Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaaluma ya Walimu, umewaibua wadau wa elimu, huku wakitoa mawazo tofauti kuhusu hatima ya chombo hicho kipya kinacholenga kusimamia taaluma ya ualimu nchini.
Awali muswada huo uliposomwa kwa mara ya kwanza bungeni na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, baadhi ya wadau wa elimu walisifu hatua hiyo, huku baadhi wakifikia hatua ya kusema kuwa bodi hiyo imechelewa.
“Tulitarajia mabadiliko haya yaletwe wakati wa (Serikali ya) awamu ya nne kutokana na umuhimu wake, kwani yanalenga kuleta usimamizi thabiti kwenye sekta ya elimu hasa kwa walimu wenyewe,” alisema Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiel Oluoch alipozungumza na Mwananchi siku za nyuma.
Mdau mwingine, Benjamin Nkonya ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Watoaji Elimu Wasiotegemea Serikali Kusini mwa Jangwa la Sahara (CIEPSSA), Benjamini Nkonya alisema: ‘’Mapendekezo ya muswada huu tuliyatoa mwaka 2008, lakini ndiyo inafanyiwa kazi leo, Serikali inapaswa kuharakisha utekelezaji wake ili kupunguza madhara yanayotokana na upungufu katika sekta yetu.’’
Miezi zaidi ya mitatu tangu muswada huo usomwe bungeni, wadau wa elimu wamekuja na mapendekezo tofauti.
Wakizungumza katika mjadala wa mapitio ya muswada huo uliofanyika wiki iliyopita jijini Dodoma, wadau walitaka kuwapo kwa marekebisho kuhusu utoaji wa leseni kwa walimu, ada ya leseni na kigezo cha kuangalia tabia kabla mwalimu hajasajiliwa na mwingiliano wa majukumu kati ya bodi na Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) iliyopo sasa.
Mwingiliano na TSC
Baadhi ya wadau wana hofu kuwa bodi mpya inaweza kuingilia majukumu ya Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC).
‘’Bodi inasajili walimu, TSC inasajili walimu, bodi inatoa namba za usajili na TSC inatoa namba, bodi inaadhibu walimu na TSC inaadhibu walimu….Majukumu ni yaleyale,’’ anasema Katibu wa Chama cha Kutetea Haki na Maslahi ya Walimu (Chakamwata), Meshack Kapange.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Benadetha Mshashu anasema ukiangalia maudhui yaliyomo katika sheria ya TSC ni kama sawa na yaliyomo katika muswada huo.
“Kama unasema kuwa TSC inashughulika na walimu walioko serikalini tu ina maana mwalimu huyu ameongezewa chombo kingine cha usimamizi,’’ anasema.
Hata hivyo, Waziri Ndalichako anasema bodi mpya ni chombo cha kitaaluma kitakachoshughulikia ukiukwaji wa taaluma kwa walimu.
Anaungwa mkono na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Peter Serukamba, anayesema wigo wa bodi ni mpana zaidi kuliko ule wa TSC kwa kuwa hauishii kwenye ufundishaji pekee kama ilivyo kwa TSC bali inasimamia taaluma kwa jumla.
‘’Bodi inahusika katika maeneo yote. TSC ni kwa ajili ya kushughulikia maslahi ya walimu, sio taaluma ya walimu,’’ anaeleza.
Faida za bodi
Wakati TSC iliwalenga zaidi walimu katika utumishi wa umma, bodi mpya imelenga walimu wote nchini bila kujali kama ni watumishi wa umma au katika sekta binafsi.
Mratibu wa Mtandao wa elimu (Tenmet), Cathleen Sekwao anasema Bodi hiyo ni kwa ajili ya kusimamia taaluma, maadili na weledi.
“Ni kama zilivyo bodi za wahandisi, wahasibu au madaktari. Lengo ni kuilinda taaluma yaualimu, kuipa heshima, nidhamu na weledi,” anasema na kuongeza kuwa sababu za kuundwa kwa bodi hiyo ni kutodhibitiwa kwa taaluma ya ualimu kiasi cha kuporomosha elimu nchini.
“Kuna matatizo yalitokea ambapo awali kulikuwa na kitengo cha utawala wa elimu kilichokuwa wizarani kilihamishiwa Baraza la Taifa la Ufundi (Nacte) linaloshughulikia elimu ya ufundi. Hilo lilikuwa ni kosa kwa sababu walimu walipewa vyetu vya ufundi wa elimu. Bodi ingekuwepo hilo lisingetokea,” anaeleza.
