Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TUONGEE KIUME: Tatizo ni tabia zetu sio simu

50940 Pic+simu

Mon, 8 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mke: Baba John, simu yako imeingia meseji.

Mume: Isome, inasemaje.

Mke: Inatoka kwa Kasimu Gereji, anasema hajaona siku zake.

Mume: Mwambie nimeziacha kwenye siti ya nyuma ya gari, aangalie vizuri.

Huku kunaitwa kujitoa akili kwa kiwango ha lami.

Unajua, mwanzo simu ilikuwa ni kama anasa. Ilikuwa inauzwa bei mbaya ambayo si kila mtu alikuwa anaweza kumudu, kwa hiyo hata ukinunua, utakuwa na uwezo wa kuwasiliana na watu wachache sana, tena wasio na umuhimu kwa kiasi kikubwa kwenye maisha yako, hapo ndipo uanasa wake ulipotokea.

Lakini baadaye wakatutengenezea nyingi na wakatupunguzia bei, ikawa karibu kila mtu anayo, sasa ikawa ukinunua simu unaweza kuwasiliana na kila mtu unayemtaka, simu ikawa moja ya kifaa muhimu sana kati ya vingi vilivyowahi kugundulika chini ya jua.

Lakini tangu simu kubadilika kutoka kuwa anasa kuwa kifaa muhimu, imeharibu mahusiano ya watu wengi.

Na ninaposema mahusiano namaanisha ya kila namna, ndoa, uchumba, urafiki, undugu, biashara, kazi na kadhalika.

Kuna watu wamepoteza wateja, kwa sababu tu waliwatumia meseji mbaya kwa makosa, kuna watu wamepoteza ajira kwa sababu meseji ya kutokwenda kazini waliyomtumia bosi, haikufika kutokana na tatizo la mtandao na wenyewe hawakuwa wakifahamu.

Na kuna ndoa za watu zimeharibika kwa sababu mchepuko uliwatumia meseji wakiwa wamesharudi nyumbani, wake au waume zao wakaziona. Simu imekuwa tatizo.

Sasa tukisema tuache kutumia simu itakuwa ni upunguwani kama mlevi aliyesoma makala kwenye gazeti inayohusu madhara ya pombe, kisha akatoka kwenda kumwambia mwenzake. “Aisee nimeona gazeti limeandika madhara ya pombe, kumbe ina madhara mengi kiasi hiki. Naapa kwa Mungu kuanzia leo, sitasoma tena gazeti.”

Hatuwezi kuacha kutumia simu kwa sababu ina faida kuliko madhara.

Na hata madhara mengi yanayotokea si kwamba yanasababishwa na simu moja kwa moja, ni sisi wenyewe ndiyo tunasababisha hayo madhara.

Tuna tabia za ajabu. Hatujui kutulia na hatujui kulinda mahusiano yetu. Na kuna muda tunafanya kuyaharibu huku tukiamini tunaweza kutumia njia zilizotengenezwa kuyaharibu lakini yasionekane yanaharibika.

Mfano passwedi ngumu ngumu kama namba za kirumi, tunaamini tunaficha yaliyomo yasionekane – kweli hayaonekani lakini uharibifu unaendelea chini chini na inakuja kuonekana siku mambo yakiwa yamefikia pabaya, hapawezekani kurekebishika.

Simu sio tatizo, bali tatizo ni sisi wenyewe, kwa hiyo ni vyema kabla hatujanunua simu mpya na kusajili namba nyingine ya simu, tununue tabia mpya kutoka kwenye maganda yake na tujisali kwenye chama cha wanaojua kulinda mahusiano ya namna zote.



Columnist: mwananchi.co.tz