Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Thamani ya uhai inavyopungua kwa kasi Afrika Mashariki

17462 Uhai+poic TanzaniaWeb

Mon, 17 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Jumamosi iliyopita (Septemba 8), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) nchini Uganda, Muhammad Kirumira, alipigwa risasi akiwa kwenye gari lake, jirani na nyumbani kwake. Tukio hilo linatajwa kutokea saa 3 usiku. Kirumira alikuwa na mwanamke ambaye alitajwa ni mkewe, lakini baadaye polisi walisema si mke wake.

Mwanamke huyo pia alipigwa risasi. Wote wawili walipelekwa katika Hospitali ya Rubaga, iliyopo Kampala ambako taarifa ilitolewa baadaye kuwa wamefariki dunia. Kabla ya kifo chake, Kirumira alikuwa kwenye mgogoro na uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi Uganda, alioutuhumu kwa kukumbatia rushwa na ukiukaji wa haki za raia.

Januari mwaka huu, Kirumira alijiuzulu kazi ya polisi, kwa kile alichodai kuwa ni kutopendezwa na tuhuma zilizofunguliwa dhidi yake. Kirumira alifunguliwa mashtaka ya uhalifu, matumizi mabaya ya cheo, na akatakiwa kushushwa daraja, kutoka nyota tatu (ASP) hadi nyota mbili (Inspekta).

Mamlaka za jeshi Uganda zilimkatalia Kirumira kujiuzulu upolisi kwa maelezo kwamba haiwezekani kwa ofisa wa jeshi aliye kwenye mchakato wa kuonywa kwa utovu wa nidhamu kuacha kazi.

Kirumira alisema kuwa misimamo yake dhidi ya maofisa wa juu polisi wanaotumia vibaya madaraka yao kukandamiza watu na kuwalinda watawala ndiyo umemponza.

Alisema kuwa tuhuma alizofunguliwa na kutakiwa kushushwa cheo, anadaiwa kuzitenda alipokuwa na nyota moja (Inspekta Msaidizi wa Polisi). Alihoji; iweje mtu mwenye rekodi za uhalifu apandishwe cheo kwa kurushwa daraja, kutoka Inspekta Msaidizi hadi Mrakibu Msaidizi? Suala hilo lilifika mpaka mahakamani.

Zipo video zinamwonyesha Kirumira alipokuwa kwenye mvutano na polisi, akiwatetea waandishi wa habari waruhusiwe kuingia mahakamani ili waripoti mwendelezo wa kesi yake na Polisi wa Uganda. Sauti yake inasikika akitaka vyombo vya habari viachwe vifanye kazi, kwani hakuna siri ya kufichwa.

Kirumira alitokea kuwa mtu wa karibu na mbunge wa Kyadondo Mashariki, Robert Kyagulanyi ‘Bobi Wine’, na alishikamana naye nyakati ambazo mbunge huyo alikuwa kwenye mvutano mkubwa na dola.

Agosti 13, mwaka huu, alikuwa na Bobi Wine kwenye gari la mbunge huyo, na walipotoka, polisi walimfyatulia risasi dereva wa Bobi Wine, Kawuma Yasin na kumuua.

Yasin aliuawa akiwa Arua, Uganda, kulikokuwa kunafanyika uchaguzi mdogo wa ubunge. Bobi Wine alikuwa akimuunga mkono mgombea binafsi, Kassiano Wadri, hivyo aliweka kambi Arua ili kumfanyia kampeni. Kitendo cha Kirumira kuwa Arua na Bobi Wine, kilidhihirisha kuwa ofisa huyo alikuwa anaunga mkono harakati zake za kisiasa.

Ukifika hapo unahesabu vifo viwili, kwa maana ya Kirumira na Yasin. Ongeza kuwa Agosti 13 na 14, mwaka huu, yalitokea machafuko kadhaa na kusababisha watu wanane kuuawa, wakiwamo askari watatu.

Chanzo cha ghasia ni kampeni za uchaguzi Arua, polisi wakimtuhumu Bobi Wine na wabunge wengine wa upinzani kufanya fujo, hivyo kumuua Yasin, kisha mauaji kuendelea mitaani.

Bobi Wine aliwatuhumu polisi kwamba walimfyatulia risasi Yasin wakidhani ni yeye. Tafsiri ya maneno hayo ni kuwa anaamini polisi walikusudia kumuua yeye. Tuhuma hizo amezirejea Jumapili iliyopita akiwa Marekani, alipokuwa anaelezea masikitiko yake baada ya Kirumira ambaye alimtaja kuwa rafiki yake wa karibu, kuuawa.

Chanzo cha machafuko Arua

Agosti 13, mwaka huu, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, alikwenda Arua kumfanyia kampeni mgombea wa chama chake cha National Resistance Movement (NRM), Nusura Tiperu. Hata hivyo, Tiperu alishindwa na Wadri, aliyekuwa akipigiwa kampeni na Bobi Wine.

Museveni baada ya kumaliza mkutano, msafara wake ulipita sehemu yenye kundi kubwa la watu ambao inadaiwa walimzomea na kumrushia mawe. Pamoja na vitendo hivyo, watu hao walikuwa wakiimba nyimbo za kumtukuza Bobi Wine kuwa ndiye rais wao.

