Dawa kubwa kuliko yote ya uovu dhidi ya utu wa mwanadamu ni kuukemea uovu huo. Rafiki na kaka yangu Charles Njagua ‘Jaguar’ ambaye ni mbunge wa jimbo la Starehe nchini Kenya amekutana na dawa ya uovu.
Kwa sababu namfahamu vizuri (japo anaweza kuwa hakumbuki) ilinipasa kumpelekea ujumbe mfupi kwenye simu yake haraka sana mara baada ya yeye mwenyewe kuweka video inayonajisi utu wa mwafrika kwenye akaunti yake ya mtandao wa Instagram.
Kwenye meseji yangu nilimweleza, “ndugu yangu salaam sana, habari ya Nairobi na pole na kazi, nimeona video yako kwenye ukurasa wako wa Instagram, nimekupigia mara kadhaa ili kujua kama akaunti yako imeingiliwa na matapeli wa mtandaoni, lakini nimeona video kama yako kwenye kurasa za vyombo vyote vya habari vya Kenya, ikiwa ni uthibitisho kuwa video hiyo ni halisi na yanayosemwa humo ni ya kwako”
“...Mara ya mwisho mimi na wewe tulionana Mombasa, ikiwa ni kwenye tamasha lililoandaliwa na wasanii mbalimbali na ulinieleza ulivyo na ndoto za kuwa mbunge wa Kenya ili usaidie kuondoa siasa za kitapeli na kuwasaidia Wakenya na wananchi wa Afrika Mashariki, lakini hiki nachokiona unafanya mara baada ya kupata ubunge sicho ambacho umekuwa ukiamini na kuhubiri, wewe ni muunganishaji wa watu na siyo mparaganyishaji, wewe ni wakala mzuri wa kuondoa utapeli kwenye siasa na siyo kuukuza, video yako hii itakuhukumu mbele ya Wakenya na Watanzania na wote kwa pamoja watakueleza kuwa maelezo yako hayawakilishi matakwa yao..”.
Pia Soma
- Wasira: TIB hawanidai, tulishalipa deni lao
- UCHAMBUZI: Jaguar anaonyesha jinsi zilivyo hulka za Waafrika kubaguana
- Jicho la wasomi na ushirika huru wenye demokrasia
Jaguar hakujibu ujumbe wangu, baadaye nikauandika kwenye akaunti yake ya Instagram, nikaongeza na ujumbe mwingine, jumbe zote baadaye niligundua zimefutwa, baadaye nilipokagua zaidi nikagundua hata ile video yake ya maneno ya ubaguzi imeondolewa mtandaoni.
Ni muhimu sana unapokuwa mwanasiasa mapambano yako yaishie kwenye kutafuta nafasi ya kisiasa na kuwatumikia wananchi wako.
Kwa uzoefu tu wa kawaida, ukifuatilia unagundua kuwa Wakenya wanaofanya kazi Tanzania (kinyemela na kwa njia rasmi) ni wengi mno kuliko Watanzania wanaofanya kazi Kenya.
Kauli ambazo tumekuwa tukizisikia kutoka kwa wanasiasa wa Tanzania ni kutaka Watanzania waamke, wapambane, wajenge uwezo na ubunifu wa kupambana na ndugu zao wa Kenya kiushindani kwenye masoko ya ajira, biashara na nyanja nyingine za maisha.
Hatukuwahi kusikia kauli za wanasiasa wa Tanzania wakihamasisha wananchi wa Tanzania wawapige na kuwafukuza Wakenya ndani ya saa 24 mahali popote. Kama kuna kauli zimewahi kutoka zitakuwa ni hizi za baadhi ya wanasiasa wa Tanzania ambao wametaka kumjibu Jaguar kwa lugha ile ile aliyotumia yeye, jambo ambalo pia halikubaliki.
Mathalani, siku hizi wazazi wengi wa Kitanzania wanawapeleka watoto wao kuanza masomo kwenye shule zinazofundisha kwa Kiingereza tangu darasa la awali ambazo ni maarufu kwa majina ya “International Schools”, wazazi wengi ni mashahidi kuwa sehemu kubwa ya walimu wa shule hizo ni ndugu zetu Wakenya na ziko sababu nyingi za msingi ambazo zinafanya Wakenya wanaajiriwa zaidi.
Hatujawahi kusikia viongozi wa Tanzania wamewapiga vita walimu wanaotoka Kenya, kwa sababu viongozi wa Tanzania wanaamini hiyo ni hali halisi ya mahitaji ya shule hizo ambayo itaondolewa miaka michache ijayo kwa sababu kizazi cha vijana waliosoma tangu shule za awali kwa Kiingereza nchini Tanzania kinapanuka na kukua sana, ndani ya miaka michache ijayo wamiliki wa shule hizi za Kiingereza watajichagulia maelfu ya walimu wa Tanzania kwani watakuwa hawana tatizo la misingi ya Kiingereza.
Majawabu ya matatizo huja bila nguvu
Majawabu ya ajira fulani kwenye nchi fulani kushikiliwa na watu fulani hutatuliwa kimkakati na bila nguvu, majawabu hayo hufanywa kwa viongozi wa nchi husika kuwezesha watu wao na kuwapa uwezo wa kushindana na wenzao waliotoka mataifa ya nje ambao nao ni binadamu kama wao. Kama Jaguar na wenzake wanaona Watanzania wanaofanya biashara ndogo ndogo kwenye baadhi ya masoko ya Kenya wanapata faida na fedha nyingi, suluhisho ni kwa viongozi hao kuwezesha pia Wakenya mbinu na uwezo wa kushindana kibiashara, siyo kuanza kuwapiga na kuwafukuza.
Na huu mchezo wa kufukuzana Afrika Mashariki ukianza, kwa vyovyote vile Wakenya wataathirika zaidi kuliko Watanzania wala Waganda. Kama kuna wananchi wanahangaika kwenye mataifa mengine ya nchi kutafuta vipato thabiti, basi Wakenya ni wahangaikaji kuliko Watanzania. Hatua yoyote ile ya kuanza kufukuzana kwenye mataifa yetu kwa vyovyote vile ikifanywa na kila nchi, Wakenya wataumizwa zaidi kuliko taifa lingine lolote la Afrika Mashariki.