Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tukokotoe alichosema CAG kuhusu kiongozi imara na taasisi madhubuti

10067 Cag+pic TanzaniaWeb

Sat, 4 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Alipofanya mahojiano na televisheni ya mtandao wa Umoja wa Mataifa Kiswahili, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad alitoa mtazamo wake kuhusu kutekelezeka kwa malengo 17 ya milenia mwaka 2015-2030.

Assad kwa maoni yake alisema, malengo yanatekelezeka, ila akaweka wazi kwamba yapo mambo ana wasiwasi nayo. Kwa kina zaidi, aligusia lengo namba 16 kuhusu amani, mshikamano na taasisi madhubuti. Alisema eneo la taasisi imara ndilo hasa ana shaka nalo.

Alisema kuwa katika miaka iliyopita, Tanzania imekuwa na bahati ya kuwa na viongozi imara kuliko taasisi madhubuti. Alifafanua kwamba uwepo wa taasisi madhubuti ni muhimu, kwani hata pale kiongozi anapokuwa si mzuri, basi taasisi zinakuwepo kumdhubiti.

Assad alitolea mfano Marekani ya sasa kwamba Rais wao, Donald Trump anaweza kuwa si mzuri, lakini uwepo wa taasisi imara unafanya nchi iende vizuri. Alimaanisha kwamba nchi ikiwa na mfumo mzuri wa kitaasisi, hata inapopata kiongozi mbaya, mambo hayawezi kuharibika.

Upo mfano alioutoa Assad kuhusu uwekezaji ambao hufanywa na bilionea wa Marekani, Warren Buffett, kwamba kwa kauli yake mwenyewe, alisema huwekeza kwenye kampuni ambazo hata mtu mjinga anaweza kuziendesha. Hapo alimaanisha kuwa Buffett huwekeza kwenye kampuni madhubuti kitaasisi na siyo zenye viongozi imara.

Kwa kumtambulisha vizuri Buffett, ni mmiliki wa kampuni ya masuala ya bima inayoitwa Berkshire Hathaway. Hivi sasa ndiye tajiri anayeshika nafasi ya tatu kwa kumiliki fedha nyingi duniani, akizidiwa na Jeff Bezos wa Amazon na Bill Gates wa Microsoft.

Kumbe sasa, umuhimu wa taasisi imara siyo tu kwa mwongozo wa Serikali, bali ndivyo hata uwekezaji wa kifedha unataka vyo. Hivyo, kama Buffett alivyoelekeza kuwa kuwekeza hisa kwenye taasisi yenye kumtegemea mtu siyo dhamana bora, ndivyo Assad anavyotwambia kwamba dhamana ya nchi kwenye mabega ya mtu si njia sahihi.

Tuanze ukokotoaji

Awali lazima kukubaliana kwamba nchi inahitaji taasisi imara kuliko uimara wa kiongozi. Haimaanishi kuwa viongozi madhubuti hawatakiwi, bali wawepo lakini mfumo wa kitaasisi sharti upewe kipaumbele. Viongozi ni binadamu, anaweza kuwa imara lakini akayumbisha nchi kwa masilahi yake au kwa kuyaamini makosa yake.

Sasa tunapaswa kujiuliza; je, upo wakati wowote katika historia Tanzania imewahi kuendeshwa kama nchi yenye misingi imara kitaasisi? Jawabu la swali hili tutalipata tu, lakini kabla ya jibu vema kutambua kwamba Tanzania tangu kuasisiwa kwake, kumekuwa na kuchomoza kwa watu imara kuliko taasisi imara. Hapa nakubaliana na Assad.

Wakati Tanzania Bara inapata uhuru wake mwanzoni mwa miaka ya 1960, kilikuwa ni kipindi ambacho dunia ilikuwa inashuhudia kupepesuka kwa nchi zenye uchumi wa kibepari na kushamiri kwa mataifa ya uchumi wa mrengo wa kushoto, kwa maana ya ukomunisti na ujamaa kwa jumla.

Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alipenda siasa za mrengo wa kushoto. Aliamini kwamba uchumi wa mrengo wa kulia ni unyonyaji. Mwalimu alivutiwa pia na itikadi ya Juche, iliyoanzishwa na Kiongozi Mkuu wa kwanza wa Korea Kaskazini, Kim II-Sung, yenye maana kujitegemea. Vilevile Juche hutafsiriwa kama ujamaa wenye kujitegemea.

