Jakaya Kikwete akiwa madarakani, kukawa na wimbi la watu kuutaka urais. Ilikuwa kama jambo rahisi ambalo linaweza kufanywa na yeyote kama vile kuwania uenyekiti wa ‘vikoba’.
Pengine hayo yalitokana na urahisi aliopitia JK kupata urais na namna alivyoongoza kila mtu akadhani anaweza.
Ilikera sana mtu anakurupuka na kutangaza nia. Nchi iligeuka motomoto kuanzia Ilula, Itigi, Korogwe, Gairo, Bumbuli, Nzega, Kigoma na huko Rungwe kama si Hanang kabisa.
Mtiti wa watu kutaka urais 2015 kupitia CCM, ilibidi wengine tujiulize sababu zinazowashawishi kiasi kwamba kila mtu aone anaweza. Maana idadi ya watu kutaka kupigiwa mizinga 21 ilivunja rekodi. Mpaka wahonga vocha wakataka kuishi Magogoni.
Yaani kila mtu kuona inawezekana kupigwa picha na kutundikwa kwenye ofisi za serikali na watu binafsi. Utani wa karne. Ni kweli wale wote walikuwa na maono na utashi wa kubeba hilo jukumu zito kwa Taifa? Walibaki tu kina Wema Sepetu, Steve Nyerere na wenzao kutangaza nia.
Kichekesho ni kwamba wengine kwenye vinafasi vidogo walivyopewa wameshindwa kuonesha uwezo. Ukuu wa mikoa, uwaziri na ubunge. Hakuna la ajabu kiasi cha sisi tujutie wao kutopata urais. Wengi wametumbuliwa kama vijipu uchungu kwa makosa ya ajabu.
Pia Soma
- Lissu kurejea Tanzania Septemba 7, kushiriki uchaguzi Serikali za mitaa
- Uchaguzi Malawi ushindani mkali
- UVCCM kuwapambania walimu wanaojitolea kupata ajira, posho
Mzee wa Mtama hakukawia kujibu kauli ya Rostam. Bila shaka aliguswa kwenye mfupa. Ilitokea kwa Edo na JK 2010. Edo ‘akitaka’ kukatisha pozi la JK Magogoni. Ilikuwa ngumu sana kupindua meza ya Mzee wa Msoga. Akaishia kulinda mifugo yake Monduli mpaka 2015 alipoamua kumwaga mboga.
Kwa JK ilikuwa rahisi. CCM ya wakati ule ni kama bwawa la kambare kila mtu alikuwa na ndevu. Fujo za Nchimbi, Adam Kimbisa na Sophia Simba pale Dodoma akitangazwa mteule wa CCM, ni matokeo ya JK kuwaachia wachukulie poa. Lakini ‘CCM mpya’ iko tofauti sana. Inahitaji ujasiri wa kijasiri kuikabili.
Lakini watu aina ya Mzee Mtama usiwachukulie poa maana hadi wanatajwa huenda kuna jambo. Na binadamu aina ya Mzee wa Mtama huwezi kutabiri awazacho. Ni suala la muda maana ni vita ya nguvu ya dola na akili ya dola.