kubwa sana kama tutashangilia kifo cha vyama vya upinzani nchini, na kwa mtu muungwana, hawezi kushabikia njama za aina hii.

Columnist: mwananchi.co.tz