Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tofauti kuu za kisaikolojia kati ya huku uzunguni na Africa

50925 Fredy Macha

Mon, 8 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanzo wa juma hili mtu anayesadikiwa kuwa mlemavu wa akili, aliibuka na kisu chake akavizia wapita njia. Katika siku tatu- aliwakata kata watu watano – wawili vibaya sana. Yalisibu kitongoji cha Enfield na Tottenham Kaskazini ya London.

Mtuhumiwa alikisiwa kuwa mweusi, mrefu, mwembamba.

Tatizo la kuharibikiwa kisaikolojia linazidi nchi hizi tajiri.

Kati ya tunayosikia kuhusu Ulaya, Marekani na Ughaibuni ni furaha ya maendeleo ya viwanda, mashine, fedha na uafadhali wa maisha.

Zamani sinema zilikuwa kioo kikuu cha Uzunguni. Tuliwaona weupe wakila raha, wakipigana mabusu, wakiendesha magari mazuri mazuri. Tuliwaona weupe wakija kwetu kutembelea mbuga za wanyama; wakikodi mahoteli makubwa makubwa ya fahari. Wale waliofanya kazi Afrika waliishi ( hata leo) mitaa bora na watumishi na hali za kutamanika.

Tulitamani ndiyo. Niliwahi kuandika kitabu - Twenzetu Ulaya -mwaka 1984. Na vijana wenzangu tuliotea maisha ya Uzunguni. Tulitaka kuwa mabaharia. Tulijificha katika meli kutoroka tabu na uchochole wa Afrika.

Hapo hapo Serikali na viongozi kama hayati Mwalimu Nyerere walituonya Ubepari ni Unyama. Ila utaouonaje uhayawani kama unakula kwa shida, unalala kwa karaha na kero za kile tulichokiita Bongo Jua Kali?

Leo si tu vya kusikia katika sinema. Tunavinusa. Kila nukta mitandao jamii inatuonjesha asali. Wanaadamu tumegeuka Ndombolo.

Utakaa hapo hapo: Dar Es Salaam, Chunya, Kilombero, Tanga au Moshi ukaiomba Google ikuonyeshe Ubalozi wetu London, mathalan. Kupitia simu yako utaiona taswira ya mtaa wa Bond Street na majengo mengine jirani... mbali ya Ubalozi. Uzunguni.

Mwanadamu amegawanyika sehemu nne. Mwili, hisia, akili na roho. Saikolojia ni mchanganyiko wa hisia, akili na roho.

Tofauti kuu ya kwetu na kwao (ughaibuni) kisaikolojia ni mahusiano na mawasiliano. Huku Uzunguni hali ya hewa huwa ya baridi asilimia 75 ya mwaka mzima. Hilo huwageuza watu kuwa wa-kimya sana. Pili, utamaduni wa kutoongea ongea huwafanya wanadamu kutowasiliana. Kila mtu anatafuta fedha alipie maisha aghali - nyumba za kupanga, magari, nk. Si wengi wanaomudu.

Halafu kipo kichuguu cha watu weusi, waliozaliwa huku. Bado wana makovu ya harakati na enzi za utumwa. Wapo walioamka na kuchukua nafasi za kielimu na kimaendeleo zinazopatikana Uzunguni. Wapo walioshindwa. Hubwia dawa za kulevya (kama bangi tuliyoitaja hapa karibuni inayopendwa sana na baadhi ya watu weusi) ; haya -huwaletea madhara kiakili. Kwa kuwa mawasiliano na mahusiano si sawawasawa na Afrika weusi huheuka.

Kuna utofauti wa kisaikolojia. Mzungu anaweza kumwona mbwa akafurahi sana. Kiasi fulani wanyama wamefidia mapenzi ya watu na watu. Kwa Mwafrika, mbwa huogofya. Mbwa ni mlinzi wa nyumba. Si ndugu au mpenzi. Hiki ndicho kinyume cha maisha yetu na tofauti hizi za kisaikolojia ni muhimu.

Afrika ni rahisi kuongea na mtu yeyote popote. Hakuna atakayekukatalia salamu. Lakini London ya leo unaweza kumsalimia mtu usiyemjua barabarani akakuchinja kisu. Huo ni ukweli. Sasa baada ya hizi simu za mkononi ndiyo kabisa watu hawazungumzi sawasawa, ana kwa ana. Bado Afrika imesheheni upendo na utajiri wa kimawasiliano. Ni hazina nzito sana. Tusiitupe.



Columnist: mwananchi.co.tz