Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TUONGEE KIUME: Wanawake na madada wa kazi ni kama wanasiasa na vyama

49659 Kelvin+kagambo

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wanawake na madada wa kazi ni wanasiasa na vyama.

Kwenye siasa tumeshazoea, si tatizo kabisa. Kwa mfano, historia inaweza ikaanza Lowassa akiwa mwanachama hodari wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Atazunguka nchi nzima, atakwenda Kaskazini Arusha kisha atarudi Kusini Mtwara, atapita Mashariki Dar es Salaam halafu atapanda treni hadi Magharibi Kigoma – kote huko anapita akiwahubiria Watanzania wenzake kwamba kama wanataka kuishi katika nchi ya ahadi waendelee kuchagua CCM.

Kisha kuna siku, ataamka na kututangazia kuwa nimehamia chama kingine cha siasa. Labda kwa mfano, atasema nimehamia Chadema. Na sababu atakayotuambia ni kwamba hana imani tena CCM, kwa hiyo kama na sisi Watanzania tunataka kuishi ndani ya Paradiso tukiwa hapahapa duniani, tuchague chama chake kipya, Chadema.

Miaka miwili mitatu itapita, mara asubuhi moja ataamka tena, atatutangazia kuwa amerudi CCM. Kwa sababu amegundua kuwa kumbe ndiyo sehemu halisi ya kutufanya Watanzania na Tanzania yetu iwe yenye maendeleo ya kustaajabisha.

Mfano huu ukitokea kweli kwenye siasa ni sawa kabisa. Kwa sababu kwenye nchi ya kidemokrasia unaruhusiwa kuhama chama cha siasa kadri utakavyo, kama Muumini Mwinjuma alivyokuwa akihama bendi za muziki.

Lakini wake zetu wameigiza hii tabia nyumbani – kila kukicha wanabadilisha madada wa kazi kama vyama. Na ukiuliza sababu, mara nyingi si ambazo zilikuwa na ulazima sana wa kufanya wanachofanya.

Jana mlikuwa na Mariam kutoka Kondoa, kesho atamtimua kwa sababu eti muda wote anashinda kwenye TV akizama tamthilia na Bongo Movie. Keshokutwa atamleta Neema kutoka Iringa, naye atakaa Jumatatu, Jumanne kisha Jumatano atamtimua, ukiuliza sababu utaambiwa hafanyi kazi, kutwa nzima anashinda akichezea simu mliyompa kwa ajili ya kuwasiliana na nyie mkiwa kazini. Kisha Ijumaa atakwambia anakwenda kumpokea Fatuma kutoka Mtwara, naye atakaa wikendi tu kisha atarudishwa kwao Namtumbo kwa makosa ya kufanana na wenzake waliotangulia.

Labda hizo sababu zote ni za kweli, lakini wanachoshinda kuelewa ni kwamba, tatizo lao mara nyingi wanachukua dada wa kazi wenye umri mdogo, ambao hawajawahi kufanya kazi sehemu yoyote kabla, na hata hawana hamasa ya ndani inayowasukuma kufanya kazi, yaani hawana watoto wanaosomesha wala hawana kodi za kulipa, ni watu ambao mara nyingi wanafanya kazi kama ratiba tu hivyo ule umakini wa mfanyakazi kwa ofisi yake hauwezi kupatikana.

Na isitoshe hawa madada wa kazi wametoka vijijini huko, kwenye maisha magumu kiukweli ambako hakuna bomba la maji, hakuna umeme, hakuna TV wala simu binafsi za mkononi. Kwa hiyo anapokuja kwako na kukuta kuna TV na king’amuzi kilicholipiwa mwezi mzima, hiyo kwake si nyumba, ni peponi, kwahiyo atahakikisha anaitumia fursa ambayo aliikosa miaka yote tangu kuzaliwa kwake.

Ninachosema ni huenda kosa linaanzia kwa namna tunavyowapata hawa wadada wa kutusaidia. Lakini suala la kubadilisha kama vyama si zuri sana kwa sababu kuna siku tutaajiri majambazi watusaidie kazi majumbani mwetu.



Columnist: mwananchi.co.tz