Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TUONGEE KIUME: Neno nakupenda na mke wako

68626 Kelvin+kagambo

Sun, 28 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kuna hii hadithi! Kiongozi mmoja wa nyumba ya ibada alifanya mazungumzo maalum na wanaume wanaosali hapo. Walikuwa takribani wanaume 30, na wote walikuwa wanaishi ndani ya ndoa.

Kabla hajazungumza akawaomba wote wenye simu wazishike mikononi, wakafanya hivyo bila kuelewa ni kwa nini. Kisha kiongozi akawaambia, ‘naomba mwende kwenye sehemu ya kuandika ujumbe mfupi. Na muandike hivi, Nakupenda.’

Wanaume wote wakafanya hivyo. Kiongozi akawaambia tena, ‘tumeni huo ujumbe kwenda kwa wake zenu’ bila woga wala wasiwasi, wanaume wote wakatuma.

Baada ya kuhakikisha kila mwanaume ametuma, kiongozi akaomba wasubiri kwa dakika moja ili huo ujumbe mfupi ujibiwe, kisha atampa fursa mmoja baada ya mwingine asome jibu alilopata kutoka kwa mkewe.

Jibu la kwanza liliposomwa lilikuwa limeandikwa. “Baba Sara. Huu ujumbe ulikuwa unamtumia nani?”

Nyingine ikasomwa; “Utakufa kwa umalaya mwanaume wewe.”

Pia Soma

Nyingine. “Mungu ameanza kukuumbua. Ulidhani utanificha siku zote. Kwamba milele daima sitojua uasherati unaoufanya?” Nyingine ikafanana na hiyo, na nyingine na nyingine na nyingine. Yaani majibu karibu yote yalikuwa yale yale.

Kwa nini? Kwa sababu wake wa wanaume wote waliokuwa pale hawakuzoea kupokea ujumbe mfupi wa namna ile kutoka kwa wenzi wao. Kimsingi neno nakupenda kutoka kwa mume kwenda kwa mke halistahili kuwa ‘breaking news’. Linatakiwa kuwa jambo la kawaida kwa sababu ndoa inaumbwa na upendo, na upendo unadhihirika kwa namna mbili tu, vitendo na maneno.

Vitendo ni uwanja mpana lakini maneno ni uwanja mpana zaidi na wenye nguvu kwa sababu kwenye kuzungumza kila kitu kinawezekana, kwenye kuzungumza unaweza kujiua kama ukiachwa na mpenzi wako, lakini ukiachwa na mpenzi wako kwa vitendo, kujiua sio jambo rahisi. Kwenye kuzungumza unaweza kumpeleka mkeo ‘shopping’ Dubai kila wikiendi, lakini kwenda shopping Dubai kila wikiendi kwa vitendo ni mtihani mgumu.

Maneno ni silaha kubwa lakini ni kwa wanaume wengi wa Afrika au tuseme tu Tanzania si desturi yetu hivi. Wengi tuna tabia kama wavuvi wanaotumia ndoano. Mvuvi wa ndoano hutumia chambo kwa jambo moja tu, kumvutia samaki. Samaki akishawishika, akanasa, basi kazi ya chambo imeisha. Wanakwambia, samaki kashavuliwa, chambo ya nini?

Kabla ya kumpata mwanamke wanaume tunatumia kila kitu kinachoitwa kizuri. Maneno mazuri, matendo mazuri, nakupenda nyingi na ahadi kibao, lakini ukishakamata mzigo na kuweka ndani hayo mambo hayapo tena.

Mtazamo wetu ni kama vile ukioa mwanamke ni kwa ajili ya kukupikia, kulea watoto na kukufulia, lakini mambo mazuri mazuri hayamfai, hayo ni kwa ajili ya vimada wetu, nje.

Ndo maana tukichukua simu kuwasiliana na wake zetu, ujue tunauliza kama luku imekwisha, fundi alikuja kutengeneza milango au kutoa taarifa kuwa leo nitachelewa kurudi nyumbani.

Hapana. Hawa wanawake wapo nyuma ya mafanikio yetu kwa kiasi kikubwa, wanastahili vitu viwili vikubwa, upendo na kuoneshwa wanapendwa.

Columnist: mwananchi.co.tz