Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TUONGEE KIUME: Tuwaache watoto wetu watimize ndoto zao

58470 Kelvin+kagambo

Mon, 20 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Karibu kila mzazi anatamani mwanaye awe kama Mbwana Samatta, Barack Obama, Diamond au Billgate — hapa tunaongelea kiwango cha mafanikio. Na waswahili wanakwambia, hakuna mtu anayependa ufanikiwe kweli kama mzazi wako. Wengine wanapenda ufanikiwe ndio, lakini sio ufanikiwe kuwazidi wao.

Na mzazi naye anapenda ufanikiwe kwa sababu nyingi, lakini moja ya sababu kubwa ni kwamba mafanikio yako ni yao. Yaani anaamini ukiwa na nyumba nzuri, kuna uwezakano mkubwa wa yeye kutoka kwenye kinyumba anachoishi sasa hivi, kuja kuishi ndani ya kasri lako. Au atibiwe kwenye hospitali nzuri akiumwa kwa sababu tu mwanaye aliyekusomesha kwa jasho lake uko vizuri kiuchumi.

Mafanikio si kitu rahisi na ndiyo maana si kila mtu anayo. Na ubaya ni kwamba, unapozungumzia mafanikio, kila mtu anayapima kulingana na malengo yake au mtazamo wake.

Kwa mfano, unakuta una ndoto ya kwamba hadi kufikia mwaka 2025 uwe mfanyabiashara unayemiliki kiwanda au kampuni ya nguo yenye thamani ya bilioni moja. Lakini hadi mwaka 2024 unaweza kuwa uko nusu ya hapo.

Kwa wanaokutazama nje wanaweza sema umefanikiwa, lakini wewe binafasi ambaye unajua malengo yako unaelewa zaidi umesimama sehemu gani, kwamba bado kuna jambo la ziadi unahitaji kulifanya.

Hapa najaribu kukupa picha ya kukuelewesha kuwa watoto wetu nao wana malengo na ndoto zao kubwa, lakini wengi bado hawajazifikia. Ingawa kwa nje, akina sisi tunaona tayari wanaishi nchi ya ahadi kwa sababu hatujui undani wa nchi ya ahadi wanayoitafuta.

Pia Soma

Sasa tatizo linakuja kwa wazazi wengi, hasa wanaume kwa watoto wetu wakiume kwa mtazamo wetu, tunataka kuanza kufaidi matunda makubwa ambayo unakuta kumbe yako nje ya uwezo wa mtoto, yaani hawezi kumudu kwa huo. Au hata kama anaweza kumudu, basi anaweza kupitia anguko baada ya hapo.

Yaani mfano, kama mtoto ana milioni 30 ya kuboresha biashara yake. Na wewe unatamani akujengee nyumba. Akikujengea maana yake unataka biashara yake ibaki palepale ilipo, maana yake asiendelee, au asifanikiwe kama mafanikio kwake ni kuboresha biashara.

Kama mfano huo ni mzito, ushushe hata kwa daraja ya kununuliwa shati jipya na mtoto anayefanya biashara ndogo ya mtaji kiduchu.

Hatusemi unakosea kutamani vizuri kutoka kwa mtoto, ni haki yako kwa sababu hata Mungu anawakumbusha watoto kuwatunza wazazi wao. Lakini ni vizuri zaidi kama hautaharakisha hilo litokee mapema kabla mambo ya mwanao hayajasimama kisawasawa.

Wenzetu— kwa maana ya mama. Wanawaelewa sana watoto wao na ndiyo maana hili huwezi kuliona kwao. Wanaelewa, wanaheshimu na wanawapatia watoto wao muda.

Tuwape vijana wetu na mabinti zetu nafasi ya kufanya ndoto zao ziwe kweli. Mambo yakikaa vizuri, tutafaidi. Hakuna mtoto anayependa kumuona mzazi wake juu ya mawe — watatusaidia.

Columnist: mwananchi.co.tz