Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TUONGEE KIUME: Hawapendi hela, wanapenda wanaume wenye hela

15140 Pic+wanaume TanzaniaWeb

Sun, 2 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wimbo wa Taifa wa wanaume wa Tanzania ndiyo huo; wanawake wanapenda hela ooooh! wanawake wanapenda hela jamani! Karibu kila mwanaume unayemgusa, ukimuuliza hupendi mwanamke wa aina gani? Atakujibu, “sipendi mwanamke anayependa hela” na ukimuuliza unapenda mwanamke wa aina gani atakujibu kuwa, “napenda mwanamke asiyependa hela.”

Na siyo kama watu wanazungumza hivi kwa kufuata mkumbo, hapana. Wana sababu za msingi kabisa. Hapo kila anayezungumza ni muathirika wa kunakoitwa kupenda hela kwa wanawake — wengine bado waathirika wapya, vidonda vibichi kabisa; na wengine wamebaki na makovu, waliyokumbana nayo baada ya kukutana na wanawake wapenda hela. Ni mazito. Hao nd’o hawataki hata kusikia kuhusu kuzihusisha hela zao na wanawake.

Huko kwenye mitandao ya kijamii, vijana wanakoshwa na machapisho ya aina mbili. Kwanza picha nzuri za wanawake na pili ni maandiko yanayowasema vibaya wanawake kuhusu kupenda hela — likiwekwa hilo la pili, linapata wachangiaji ‘kama wote’. Kila mtu anachangia uzoefu wa maumivu yake.

Wakati watu wazima wenye hekima wao wanaendelea kutafuta hela kwa sababu wanayatazama maisha kwa uhalisia sio nadharia. Wanaelewa hakuna mtu yeyote anapenda hela duniani; sote tunapenda huduma zinatokana na hela.

Ukitaka matibabu mazuri unahitaji kuwa nazo, kujenga nyumba nzuri, gari ya kisasa, nguo bora, kulea watoto vizuri, kula ujana na kila kitu kizuri utakipata ukiwa na hela. Cha bure kwenye dunia hii ni pumzi tu, hata salamu inalipiwa.

Ubaya sasa unakuja ili upate hela kuna mchakato mchungu na mgumu unatakiwa upitie; Yaani unatakiwa ufanye kazi, na mara nyingi kazi haifurahishi.

Unatakiwa uamke mapema asubuhi ujiandae kwenda kazini, na ili uamke mapema unatakiwa ulale mapema, maana yake nini, kama mwanamke aache kutazama tamthilia na Shilawadu ili kesho yake awahi kazini. Na ukifika kazini hakuna kulala, ni mchakachaka mwanzo mwisho, jumlisha makelele na matusi ya mabosi pasua kichwa — na ikifika muda wa kulipwa, ni vipesa kiduchu tu ambazo atanunua vigauni vitatu na kwenda saluni mara moja baada ya hapo anabaki mweupe kama sufi.

Sasa wanawake wakajiongeza; kwa nini wateseke kiasi hicho, watoe jasho kubwa kwa malipo yasiyolingana nguvu iliyotumika. Wakatafuta njia fupi ya kurahisisha maisha na wakaipata. Wakaanza kupenda wanaume wenye hela ili wapate huduma kwa urahisi na kila kizuri wanachokihitaji.

Hilo lilipokuja kwa wanaume tukalipokea vibaya tukiamini wenzetu wanapenda hela na kuanza kuwapachika majina.

Narudia wanawake hawapendi hela, wanapenda huduma zinazopatikana. Kwa hiyo kama unapenda mwanamke, hakikisha unapenda kutafuta hela pia. Achana na kuishi kwa nadharia kwamba anayekupenda hajali— hakuna aliyewahi kula mapenzi akashiba.

Columnist: mwananchi.co.tz