Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TUONGEE KIUME: Watoto wa kike wanatusahaulisha kuwa tunaO PIA watoto wa kiume

81082 Pic+kiume TUONGEE KIUME: Watoto wa kike wanatusahaulisha kuwa tunaO PIA watoto wa kiume

Mon, 21 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tunawachunga na kuwalinda sana watoto wa kike hadi tunasahau kama tuna vijana wa kiume pia, hii si nzuri tena ipo kwenye ngazi zote, kuanzia kitaifa hadi familia.

Sikiliza televisheni, tazama redio, soma gazeti, ingia mtandaoni, ukikuta harakati hazihusu kulinda watoto kwa ujumla wao, basi lazima zitakuwa zinahusu kulinda watoto wa kike pekee, lakini kukuta za mtoto wa kiume kuna ugumu hili ni tatizo.

Majumbani mwetu tuna sheria lakini hazifanyi kazi kwa usawa kwa watoto wote. Binti akichelewa kurudi nyumbani ni vita kuu ya tatu ya dunia na ni tatizo kubwa kuliko deni la taifa, ni gharika zito kama upepo wa kisulisuli lakini akichelewa kurudi mtoto wa kiume hakuna tatizo, na hata likiwepo basi ni tatizo la kawaida sana, la kuambiwa maneno makali mawili matatu na likapita.

Tunaamini tunafanya hivi kwa sababu si kwamba tunawapenda watoto wetu wa kiume zaidi, hapana, bali tunaamini tunawalinda mabinti zetu tunaamini kwamba msichana yuko kwenye hatari zaidi ya kukumbwa na majanga kuliko mvulana. Lakini jambo ambalo labda tunashindwa kulielewa ni kwamba kwa sasa tunaishi dunia ya tofauti sana.

Mtoto wa kiume na wa kike, mvulana na msichana, wote wapo na viwango sawa vya kukumbwa na hatari katika ujana au utoto wao.

Kama unaogopa binti akichelewa kurudi nyumbani anaweza kukutana na manyang’au watakaomchezea na kumjaza ujauzito na kumtoa nje ya reli uliyokuwa unajaribu kumtengenezea.

Pia Soma

Advertisement
Basi unatakiwa pia uogope hivyo hivyo kwa mwanao wa kiume akichelewa kurudi huenda yuko sehemu anakula mihadarati na atarudi akiwa teja, anaiba na atarudi akiwa maiti kama sio mfungwa, ananunua kahaba na atarudi na gono kama sio kaswende na Ukimwi, anatumika kama mwanamke au mwanaume katika mapenzi ya jinsia moja na atarudi akiwa mtoto ambaye hutokuwa unajivunia hata kumtambulisha mbele za watu kuwa ni mwanao.

Anaweza pia akawa hayuko darasani kama alivyokuaga, na utagundua hilo akirudi na sifuri nyumbani.

Haya tunayoyazungumza hapa si hadithi za kubuniwa, kwa sasa tunaishi kwenye dunia ya namna hiyo. Fuatilia habari zinazoendelea mijini utaelewa. Hatuyasemi kwa sababu ya kutishana au ili kuifanya dunia ionekane ni hatari, hapana. Tunasema ili tuwe makini na kufuatilia nyendo za watoto wetu kwa karibu na kuwakumbusha namna ya kuwa mtu bora, kuwaeleza ukweli kwamba dunia haijawahi kuwa mbaya wala nzuri, dunia iko katikati, ambapo sasa walimwengu ndiyo huamua waipeleke wapi.

Wakiwa wabaya, inakuwa mbaya na wakiwa wazuri huwa hivyo pia.

Columnist: mwananchi.co.tz