Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tekonolojia mpya uhifadhi wa nafaka itamkomboa mkulima

13502 Mkulima+pic TanzaniaWeb

Fri, 24 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Licha ya kwamba kilimo ndio uti wa mgongo wa Taifa, wakulima wengi bado wanatumia mbinu duni kuhifadhi mavuno yao.

Mbinu hizo ni pamoja na maghala ya kienyeji ambayo huyaweka mazao katika hatari mbalimbali ikiwamo ya kushambuliwa na wadudu waharibifu.

Pia, mazao mengi yameendelea kupotea kuanzia kipindi cha uvunaji, usafirishaji, uanikaji hadi kwenye uhifadhi.

Inakadiriwa kuwa kati ya asilimia 30 hadi 40 ya mazao yanayovunwa na wakulima hasa nafaka hupotea kabla hayajafika sokoni kutokana na uhifadhi duni na ubebaji usiozingatia usalama.

Inaelezwa kuwa wakulima wengi hutumia dawa za viwandani kunyunyuzia mazao hayo ili yasiharibike bila kujua baadhi ya kemikali zina madhara makubwa kwa afya ya binadamu.

Kutokana na changamoto hiyo, wataalamu wa Chuo Kikuu cha Purdue cha Marekani waliamua kufanya utafiti wa kupatikana kwa nyenzo bora ya kuhifadhi mazao, ndipo wakaja na teknolojia ya mifuko ya waliyoiita, Purdue Influede Crops Storage (Pics)

Mifuko hiyo ilibuniwa nchini Ivory Coast na Guine Bissau miaka 10 iliyopita kuhifadhia choroko.

Na sasa mifuko hii inatumiwa na baadhi ya wakulima kuhifadhi mazao na kusafirishia katika baadhi ya nchi za Afrika na zile za mashariki ya mbali kwa ufadhili wa taasisi ya Melinda and Gates Foundation.

Utengenezaji wake

Mifuko hii imetengenezwa ikiwa na tabaka tatu na unatumika kuhifadhi nafaka kavu bila kutumia kemikali ya aina yoyote.

Meneja mradi kiwanda cha Pee Pee Tanzania Limited (PPTL) kilichopo mkoani Tanga, Ladislaus Ngingo anasema,

“Teknolojia ya mifuko hiyo haikuishia kwenye kuhifadhi choroko pekee, bali ilijaribiwa kwenye nafaka nyingine kavu na kuwa na majibu chanya,” anasema Ngingo.

Anasema kwa Tanzania teknolojia ya utengenezaji wa mifuko hiyo ambayo ilianza kutumika 2014 na kiwanda kinachozalisha vifungashio na mifuko cha PPTL baada ya kupatiwa kibali.

Teknolojia hiyo imekuja na ubunifu wa mifuko hiyo ya kinga ya njaa maarufu Pics, ni maalumu kwa ajili ya kuhifadhi mazao bila kutumia kemikali.

Ngingo anasema anasema mifuko hiyo ni mkombozi wa mkulima kwasababu sasa hatatalazimika kutumia kemikali tena kwa ajili ya kuhifadhi mazao yake.

“Mifuko hii imekujaa maalumu kwa ajili ya kuachana na matumizi ya kuhifadhi mazao kwa njia ya kemikali kwa kuwa sasa mkulima ataweza kuhifadhi mazao yake katika mfuko maalumu ambao haupitishi hewa na kuruhusu mdudu wa aina yoyote kupenya,” anasema Ngingo.

Katika maadhimisho ya sikukuu ya Wakulima (Nane nane) yaliyofanyika kitaifa mkoani Simiyu, mifuko hiyo ilikuwa kivutio si tu kwa wakulima pekee, bali hata wafanyabiashara wa nafaka. Wengi walisema ni mkombozi aliyeletwa nchini kuwakomboa namna ya kuhifadhi nafaka zao.

Katika banda la Wizara ya Kilimo, Wakala wa Chakula Tanzania na taasisi ya World Food Program (WFP), waliitangaza mifuko hiyo. Na banda la mifuko ya Pics lililokuwa bize muda wote, kipindi chote cha maonyesho.

