Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TUONGEE KIUME: Majibu matatu ukiomba mkopo kwa ndugu, rafiki

67699 Kelvin+kagambo

Mon, 22 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kama mwaume shida inayohitaji pesa inakukumbuka ghafla, unatazama pochi yako haina kitu, simu yako ni nyeupe, unachungulia kwenye akiba yako kuna pesa lakini haifui dafu kwenye hili tatizo, tatizo lenyewe ni nene sana.

Unasema hapana, siishi jangwani, siwezi kufa mwenyewe tu wakati nina maswahiba zangu wa nguvu wanaoweza kunisaidia kama mimi ambavyo huwasaidia wanapokwama kwenye ishu kama hizi. Basi unachukua simu unaanza kuwapigia.

Wa kwanza anapokea, unamwambia ‘kaka nimekwama kidogo, nina shida ya laki moja, nitakurudishia Jumatano.’ anasema ‘Daaaah! Ndugu yangu umechelewa kidogo tu, sasa hivi nimetoka kumpa mtu laki moja, naye alinipigia alikuwa anataka kuongezea kodi. Yaani ungenipigia saa saba mchana, mbona yaani ingewezekana kabisa.’

Mwanaume mwenzako anapokupa jibu la namna hii usijisumbue hata kuendelea na stori za pesa porojo hii tunaitumia sana wanaume kumaanisha kwamba hatuna pesa hata kama ungepiga hiyo saa saba mchana kama anavyokwambia, angekwambia ungepiga saa tatu asubuhi ungepata na ungepiga saa tatu asubuhi, muda ungerudishiwa nyuma zaidi.

Basi unasema bado, ngoja nimpigie mwingine. Ile anapokea tu unamuelezea shida yako vizuri sana. Anakuelewa na sasa inakuwa zamu yake kukujibu. Mara anakuuliza ‘Mwisho saa ngapi? Au ni lazima sana kuipata sasa hivi?’. Unamjibu ‘kama nitapata saa hizi itapendeza lakini hata baadaye si mbaya.’

Hapo ukisikia umeambiwa. ‘Basi sawa. Kuna ishu naisikilizia, hadi jioni mida ya saa 11 hivi au 12 ikikamilika tu nakutumia kaka.’ ukisikia jibu la namna hii, nakushauri usiache ndoano zako hapo, chomoa, endelea mbele kajaribu kutafuta sehemu nyingine.

Pia Soma

Mwanaume akikwambia kuna mishe naisikiliza halafu nakutumia, anamaanisha amechoka vibaya kiuchumi tena ungechelewa kidogo kumuomba, ni yeye ambaye angekupigia kuomba umkopeshe. Kwa hiyo endelea mbele, katafute sehemu nyingine.

Mwenyewe unajipa matumaini, unakaa hadi saa 11 jioni kimya, unasema labda saa 12 jioni, nayo inapita bila simu wala meseji. Unampigia tena hapokei au akipokea anakwambia ile mishe haijakamilika.

Basi kwa sababu tatizo lako halijakwisha unaamua kumpigia mtu mwingine. Anapopokea tu unamuelezea kwa njia rahisi sana na anakuelewa. Na anapokujibu anakwambia ‘Pole broo. Sasa naomba kama dakika tano hivi nitakupa jibu.’

‘Nitakupigia kukujibu’ unapoambiwa hivi maana yake ni kwamba mimi sina hela ndugu yangu, sema hapa nilipo siwezi kusema sina hela hivyo nitakupigia baadaye kukujibu kwamba siwezi kukukopesha. Cha msingi unaposikia jibu la hivi pia endelea kufikiria namna nyingine ya kupata hiyo pesa, ila sio kwa huyu ndugu yetu.

Wanaume wa Kitanzania tuna porojo nyingi sana linapokuja suala la pesa, lakini hizi tatu ni miongoni mwa zinazoongoza kwa hiyo ni vyema ukazielewa.

Kanuni rahisi ambayo naweza kukupa ni kwamba, Watanzania hatuwezi au hatupendi kusema maneno mawili neno ‘sijui’ na ‘sina’.

Columnist: mwananchi.co.tz