Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tuache uzembe barabarani

45102 Barabarani+pic Tuache uzembe barabarani

Wed, 6 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Siku hizi tumekuwa tukipokea taarifa za kusikitisha na kutisha za ajali za barabarani Bara na Visiwani na watu wengi hubaki kusikitika badala ya kulitafakari suala hili kwa undani na kutafuta njia za angalau kuzipunguza.

Wapo watu ambao humalizia tafakuri zao za hizi ajali kwa kujifunika chandarua cha msemo maarufu wa Kiswahili wa …ajali haina kinga.

Kwa mtazamo wangu hii sio sahihi kwa sababu unapochunguza utaona uzembe umefanyika, dharau ya sheria za barabarani na watu kutojali

usalama wao ndio kunakochangia kuwepo hali hii mbaya.

Katika siku za nyuma palisikika malalamiko kwamba barabara zetu ni mbaya na ndio sababu za kutokea kwa ajali nyingi.

Lakini, wakati sasa hali ya barabara zetu ni bora zaidi utaona hayo maeneo yenye barabara safi ndio ajali zimeongezeka.

Kila wakati ambapo askari wa kikosi cha usalama barabarani wanapojaribu kuchukua hatua za kudhibiti uzembe ili kuwasaidia wanaohatarisha maisha yao na ya wenzao barabarani, jamii hukurupuka kuwalaumu hawa askari.

Sikatai kuwepo wachache wanaotumia vibaya mamlaka yao ya kisheria, lakini sio haki kukilaumu kikosi chote kwa makosa ya wachache.

Kwa mfano, Zanzibar utaona ni jambo la kawaida kuona kwa kila gari nne au tano zinazopita barabarani, hasa za mabasi na daladala, dereva wake anazungumza na simu huku amekamata usukani kwa mkono mmoja.

Wakati wa usiku ni kawaida kuona gari, pikipiki na baiskeli zinaendeshwa bila ya taa kama vile sheria zinaruhusu, lakini ikitokea ajali ni nadra kumuacha salama dereva wa chombo husika.

Tatizo la Zanzibar ni la watu kuoneana muhali hata kwa masuala ambayo mtu huwa amefanya jambo kwa makusudi ambalo linahatarisha usalama wa maisha yake na watu wengine.

Baadhi ya wenye pikipiki wamefanya huo mtindo unaoitwa ‘mshikaki’ wa watu watatu hadi wanne kupanda pikipiki moja kuwa ni wa kawaida.

Wapo watu utaona amepakia watoto watatu kwenye pikipiki bila ya kujali kwamba hiyo ni hatari na wanapoonywa au kushitakiwa, huuishia kutoa lawama kwa askari ikiwamo kuwatupia shutuma za rushwa.

Idadi pia ya watoto wanaoendesha vyombo vya moto, ikiwa pamoja na magari, siku hizi imeongeza Zanzibar na matokeo yake ni kwamba baada ya kila muda mfupi utasikia ajali iliyopoteza maisha ya vijana hao wadogo iliyosababishwa na mwendo wa kasi.

Nadhani wakati umefika kwa watu wa Visiwani kuitafakari kwa makini hali hii inayopoteza maisha ya watu wengi kutokana na uzembe, dharau na kutojali sheria.

Pamoja na kutolewa elimu mara kwa mara, upo umuhimu kwa kikosi cha usalama barabarani kuchukua hatua madhubuti kwa watu wanaotumia simu wakati wakiendesha vyombo, wanaokwenda mwendo wa kasi kupita kiasi na kutokuwa na taa nyakati za usiku.

Mtindo wa mabasi ya shamba na daladala kupakia abiria zaidi ya uwezo wa gari na wengine kuning’inia kwenye milango lazima ukomeshwe.

Ni muhimu watu wakatae kujazwa katika gari za abiria kama dagaa kwenye mkebe. Lakini, wanapokubali na gari inapokamatwa basi polisi wahakikishe na abiria wanaopatikana wamesimama ndani ya gari au wamekalishwa chini wanashitakiwa na kupewa adhabu.

Tuache kujilinda na kisingizio cha ajali haina kinga na badala yake tuchukue kinga za kutusaidia kujikinga na ajali na wale ambao hawataki kuchukua hizo kinga wachukuliwe hatua za kisheria.

Huu mchezo unaoendekezwa Zanzibar wa watu kuchezea maisha yao na ya wenzao barabarani, haupaswi kuvumiliwa hata kidogo.

Tukipe nafasi kikosi cha askari wa usalama barabarani kifanye kazi yake kwa mujibu wa sheria, kila mmoja ajitahidi kuchukua hatua za kuhakikisha usalama wake na wa wenzake.



Columnist: mwananchi.co.tz