Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tafakuri: Kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli

12068 Pic+magu TanzaniaWeb

Wed, 15 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nikiwa kijana wa Kitanzania ninayependa maendeleo ya nchi yangu, sina budi kuunga mkono juhudi za kimaendeleo si tu za Rais, bali za Watanzania wote.

Nimemsikia mara kadhaa Rais John Magufuli akisema yeye ni rais wa Watanzania wote, haangalii vyama, dini wala kabila, kwamba yeye anawatumikia wananchi wote. Ni jambo la faraja kusikia maneno haya na pengine ndiyo maana Watanzania wote wanafanya kazi kwa bidii na kulipa kodi ili nchi iendelee.

Lakini, wakati mwingine ninachanganyikiwa na kushindwa kuelewa ninaposikia kiongozi anahama chama kwa sababu anaunga mkono juhudi za Rais. Huwa ninatamani nipate walau nafasi ya kumuuliza swali anieleweshe.

Ninatamani nipate walau nafasi ili niulize kama huwa wanamaanisha mtu akiwa nje ya chama cha Rais, huwa haungi mkono juhudi za maendeleo.

Huwa natamani niulize iwapo wanaowapigia kura watu hao wanakuwa wamekubaliana nao kuhusu “kutokumuunga mkono Rais”?.

Au nijue kama kabla ya kuhama, pale wanapokwenda kuomba kura wanawaambia nini wananchi hadi wanawachagua, halafu wanakuja kusema wanaondoka kumuunga mkono Rais.

Ninaomba nieleweke kuwa sina tatizo na mtu anayehama chama chochote kwa sababu ni haki ya kila mtu na ya kisheria, lakini ninachoshindwa kuelewa ni kauli ya “kuunga mkono juhudi za Rais”.

Hivi ni nani aliyetuambia ukiwa chama cha Rais wa nchi yako ni kuunga mkono juhudi za kimaendeleo. Hivi mnataka kutuaminisha kuwa watu wote ambao wapo nje ya chama tawala hawaungi mkono juhudi za Rais?

Mimi binafsi siwezi kukubali haya mawazo mnayotaka kuwapandikizia Watanzania, ninafahamu kwamba maendeleo anayoyaleta Rais yanapaswa kuungwa mkono na watu wa vyama vyote, dini zote, makabila yote na itikadi zote.

Kwa sababu kama mlienda kuomba kura kwa wananchi na mkawaeleza kwamba mna nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo huku mkiwa kwenye vyama vyenu vya kisiasa na Rais naye akaomba kura akiahidi maendeleo akiwa kwenye chama chake, basi wote mlikuwa mna nia moja ya kuwaletea wananchi maendeleo. Sioni hoja ya kusema unahama chama chako kwa sababu ya kuunga mkono juhudi za Rais kama ina mashiko.

Hoja yangu, kuhama kwenu kunailazimisha Serikali kila mara kutumia pesa kwa ajili ya kurudia uchaguzi kwa sababu zisizo za lazima, ingawa ni suala la kikatiba.

Katiba inatupa uhuru huo lakini tusiutumie kiholela, yaani itafika mahali mtu anaangalia chama kinachokubalika maeneo yale anajiunga na kugombea halafu akishapata uongozi anatangaza kurudi alipotoka kwa sababu tu katiba inaruhusu. Huu mchezo ni mchafu.

Ni jambo ambalo si la kutazama tu kwani kati ya Oktoba 2015 mpaka kufikia Septemba 16, zitakuwa zimefanyika chaguzi ndogo tano kwenye majimbo tisa na kata 86. Kuna sababu kadhaa za kurudia chaguzi hizo, wapo wabunge waliofariki dunia na walioenguliwa kwa sababu mbalimbali za kisheria.

Lakini, wapo wanaohama kwa sababu ambazo hazina mashiko kabisa ikiwemo hawa wanaotuimbia wimbo wa “kuunga mkono juhudi za Rais.”

Ninafahamu kuwa kuna uwezekano wa kuhama kwa sababu nyingine ambazo sio za msingi kwa sababu wapo pia wabunge waliohamia vyama vingine kutoka chama tawala lakini mimi ninapata shida na hii kauli ya “kuunga mkono juhudi”.

Rais mwenyewe husema kila wakati kwamba muda wa siasa umepita umebaki wa kufanya kazi, mbona ninyi mnatuendelezea siasa na kampeni za kila kukicha?

Wanasiasa muwe na msimamo thabiti, muwe na uhakika na mnachokifanya, kuweni na uhakika na mahali mlipo, acheni kujiendea kama watu mnaobahatisha.

Acheni kuwahadaa Watanzania. Sote tuna wajibu wa kushiriki kikamilifu kuliletea taifa maendeleo bila kujali vyama vya kisiasa, dini na makabila.

Kuunga mkono juhudi za Rais ni kukubaliana na kufanya kile ambacho anataka kufanya, kama anataka barabara ijengwe na wewe ukakubaliana naye, kama anataka kodi zilipwe, kama anataka reli ijengwe na wewe ukakubaliana naye, kama anataka hospitali ziwe na dawa na wewe ukakubaliana naye, kama anataka nchi hii itoke kwenye umaskini na wewe ukakubaliana naye huko ndiko kumuunga mkono Rais hata kama upo chama kingine.

Kuna uwezekano wa kuwepo watu waliopo katika chama chake lakini wakawa hawakubaliani naye au wanarudisha nyuma juhudi za Rais. Kwani hujasikia mawaziri wakitumbuliwa kwa kuonekana kushindwa kumridhisha katika utendaji wao. Kwani hao hawapo chama kimoja naye? Hameni vyama, ni haki yenu lakini msituhadae kwa kauli ya “kuunga mkono juhudi”.

Mwandishi ni mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 067239558

Columnist: mwananchi.co.tz