Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tanzania ni kubwa kuliko vyama vyetu vya siasa

9269 Mtatiro TanzaniaWeb

Wed, 1 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

“Nchi hii bila CCM hakuna maendeleo, sisi tukiamua yanakuja na tukiamua hayaji, na cha kutufanya hakipo.... Eeh, kwani wewe diwani ulivyokuwa Chadema tulileta kitu hapa? Waambie, tulileta nini? Hakuna! Hatuwezi kuleta, tunaletaje? Yaani tukuletee letee tu kienyeji hivi? Hatuleti! Na hatuleti kwa nini? Hatuwezi kuleta fedha kwa sababu wewe hukuwaahidi watu mambo hayo? Sisi tuliahidi shule, ukakataa shule....”

“...Tuliahidi zahanati, ukakataa zahanati, tuliahidi barabara, ukakataa barabara, sasa tunaleta fedha za nini? Kitendo cha kumchagua diwani wa Chadema maana yake umekataa mipango ya nini, ya CCM, sasa unailaumu CCM kutokuleta maendeleo, wewe pambana na hali yako bwana, utauza vitumbua na mwisho utauza na kigoda cha kupikia vitumbua, (wanawake wanashangilia), adui mwombee njaa......!”

Hii ni sehemu ya hotuba ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM – Taifa), Kheri James ambayo ameitoa kwenye moja ya kata zinazojiandaa kufanya uchaguzi wa marudio mwezi Agosti mwaka huu. Na hotuba hii ndiyo nitaitumia kujenga hoja ya leo, hakika siyo kwa kumjadili Kheri James, lakini kujadili hoja yake na hoja zinazofanana na hiyo.

Hoja za zama za kale

Ukiisikiliza hoja ya Kheri James na ukitizama anavyoongea kwa kujiamini na mambo anayoyaongea, ndipo unaweza kutambua mustakabali wa taifa letu, vijana lilio nao kwenye kujifunza uongozi wa leo na watu wanaotegemewa kushika nyadhifa kubwa siku zijazo, hapo ndipo unaweza kujua mwelekeo wa taifa.

Hotuba hiyo ukiisoma, huwezi kuitofautisha na hotuba zilizokuwa zinatolewa na vijana na wana propaganda waliokuwa wanampigania Hitler kule Ujerumani, Mussolini kule Italia, De Clerk na uongozi wa kikaburu kule Afrika Kusini. Ni aina ya hotuba iliyojaa dharau kwa wanaopewa ujumbe, majivuno makubwa na ubaguzi wa hali ya juu.

Ni hotuba ambayo inawaandaa vijana wa CCM kuamini kuwa CCM ni kubwa kuliko taifa la Tanzania, ni kubwa kuliko wananchi, ni kubwa kuliko Katiba ya nchi na sheria zake, ni kubwa kuliko haki za msingi za raia na kwamba ni kubwa kuliko utu wa Watanzania.

Heri ya Kheri kuliko tatizo lenyewe

Tatizo kubwa kuliko yote siyo Kheri, namaanisha siyo huyu mwenyekiti wa UVCCM, tatizo kubwa ni wale waliomfunda kuwa hiyo ndiyo hotuba atakayokwenda kuwaeleza wananchi. Tatizo ni kubwa kwa sababu haiba hii ya mwenyekiti wa vijana, ndiyo haiba waliyonayo pia vijana wengi wenye dhamana mbalimbali ndani ya chama hicho kinachoongoza dola.

Tatizo kubwa zaidi kuliko yote tena ni wale wanaowafunda vijana hao kuwa viongozi, kwamba wala hawawaandai kuwa viongozi, wanawaandaa kuwa kina Hitler, Musolini, Idd Amin, Makaburu na kina Mobutu Seseseko.

Ikiwa leo kijana wa kimasikini anasimama mbele ya Watanzania wanaolipa mabilioni ya kodi ili nchi yao isonge mbele, kisha anawaeleza maneno hayo bila kujishtukia wala kuwa na mishipa ya aibu, ati kwa sababu yeye ni mwana CCM mwenye cheo – ndipo mtambue kuwa tunajenga taifa lenye vijana wenye ujasiri uliojaa dhambi na mauti.

Nataka kurudia kwamba, hiki anachokifanya mwenyekiti wa UVCCM ndiyo picha halisi ya nini wanafanya vijana walioko chini yake huko ndani ya UVCCM na chama chenyewe.

Kwa mfumo wetu mbovu wa kiuongozi na kiutawala, ambao kwa sasa unazidisha kasi ya chama kinachoongoza kushikamana na kudhibiti vyombo vya dola na mihimili mingine ya dola, na kwa utaratibu wa fikra hizi za vijana ambao kwa mfumo wetu ndani ya miaka miwili mitatu ni vijana hawa ndiyo wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na mawaziri – hebu fikiria Tanzania ya vijana wa namna hii itakuwa ya namna gani?

Tusisahau chanzo cha matatizo

Mwaka huu 2018 mawaziri kadhaa walijitokeza hadharani (akiwamo waziri wa Afya, Ummy Mwalimu), kuwakanya wakuu wa wilaya na mikoa wasiwaweke watendaji wa serikali mahabusu bila kufuata utaratibu wa kisheria.