Hamaki ya polisi ilisababisha kifo cha Yasini, kisha Bobi Wine alikamatwa alipokuwa amejificha hotelini, akafunguliwa mashtaka ya uhaini na kumiliki silaha kisha akapelekwa mahakama ya kijeshi. Inadaiwa alipewa mateso makali ambayo yamemfanya mpaka sasa aendelee kutembea kwa msaada wa magongo.

Arua wamefanya uchaguzi mdogo Agosti 15, mwaka huu, baada ya aliyekuwa mbunge wa manispaa hiyo, Ibrahim Abiriga kuuawa kwa risasi jirani na nyumbani kwake eneo la Matugga Juni, mwaka huu.

Machi 17, mwaka huu, ulitimia mwaka mmoja tangu alipouawa kwa kupigwa risasi, aliyekuwa Inspekta Jenerali Msaidizi wa Polisi (AIGP) nchini Uganda, Andrew Kaweesi. Kwa namna ya pekee, Waganda waliamua kumkumbuka kwa kufanya marejeo ya picha za video, jinsi alivyokuwa akiwajibika kwa uadilifu na utu.

Moja ya video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikiandikwa: “Itachukua miaka Uganda kumpata mtu wa kuziba pengo la huyu mtu.” Ndani ya video hiyo Kaweesi anaonekana akihimiza polisi kutowadhuru watu katikati ya misheni za kipolisi.

Kaweesi aliuawa umbali kidogo kutoka nyumbani kwake, saa 4 asubuhi, akiwa kwenye gari pamoja na dereva na mlinzi. Pikipiki yenye dereva na abiria wawili wenye bunduki, ilitokea mbele ya gari, kisha watu hao wawili waliwashambulia Kaweesi, dereva na mlinzi wake. Mwili wa Kaweesi ulikutwa na risasi 27.

Dereva, Godfrey Wambewo alipigwa risasi 11 na mlinzi, Kenneth Erau alimiminiwa risasi 33.

Gari la Kaweesi ambalo lilikuwa mali ya Jeshi la Polisi Uganda, lilitobolewa na risasi 77. Tangu kutokea kwa tukio hilo, hakuna mtu yeyote aliyefikishwa mahakamani.

Kwa Waganda, Kirumira alikuwa sawa na Kaweesi. Kitendo cha kuingia kwenye migogoro na polisi kisha kuuawa, kimezua mjadala wenye maswali; ni kwa nini maofisa wa polisi wenye kusimama kutetea raia wanauawa? Kwa nini watu wanauawa kama viumbe visivyo na thamani?

Thamani ya uhai

Thamani ya uhai wa mtu huonekana jinsi usalama wake unavyolindwa. Inapotokea watu wanauawa kama viumbe visivyothaminika maana yake thamani ya uhai wa mtu inakuwa imepungua. Ukifuatilia kwa makini utaona mambo kama haya yanayotokea katika nchi nyingi za Afrika Mashariki. Hivyo, ni sahihi kusema katika nchi hizo kuna hali ambayo thamani ya uhai wa watu inapinguzwa.

Kwamba kuna mtu au watu wakikaa na kupanga akina nani waendelee kuishi na wengine wafe, wanatekeleza mpango wao na wahusika hawakamatwi. Usalama wa watu na maisha yao havipaswi kuchukuliwa kwa urahisi.

Hapo tumezungumza Uganda, upande wa Tanzania, Januari 16, mwaka huu, Dar es Salaam, aliuawa kwa kupigwa risasi mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilina akiwa kwenye daladala. Polisi walikuwa wakiwatawanya waandamanaji wa Chadema, waliokuwa wanakwenda ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi Kinondoni, kushinikiza wapewe hati za viapo na barua za utambulisho kwa ajili ya mawakala wao.

Chadema walifanya maandamano hayo kwa sababu ya kile walichodai kuwa walikuwa wanahujumiwa kwa mawakala wao kucheleweshewa viapo na barua za utambulisho ili wakose sifa za kusimamia uchaguzi mdogo wa Februari 17, mwaka huu. Inadaiwa kwamba polisi walitumia risasi za moto kusambaratisha maandamano hayo.

Tangu Akwilina alipopigwa risasi ni takriban miezi saba sasa. Mhusika aliyesababisha kifo chake hajapatikana na zaidi polisi wametangaza kufunga jalada, kwa hiyo upelelezi hauendelei. Hii ni alama ya wazi kwamba aliyemuua mwanafunzi huyo hatapatikana tena. Je, thamani ya uhai wake imepewa uzito kiasi gani?

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, Septemba 7, mwaka jana, alipigwa risasi akiwa kwenye gari, kabla hajashuka nyumbani kwake. Baada ya shambulio hilo Lissu alipewa matibabu Hospitali Mkoa wa Dodoma, Nairobi, Kenya na sasa anaendelea kutibiwa Brussels, Ubelgiji.

Tangu kutokea kwa shambulio hilo, hakuna mtu yeyote aliyewahi kuripotiwa kukamatwa kuhusiana na tukio hilo. Shambulio la Lissu ni dhahiri lengo lake lilikuwa kumuua. Tukio lilitokea mchana na waliolitekeleza walifanikiwa kutoroka pasipo bughudha yoyote. Je, watu wanaweza kupata urahisi wa kuujaribu uhai wa mtu kiasi hicho?

Columnist: mwananchi.co.tz