Kuku wa kienyeji kwa mbio hana mpinzani —lakini ukimfunga kamba mguuni kwa muda mrefu, kisha ukamfungua hatokimbia. Atakaa palepale alipokuwa muda wote kwa sababu akili yake inamwambia bado amefungwa kamba.
Ndio shida tunayopitia wanaume kipindi hiki. Ukifungua gazeti unakumbana na tafiti za jinsi wanaume wa sehemu fulani wanavyoongoza ligi ya tatizo la upungufu wa nguvu za kiume.
Ukiwasha redio, utasikia mahojiano na anayejiita daktari bingwa wa tiba mbadala, anataja namba zake za simu na ilipo ofisi yake ili wanaume wote wenye tatizo la upungufu wa nguvu za kiume wakamuone, ana dawa inayotibu kwa kutoa matokeo ya haraka kama chumvi, ndani ya siku tatu tu unapona kabisa.
Ukiwasha TV, tangazo lingine hili hapa. Mtabibu mwingine anaelezea namna ya kumaliza tatizo la upungufu wa nguvu za kiume kwa dawa alizozitengeneza kwa kutumia matunda na mitishamba baada ya kuzifanyia utafiti wa miaka minne.
Utachoka; utasema utoke nje, huko utakutana na kibao kimebandikwa kwenye nguzo ya umeme, kinasomeka; Dokta Mfumalanga kutoka Handeni. Anatibu nguvu za kiume… kisha namba ya simu chini ya maneno hayo kwa ajili yako kumpigia, upate dawa.
Ukiingia kwenye mitandao ndiyo utapotea kabisa, kila sehemu habari ni wanaume na tatizo la upungufu wa nguvu za kiume siku nzima. Tatizo linazungumzwa kwa herufi kubwa kana kwamba ni tatizo kubwa kuliko tatizo lolote kuwahi kutokea Tanzania.
Pia Soma
- Dalili za mwanaume aliyemchoka mpenzi
- ANTI BETTIE: Binti huyu amenitongoza, je anafaa kweli kuwa mke wangu?
- USHAURI WA DAKTARI: Mambo yanayoweza kuharibu ujauzito
Hata juzi kuna waziri alikuwa anatushawishi Watanzania tununue korosho za Kusini zilizoko ghalani kwa sababu inasemekana zinaongeza nguvu za kiume.
Cha kujiuliza ni je, kweli hili tatizo lipo kwa namna linavyozungumzwa, au ni vile linaongelewa kwa kupakwa rangi na kunogeshwa sana kiasi kwamba linaingia kwenye vichwa vya watu kufikia hatua hata wasiokuwa na tatizo wanakuwa na mashaka na afya zao.
Isije ikawa siasa za kibiashara, kwamba watu wametengeneza tatizo ili wajifanye wana suluhisho, wachume pesa zetu.
Hii ndio kama stori ya kuku wa kienyeji tu, tunafungwa kamba kwa kulishwa taarifa nyingi kuhusu afya zetu, ili hata siku wakitufungua, tusiende kokote, tuwe chini yao.