Tangu serikali ya awamu ya tano imeingia madarakani tumeshuhudia watendaji wengi wa serikali wakisimamishwa kazi au kuwekwa mahabusu kwa amri za Ma DC na RC kwa sababu tu watendaji hao walishindwa kujibu maswali au walipishana nao mitizamo.

Wengi wetu tulipigia kelele tabia hiyo, tukisisitiza kuwa ni tabia ambayo inavunja haki za watendaji wa serikali, inavunja sheria na katiba yetu, na nadhani mawaziri wenyewe uzalendo uliwashinda.

Kumbe basi, tabia hiyo ya wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa, kuamini kuwa wao ni wakuu kushinda utu wa watu wengine, kuamini kuwa CCM ina nguvu kuliko haki za Watanzania na kuamini kuwa ukiwa kiongozi wa chama tawala wewe ni bosi wa kila mtu, ni imani ambayo vijana hawa wanajengewa tangu wakiwa wanajifunza uongozi, na hakuna mtu wa kuwakanya.

Mafunzo ya siasa hizi za kinazi yanawafanya vijana hawa wanaamini kuwa bila CCM hakuna Tanzania, na wanaamini kuwa wana wajibu wa kuipigania kwa gharama zote hata zile zinazovunja utu wa watu, haki za watu, sheria za nchi, katiba ya nchi na misingi ya uanzishwaji wa taifa hili ya kupigania haki, usawa na kuondoa udhalimu na utwezaji – mambo ambayo Mwalimu Nyerere na waasisi wengine walihangaika nayo usiku na mchana.

Kuna CCM ngapi?

Nimemsikiliza Dk Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM akijenga hoja zake kule Buyungu, Kigoma, kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi wa marudio wa nafasi ya ubunge. Ukiisikiliza hotuba ya Dk Bashiru, halafu ukawasikiliza hawa vijana wanaofundwa ndani ya chama, unaweza kudhani kuwa CCM ni vyama viwili tofauti kabisa, kwamba kuna hii ya hawa wanaodhani ni kubwa kuliko taifa na kuna wale ambao wanadhani chama kina dhamana ya muda mfupi tu kwenye taifa.

Mfano wa Dk Bashiru unaweza kutokuwa mzuri sana kwa sababu yeye ni mtu mpya mwenye mamlaka makubwa ndani ya chama, na sisi ambao tumekuwa wanafunzi wake darasani tunamjua ni mtu wa namna gani – lakini labda iko CCM ya asili ambayo inawaaminisha vijana wake ufalme, ukuu, dharau, majivuno na imani za ajabu kama iliyomo kwenye hotuba hiyo niliyoinukuu.

Na baya kuliko yote ni je, huko ndani ya CCM wako watu ambao wana uthubutu na uwezo wa kuwafundisha vijana hawa kwamba chama chao ni kweli kinaongoza nchi lakini chama chenyewe siyo nchi? Je, huko ndani kuna mtu anaweza kuwakanya vijana hawa ya kwamba hata kama wanaamini CCM ni kubwa kuliko Tanzania basi wakae kimya wasitamke dharau na ujinga huo hadharani?

Vijana wa sasa wanasoma?

Vijana wa sasa ambao wanalazimisha hali hii, wamekaa darasani na kusoma vizuri kweli? Mbona kijana wa CCM anazo hoja nyingi za kwenda kuongea kwa wananchi? Ununuzi wa ndege, ujenzi wa reli ya SGR, elimu bila malipo, ongezeko la bajeti ya Serikali kuu, ukuta Mirerani, barabara mbili au tatu za juu, kuhamia Dodoma na mambo mengine mengi?

Haya mambo yote viongozi wanaojifunza uongozi kupitia CCM wanaweza kuyasoma kwenye nyaraka za serikali na wakaenda kuwafafanulia wananchi kwenye kata mbalimbali za uchaguzi ni jinsi gani maendeleo hayo yanabadilisha maisha ya wananchi hao wa vijijini sasa na baadaye.

CCM ina mambo mengi na hoja nyingi za kuzungumza na wananchi kuliko kuwatisha, kuwaonyesha kwamba wao (wananchi) siyo chochote, kuwaambia wananchi kuwa kuchagua chama kingine ni kujitenga na uongozi na maendeleo ya nchi na kuwatishia wananchi kuwa watauza vitumbua hadi kiama na vitumbua vikiisha watauza hadi vigoda vya kuuzia vitumbua hivyo.

Kwa kweli hizi si lugha za kuzungumza na Watanzania, na mbaya zaidi, hawa si vijana wanaoandaliwa kuliongoza taifa hili leo na kesho, vijana wa namna hii wangeliweza kuwa viongozi wazuri sana kwenye karne moja iliyopita siyo leo.

Tuendelee kujifunza kuwa Watanzania ni wakubwa kuliko CCM na kuliko chama chochote, Tanzania ni muhimu kuliko CCM kutawala milele kama ambavyo vijana hawa na wawafundishao wanaamini na kuapa hadharani.

Julius Mtatiro ni mchambuzi wa mfuatiliaji wa utendaji wa Serikali barani Afrika; ni mtafiti, mwanasheria, mwanaharakati na ni Mwenyekiti wa Kamati ya m CUF. Simu; +255787536759 (Whatsup, Meseji na Kupiga)/ Barua Pepe; [email protected])

Columnist: mwananchi.co.tz