Kwa kutafsiri, kuchambua na kuendeleza itikadi ya mrengo wa kushoto, Mwalimu Nyerere aliitambulisha falsafa ya ujamaa na kujitegemea kuwa ndiyo nadharia mama kwa nchi. Tanzania ikawa adui wa ubepari. Kukawepo viongozi wengine ambao hawakukubaliana na itikadi hiyo ya Mwalimu.

Mfano hai ni Waziri wa Elimu wa kwanza wa Tanganyika, Oscar Kambona ambaye pia alipata kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi. Ugomvi mkubwa kati ya Kambona na Mwalimu Nyerere ulisababishwa na uchaguzi wa falsafa ya nchi. Kambona aliamini katika ubepari na alikosoa ujamaa.

Mabadiliko ya kikatiba yalipofanyika yenye kupiga marufuku mfumo wa vyama vingi na kuchukua mkondo wa chama kimoja, Kambona alipingana na Nyerere. Kambona alitofautiana pia na Nyerere wakati wa utekelezaji wa operesheni ya vijiji vya ujamaa. Hali ikawa mbaya zaidi wakati wa kupitisha Azimio la Arusha.

Nyakati zote ambazo Nyerere kama Rais wa Tanganyika na baadaye Tanzania, vilevile mwenyekiti wa kilichokuwa chama tawala, Tanu, alipokuwa akivutana na Kambona ambaye pia alikuwa katibu mkuu wa Tanu, tafsiri iliyokuwepo ni mapambano kati ya Nyerere na Kambona.

Hali hiyo ilisababisha nchi ionekane kama ina mafahali wawili. Hata Nyerere alipomdhibiti Kambona ambaye aliamua kukimbilia uhamishoni nchini Uingereza, matokeo yaliyoonekana ni kushinda kwa Nyerere na si ujamaa wala Azimio la Arusha.

Matokeo yake ni kwamba ujamaa na utekelezwaji wake kupitia Azimio la Arusha ni mambo yaliyopewa afya na uimara wa mtu ambaye ni Mwalimu Nyerere. Ni kwa sababu hiyo, Mwalimu Nyerere alipoondoka madarakani, ujamaa ulianza kupewa mkono wa kwa heri na Azimio la Arusha lilipinduliwa na Azimio la Zanzibar mwaka 1991.

Kama Mwalimu Nyerere angefanikiwa kujenga taasisi imara yenye kuamini katika misingi ya ujamaa na kujitegemea kisha kulikumbatia Azimio la Arusha kama mwongozo wa ujenzi wa maisha ya Mtanzania, maana yake itikadi hiyo isingepotezwa kirahisi. Azimio la Arusha lisingepinduliwa ndani ya siku 181 tangu alipostaafu uenyekiti wa CCM Agosti 17, 1990.

Ni tatizo endelevu

Rais wa Pili wa Tanzania, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, alipoingia madarakani ni kama alianza upya, hakukuwa na mfumo wenye kumdhibiti kuendelea alipoishia Mwalimu Nyerere. Ni kwa sababu aliikuta nchi ambayo aliyempisha madarakani alikuwa ndiye kichwa cha Serikali.

Kama alivyomkuta Nyerere, Rais Mwinyi naye hakuunda mfumo wa kitaasisi. Ikatokea tu baadhi ya mawaziri kung’ara sana binafsi badala ya wizara zao. Mfano, Augustine Mrema alipokuwa Wizara ya Mambo ya Ndani, Profesa Kigoma Malima Fedha na baadaye Viwanda na Biashara, John Malecela Waziri Mkuu na wengine.

Sawa tu na Edward Sokoine na Salim Ahmed Salim walipopishana ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa Nyerere. Ni nyakati ambazo kiongozi alipoonesha tofauti aling’ara yeye binafsi, na baada ya kuondoka kwake, taifa lilianza kushuhudia tofauti kubwa kiutendaji.

Mwaka 1995, kuelekea mkutano mkuu wa CCM wa kupitisha jina la mgombea urais wa chama hicho, Mwalimu Nyerere alifanya mkutano na waandishi wa habari na kukataa kutaja jina la mwana CCM ambaye aliona anafaa, alisema watu wasijielekeze kwenye majina, bali watazame sifa ambazo mgombea anatakiwa awe nazo.

Kimsingi Mwalimu Nyerere alikuwa anakosoa jambo ambalo hakuliwekea misingi. Alipoingia madarakani alibeba ushawishi binafsi na alibaki hivyo akiwa madarakani, Mwinyi naye akatazamwa kama yeye, hivyo mwaka 1995, lilikuwa likitazamwa jina la nani angeshinda? Kukawa na mwendelezo huo mwaka 2005 na 2015, bila shaka utaendelea hata wakati wa kumrithi Rais John Magufuli.

Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa na mrithi wake, Jakaya Kikwete, walibeba thamani binafsi, kwamba wao ndiyo walikuwa kila kitu kwa Serikali walizoziongoza, waliamua taswira, muundo na mwendo wa utawala. Hata sasa, Rais Magufuli ndiye anaamua Serikali iende vipi. Hii Ni dhahiri kwamba hakuna taasisi zenye kusimamia misingi iliyotengenezwa.

Anaweza kutoka Rais ambaye alikuwa anaipeleke nchi Mashariki, anayemfuatia akawa anaielekeza Magharibi. Mwingine atashika uelekeo wa Kaskazini, anayemrithi atataka nchi iende Kusini. Mfumo wa kitaasisi huamua nchi iende wapi, hata wakifuata watawala wengine, wataendeleza kule ilipoelekezwa na si kuigeuza uelekeo. Kiongozi akitaka kufanya tofauti anadhibitiwa na taasisi.

Miaka nenda rudi, nchi imekuwa na mipango mingi. Fedha nyingi zinawekezwa kwenye utafiti, ripoti zikikamilika na kujengewa mpango wa utekelezaji, Serikali ikibadili utawala kila kitu kinafutwa na kuanza upya. Nchi haiwezi kuendelea ikiwa kila baada ya miaka 10 wizara zinaanza upya kutokana na maono ya Rais aliyeingia madarakani.

Tuangalie pa kushika

Urusi kwa sasa inaitwa Urusi ya Vladimir Putin. Marekani haiitwi ya Donald Trump, wala China siyo ya Xi Jinping. Urusi tangu anguko la Dola ya Nchi za Sovieti (USSR), ilijikuta inaanza upya kuanzia kwa Boris Yeltsin, aliyechukua mpini kwa kiongozi wa mwisho wa Sovieti, Mikhail Gorbachev. Yeltsin hakuweka misingi ya kitaasisi, hivyo Putin anajenga nchi atakavyo na si Warusi wapendavyo.

Hata kipindi cha miaka minne ambacho Dmitry Medvedev alishika mpini, hakukuwa na mfumo madhubuti wa kitaasisi na Putin aliporejea, amekuwa na mwendelezo wa kutoka pale alipoishia. Inajengwa Urusi ya maono ya mtu, hivyo akiondoka anaweza kutokea mwingine akawa na sura ya peke yake. Hapo nchi itazidi kuumia.

China inaonekana ni nchi yenye utawala wa kiimla, hata hivyo tofauti kubwa ni kwamba China siyo ya mtu, bali ya Chama cha Communist. Tangu mwaka 1949, Communist walipowashinda Kuomintang katika vita ya kiraia, walihakikisha wanajenga taasisi imara ya chama ili iweze kuiongoza nchi yao kwa masilahi ya wengi.

Kumekuwa na utaratibu mgumu wa kuchakata, kuwaandaa na kuwapitia vijana na watu ambao wanaweza kuongoza nchi kwa masilahi ya China kama ambavyo Communist wanataka. Hatokei tu mtu kuwa kiongozi mpaka awe amethibitishwa na mfumo wa chama. Vilevile Bunge la China na Kamati Kuu ya Communist, ni vyombo vikubwa vyenye uamuzi kuliko Rais na Waziri Mkuu (Premier).

Marekani Rais ana mamlaka makubwa lakini yameshikwa na mfumo wa kitaasisi. Anaweza kutaka jambo na likawa, ila sharti lipitie bungeni, wabunge wakubali au wakatae na wakikataa hana ujanja. Ni mambo mengi tu Trump anashindwa kuyafanya hivi sasa kwa sababu anajua Bunge kwa maana ya Congress au mabaraza yake mawili, Seneti na Wawakilishi, hawezi kupata kura.

Hivi ndivyo Assad anataka

Maendeleo ya nchi yanataka taasisi madhubuti kama Marekani, China (japo inaonekana ni demokrasia ya wachache), vilevile mataifa mengine mengi. Siyo kuwa na kiongozi imara kuliko taasisi mfano wa Urusi ya sasa. Hata Kenya, kwa Katiba ya sasa, inalifanya taifa hilo kuwa na mfumo wa kitaasisi kuliko nchi zote za Afrika Mashariki.

Columnist: mwananchi.co.tz