Anaongeza: “Kuna wakati kulikuwa na uhaba wa walimu, wakawa wanachukua wanafunzi waliomaliza kidato cha sita na kuwapa mafunzo ya miezi sita kisha wanakwenda kufundisha…. Bodi ingekuwepo hili lisingetokea. Siyo kila mtu anafaa kuwa mwalimu eti kwa sababu amesoma Kiingereza nchini Kenya.”
Pamoja na muswada wa kuanzishwa kwa bodi hiyo kusomwa kwa mara ya kwanza mwaka 2018, wadau wa elimu wanasema wazo hilo walishawahi kulipeleka serikalini miaka mingi iliyopita.
’Mapendekezo ya muswada huu tuliyatoa mwaka 2008, lakini ndiyo inafanyiwa kazi leo, Serikali inapaswa kuharakisha utekelezaji wake ili kupunguza madhara yanayotokana na upungufu katika sekta yetu,’’ anasema Nkonya.
Aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba anasema pamoja na kuunga mkono wazo la bodi hiyo, bado mchakato wake umegubikwa na maeneo yenye upungufu ambayo mengine walishawahi kuyapendekeza siku za nyuma.
Ana wasiwasi kuwa bodi mpya inaweza isiwe na matokeo chanya hasa kwa kuzingatia kuwa walimu wana kero nyingi ikiwamo ya kusimamiwa na mamlaka zaidi ya moja.
“Pamoja na kwamba majukumu ya Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) yanafanana na bodi itakayoundwa, mpaka sasa wamekataa kuweka mwajiri moja wa walimu. Jambo linaloombwa na CWT ni kuwa na chombo kitakachofanya kazi kama Tume ya utumishi wa Walimu ya Kenya,” anasema Mukoba.
Anaongeza: “Tatizo letu hapa mwalimu anaajiriwa na Wizara ya Tamisemi, analipwa na Wizara ya Fedha, anakaguliwa na Wizara ya Elimu, anapandishwa madaraja na na Tume ya Utumishi wa Walimu. Mwalimu akipata shida anazungushwa kote huko hadi apatiwe ufumbuzi. Hakuna tulichofanya ni kucheza makida makida tu.”
Akifafanua zaidi, Mukoba anasema wakati akiwa CWT walitembelea nchini Kenya kujifunza jinsi Tume ya walimu inavyofanya kazi ili kuiunda upya tume ya Tanzania. “Tuliporudi walikwepa kutengeneza sheria itakayoipa nguvu TSC kusimamia mambo yote ya elimu. Bodi hii ni kama kiboko cha Waziri wa Elimu, ndiyo maana tulitaka kuwe na mjadala wa kitaifa kuhusu elimu, siyo kuja na kitu kimoja kimoja.”
Kuhusu walimu kupewa leseni, Mukoba anasema sheria hiyo inapaswa kueleza mwalimu apewe kwa sababu gani.
“Hiyo leseni walimu wanalipia ya nini kama mtu anafanya kazi hapewi semina au mafunzo ya kujiendeleza? Kwa sababu siku zote hawatoi mafunzo kwa sababu hawana fedha, labda sheria iseme hizo ada za leseni ndiyo zitatumika kutoa mafunzo,” anasema.
Kwa mujibu wa muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaaluma ya Walimu, bodi itakuwa na jukumu la kuinua kiwango cha taaluma ya ualimu na kupata walimu mahiri, kuanzisha na kutunza mfumo wa usajili wa walimu, utoaji wa leseni za kufundishia kwa walimu, kuweka vigezo na viwango. Muswada huo ambao awali uliwasilishwa bungeni Mei 2 na Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako unaainisha masharti kuhusu usajili wa walimu, vigezo vya usajili, aina za usajili, ulipaji wa ada za usajili, utoaji wa leseni na kuweka masharti na namna ya kuweka na kutunza orodha ya walimu. Vilevile unapendekeza kuweka masharti kuhusu utaratibu wa kuondoa jina kwenye rejista (orodha), kufuta na kusimamisha usajili pamoja na adhabu kwa makosa yatokanayo na kuajiri mwalimu asiyesajiliwa.