Matumizi yake

Ngingo anasema tofauti ya mifuko ya Pics na mingine ya salfeti, hii imetengenezwa maalumu kwa ajili ya kuhifadhia nafaka kavu kwa zaidi ya miezi sita na nafaka zikaendelea kubaki katika ubora wake kama zilivyovunwa shambani.

“Kila mfuko wa pics una nailoni mbili nzito ndani kila moja ikiwa na ‘macron’ 80, maalumu kwa kuhifadhi nafaka kavu,” anasema.

Meneja huyo anasema uhifadhi wa nafaka kwa kutumia mifuko hiyo ni tofauti na ule uliozoeleka wa kutumia dawa kuchanganya na nafaka.

Ngingo anasema kabla ya kuipeleka mifuko hiyo kuitangaza kwenye maonyesho hayo, waliifanyia majaribio kwa miezi sita kabla ya maonyesho hayo na hakuna mfuko ulioingiza wadudu waharibifu wa nafaka kavu.

Wakulima

Mkulima wa mahindi na maharagwe kutoka mkoani Tabora, Helena Magere anasema, “Nimekuwa mtumiaji mzuri wa mifuko hii Pics tangu 2015 nilipoikuta kwenye maonyesho ya Nane nane ya 2015. Sikuwa naifahamu kabla, niliinunua michache kwenda kuijaribu kusudi nijionee mwenyewe ni kweli ni hifadhi nzuri ya nafaka.”

Anasema ameachana na uhifadhi wa mazao yake kwenye vihenge na kuyatia dawa na sasa anahifadhi kwa kutumia mifuko hiyo.

“Sina presha sasa ya kuhifadhi mazao yangu kuharibika, hata baada ya msimu kupita au soko kutopatikana,” anasema Magere.

Mkulima mwingine, Bwire Shija wa Lamadi anasema ujio wa mifuko hiyo nchini utawasaidia pia kuuza mazao yao kwa bei ile ile tofauti na awali, walilazimika kuuza kwa bei ya chini ili kwa kuhofia kuharibka.

Ngingo anasema kabla ya kuisambaza mifuko hiyo walifanyia majaribio ya matumizi yake katika vijiji 4,000 vya mikoa tisa nchini.

“Tulipata ushirikiano kwenye Serikali za vijiji, uliitishwa mkutano wa kijiji tukagawa mfuko mmoja katika kila kijiji na mkulima aliyepatiwa alielekezwa jinsi ya kuhifadhi nafaka na wengine walishuhudia.

“Baada ya kumaliza tuliandika tarehe ulipojazwa nafaka kavu juu ya mfuko na ukahifadhiwa na baada ya miezi sita tuliwaambia wafungue.”

Meneja Masoko wa Pics, Thomson Mwakibinga anasema inapatikana kwa mawakala wao ambao ni wauzaji wa Pembejeo za kilimo.

“Ila bado tunachangamoto ya kuifikisha kwenye ngazi ya vijijini, japo inafika, lakini kwa bei kubwa ambayo si elekezi kutoka kwetu.

Anasema mfuko mmoja unaweza kuhifadhia nafaka kavu kwa miaka mitatu mfululizo bila kuharibika.

Hata hivyo, anasema kwa sasa wanajiandaa kuisambaza mifuko hiyo vijijini ili kuwabana wajanja wachache wanaowaibia wakulima kwa kuwauzia kwa bei kubwa tofauti na ile elekezi iliyotolewa na kampuni yake.

Meneja huyo anatoa shime kwa wakulima nchini kugeukia uhifadhi huo wa kisasa na usio na gharama kubwa kama ilivyo kwenye uhafidha mwingine.

Anasema uhifadhi huo unamsaidia mkulima mdogo kupata uhakika wa mazao yake kama alivyoyavuna shambani bila kuathiriwa na wadudu.

Hata hivyo anasema licha ya mifuko hiyo kuzalishwa nchi kwa sasa, bado mwitiko wa matumizi yake ni mdogo tofauti na nchi za nje ambako kuna uhitaji mkubwa wa mifuko hiyo.

Columnist: mwananchi.co.tz